Profesa Issa Shivji |
BARUA NDEFU KWA KOMREDI PROFESA ISSAGULAMHUSEIN SHIVJI-(1)
S.L.P kijiji cha Namasakata,
Wilaya ya Tunduru.
Kwako Komredi Profesa Issa Shivji,Shikamoo!
Ni matumaini yangu u mzima wa siha njema na unaendelea vyema na harakati za
kutuamsha wanyonge tuliolala usingizi fofofowakati rasilimali na utajiri wetu
ukipokwa na mabeberu mamboleo kwa kushirikiana na ‘’makuwadi wa soko huria’’
kama alivyowaita swahibu wako mpendwamarehemu profesa chachage(Mungu ailaze
roho yake ya kizalendo mahala pema peponi).
Pia nichukue fursa hii adhimu
kukupongeza kwa jinsi unavyotumia kalamu yako kutukomboa kifikra sie
‘’wasakatonge’’ tulio kwenye kiza totoro.Naamini bado unakumbuka nasaha za mwalimu Nyerere alivyowaasa wanazuoni tarehe
27 June 1966 kwenye kongamano la wanazuoni pale chuo kikuu cha Dar es salaam(UDSM)
kwamba jukumu kuu la mwanazuoni wa chuo kikuu ni kuutafuta ukweli;kuuzungumza
kadiri anavyouona na kuusimamia kwa uthabiti bila kujali gharama yake. Je na
wewe upo tayari kuuzungumza na kuusimamia ukweli mpaka mwisho wa dahari?
Kwa hakika nafahamu kuusimamia ukweli
kuna gharama kubwa.Lakini nina hakika hakuna jipya linaloweza kumwandama
mzalendo yeyote ambalo wasemakweli wengine duniani hawajalipitia. Wanatheolojia
wanatujuza kwamba ‘’hakuna jipya chini ya jua’’.Kwa hakika ipo gharama ambayo
kila msemakweli duniani anapaswa kuilipa!
Ni hatari gani inayoweza kumkabili
msemakweli hapa duniani kushinda dhoruba ya mlipuko garini iliotupokonya
kipenzi chetu Walter Rodney na unyama wa maharamia wa kenya waliomuangamiza
komredi Tom Mboya kwa sababu ya uchu wa madaraka? Nakuuliza profesa! Ni vioja
gani vinaweza kumsibu mtu kushinda vitimbi vya rais Mobutu Sese Seko kwa Profesa
Wamba Dia Wamba na vile vya raisi Obote kwa komredi Nabudara Wadada?Au kuna
shubiri chungu namna gani anayoweza kuinywa
mwanazuoni mzalendo kupita uchungu wa korokoroni aliyopitia Ngugi wa
Thiong’o na masaibu yaliyomuandama mwana-umajumuhi wa Afrika Dr Osagyefo Kwame
Nkurumah?
Nijibu Profesa.Nijibu komredi!Kuna changamoto gani mnaweza kuipata sasa
kuliko zile mlizopitia zama za harakati zenu za University Students African RevolutionaryFront(USARF) wewe na
makomredi wenzio kina Profesa Karim Hirji,Henry Mapolu na Liundi pale chuo
kikuu Mlimani?Alas!,niwie radhi;nilitaka
kuwasahau kina Yoweri kaguta Museveni,Zakia Hamdan Meghi na Omari Ramadhani
Mapuri!Kuna watu huku mtaani eti wanaona hawa makomredi niliotaka kuwasahau wamesaliti
kile mlichopigania miaka ya sabini.Na wewe unaamini hivyo?
Karibuni umewahi kutufunda kuhusu
thamani ya kalamu ya mwanazuoni(Rejea kitabu chako cha Insha zaMapambano Ya Wanyonge).Ulisema kwamba silaha pekee ya
mwanazuoni ni kalamu yake na kwamba ni lazima mwanazuoni atumie kalamu yake kwa
uthabiti kila anapopata nafasi kuwasemea wanyonge wasio na sauti hususani
wakulima na wafugaji(Naomba unipe ruksa niongeze ‘’na machingawa Tandika, Ubungo na kwingineko Tanzaniawanaofurushwa na
wanamgambobila ya kuelekezwa pa kwenda!”).
Binafsi sina maneno toshelezi kuielezea
thamani ya kalamu ya mwanazuoni wa wanyonge zaidi ya sifa zilizotolewa na
Kajubi kwenye Shairi lake la You write(Rejea
kitabu cha Summons:Poemsfrom Tanzania).Inanilazimu
kufasili kwa Kiswahili kwa sababu nakala ya barua yako nimeituma kwa umma wawanyonge
wa uswahilini na vijijini:wanyonge ambao
mfumo wetu wa elimu umewafanya kuwa wahitimu wa shule za kata wasioweza
kuunganisha hata sentesi tatu za kizungu!kajubianamsifia msomi wa wanyonge kwa
maneno yafuatayo;
You weep with them
Unalia pamoja nao(wanyonge)
You sigh with them
Unahema nao(wanyonge)
You suffer with them
Unataabika nao(wanyonge)
But you lift high
Lakini unainua juu
Thebanner of their struggle
Bendera ya
harakati yao
With your sacred pen
Kwa peni yako takatifu!
Naam!hayo siyo maneno yangu. Hayo ni
maneno ya Kajubi kuhusu msomi wa wanyonge.wanyonge wakiteseka,na yeye anahisi
kuteseka;wakihema na yeye anahema;wakilia na yeye anabubujikwa machozi! Ndiyo,
ni kupitia kalamu yake iliyotukuka ,bendera ya harakati za wanyonge inainuliwa juu zaidi na kupepea kuadhimisha
ushindi wa umma wa walalahoi.Kwa kweli kajubi alikuwa anawazungumzia waandishi
kama wewe, chinua Achebe, wole Soyinka na Ngugi wa Thiongo ;waandishi wa
wanyonge.
Kwa hakika beti hizi za kajubi
zinawahusu waandishi sampuli ya komredi Abdilatif Abdallah. Si unakumbuka huyu
bwana alipowekwa gerezani na Mzee Jomo Kenyata kwa kuhoji Kenya inakokwenda? Je
alitokwa na machozi?Gereza lilimkatisha tamaa? La hasha! Aliendelea kuandika
kazi zake za kiukombozi akiwa jela kwa kutumia karatasi za chooni!(toilet paper)
Sasa turudi kwenye barua yangu. Kwa
kweli asili ya barua yangu ni historia ndefu.Ili kuelewa vyema usuli wake,
inanipasa nirejee nyuma kidogo.Miaka kadhaa nyuma nikiwa sekondari, nilipata bahati
ya kusoma, kusimuliwa na kutizama habari kuhusu weledi wa wahadhiri wa UDSM. Na
kwa kweli baada ya kuja chuoni, nimejionea maprofesa na madaktari wa falsafa
waliobobea kwenye fanimbalimbali.
Wakati ule wa sekondari nilivutiwa sana na habari ya Profesa Haroub
Othman, Profesa Rwekaza Simpho Mkandala na Wewe.Kwa bahati mbaya,mauti
yalitupokonya profesa Haroub Othman hata kabla sijamuona.Hata Profesa mkandala
hakuwa tena kwenye taasisi ya utafiti wa siasa na Demokrasia-REDET.Nilimkuta
ametingwa na majukumu ya utawala wa chuo.Mwenyewe amewahi kutueleza kwamba
kiutawala, ana malengo(objectives) matatu.Mosi,kuiendeleza UDSM. Lengo lake la pili
,anasema, ni kuiendeleza UDSM.lengo lake la tatu pia ni kuiendeleza UDSM.Ndiyo;
anasema hana malengo zaidi ya kuiendeleza UDSM!
Hata wewe nilikuta umekwishastaafu
shughuli za uhadhiri.Sikubahatika kukaa darasani ambamo mbele yake kuna
mhadhiri aliyeitwa Issa Gulamhusein Shivji.Mwishowe niliamua kujifariji kwa
kufuata kivuli chako kila mahali.Nilinunua vitabu vyako,kuhudhuria makongamano
na mihadhara yako mingi.Nisingekosa mhadhara wako kirahisi(labda niwe hoi bin
taabani kitandani). Swahibu zangu wa karibu wanajua jinsi nilivyokuwa mnazi wa kazi zako.
Hivyo basi mimi ni mwanafunzi wako;mwanafunzi nje ya utaratibu
rasmi.Kama unavyofahamu,ulimwengu wa wanafunzi umejaa maswali. Wanafunzi
wasipododosa na kuuliza maswali basi fahamu hapo hakuna uanafunzi(bila shaka kuna ububusa au labda wanafunzi wamekuelewa
kwa asilimia mia!). Wanafunzi wa yesu walimsonga masihi wa Mungu kwa
maswali.Maswahaba walimuandama mtume Muhamad(S.A.W) kwa maswali yakufikirisha.
Na mimi mwanafunzi wako nina
maswali.Barua yangu imejaa maswali;maswali ambayo ningekuuliza darasani kama
ningepata bahati ya kufundishwa na wewe.Na kama asemavyo Okot p Bitek(Rejea
kitabu chake cha Songs of Lawino and Ocol),’’maswali
yanapokosa wa kuyajibu yanaumiza kichwa;yanachoma ndani kwa ndani zaidi ya
kichomi!.
Ni matumaini yangu utavumilia maswali yenye dalili za‘’umbumbumbu’’
kwenye baadhi ya maeneo.Naweza( bila kukusudia) kuuliza maswali kuhusu mambo
ambayo umekwisha yatolea ufafanuzi kwenye vitabu,mihadhara na maandiko
yako.Kumbuka siyo kazi ndogo kumaliza rundo la vitabu vyako.Pia naweza
kukuuliza maswali ya ‘’kijuha’’ hapa na pale.Bila shaka,kwa miongo kadhaa ya
huduma yako ya ufundishaji UDSM umevumilia ujuha na vimbwanga vingi vya
wanafunzi.Vumilia na vituko vyangu!.
Sasa nianze maswali yangu….
Fuatilia waraka huu kwenye sehemu ya pili itayowajia baada ya siku
chache.
11 comments:
very interesting...tutapataje sehemu ya pilli?
tuletee na sehemu ya pilli mkuu..
tunasubiria kwa ha
mu sehemu ya pili
kaka i real appreciate your contribution towards right and equality. keep it up. god be with you.
thanx a lot for your comments, i got it from john mnyika group on facebook...so i will try harder to bring you the second part
jamani swahiba nimependa kazi yako inshaalah mwenyez mungu atafungua njia kwako na kazi zako
asante sana hafsa..inshallah mwenyezi mungu atajalia..kazi njema kwako pia
I always proud being among your best friend,namshukuru mungu aliyenileta UDSM na kunikutanisha na beloved kaka anayejielewa, i always pray for u kaka,all the best beloved
very gud kaka addo shaib...i believe utakuwa mwandishi mahiri huko mbele..nina hamu sana na sehemu ya pili...tutaipata lini
this is for z blog owner: sehemu ya pili iko tayari.kwa sababu ya kukata kiu ya wasomaji wako ya kufahamu mwendelezo wa barua hii,tuwasiliane kwa kutumia ukurasa wa fb(ado shaibu),e-mail adoado75@hotmail.com, simu:0653619906
nimefurahi sanaaa...ADO SHAIBU...nakufuata FB..nipate mengi
Post a Comment