Daudi Mwangosi, enzi za uhai wake | |
KUNA jambo moja linawasumbua watu na wapenda haki, namna ambavyo marehemu ameuawa.
Kwa
ufupi ni kuwa ‘BOMU LA MACHOZI’ halijakusudiwa kuuwa na watengenezaji
wake, lakini linapotumika isivyo sahihi huuwa, hiyo hakuna shaka
Marehemu DAUD MWANGOSI ameuawa na askari polisi.
Taarifa za
awali kutoka katika eneo la tukio huko Nyololo, wilayani Mufindi
zineonesha kwamba amepigwa bomu hilo akiwa amekamatwa na FFU.
Alipigwa bomu hilo baada ya kupokea kipigo kikali kutoka kwa baadhi ya
askari waliokuwa wakizuia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kisiendeshe harakati zake za kufungua tawi katika eneo hilo.
Mwangosi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa
wa Iringa (IPC), mbali na kuuawa mbele ya wananchi wa eneo hilo,
walikuwepo pia askari Polisi wengi wa Kutuliza Ghasia (FFU) na Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Iringa (IPC).
Mwili wa marehemu Mwangosi umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya ya Mufindi.
Taarifa kutoka kwa Katibu Msaidizi wa IPC, Francis Godwin zinaonesha
kwamba taratibu za kuutoa mwili huo kutoka katika hospitali hiyo
zitafanywa baada ya wahusika kuufanyia uchunguzi.
Hakuna uthibitisho kwamba IGP Said Mwema atakwenda Mafinga, lakini
taarifa zisizo rasmi kutoka Mafinga, zimedai kwamba kesho Septemba tatu
atatua Mafinga kushiriki katika uchunguzi huo.
Baada ya kufanyiwa uchunguzi, mwili wa mpambanaji Mwangosi utasafirishwa
hadi mjini Iringa na taratibu zingine zikiwemo za mzishi zitatangazwa
baada ya familia yake kujadiliana.
Kabla ya kushiriki tukio hilo lililositisha maisha yake hapa duniani,
Mwangosi aliongoza Mkutano Mkuu wa IPC uliofanyika Septemba 1, katika
ukumbi wa Maktaba mjini Iringa.
Mkutano huo ulihitimishwa kwa wanachama wa IPC kukutana na kula chakula
cha jioni katika moja ya sehemu za burudani mjini Iringa.
Septemba 2, Mwangosi alishiriki Press Conference iliyoitishwa na RPC wa
Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na baadaye ile iliyoitishwa na Katibu
Mkuu wa Chadema Dk Wilboroad Slaa.
Wakati RPC alipiga marufuku kufanya mkutano wowote wa nje mpaka zoezi la
sensa litakapokamilika, Chadema waliahidi kuendelea na ratibu ya
kukijenga chama chao mkoani Iringa.
Mwangosi hakuwa ameambatana na msafara wa Dk Slaa wakati ukielekea
Mafinga. Taarifa zinaonesha kwamba baada ya kumaliza kazi zake zingine
za kiuandishi majira ya saa saba na nusu mchana alipanda basi la Abood
lililokuwa likitokea Dar es Salaam hadi Nyololo ambako chadema walikuwa
na ratiba ya kufungua tawi.
Wakati wakifungua tawi hilo, wananchi walianza kukusanya na ndipo,
Polisi wakatoa tahadhari iliyowataka watawanyike kwasababu shughuli ya
ufunguzi wa tawi hilo ilikuwa inafanywa nje tofauti na maelekezo ya
jeshi hilo.
Katika kurukushani hiyo mwandishi mmoja Godfre Mushi inadaiwa alikamatwa
na Polisi wakati akipiga picha, na Mwangosi alipotaka kujua sababu za
askari hao kumkamata naye alishambuliwa kwa virungu kabla hajalipukiwa
na bomu hilo.
Mmoja wa askari wa jeshi hilo aliuumbaia mtandao huu kwamba
kinachomtambulisha Mwangosi, ni kichwa na sura yake kwa kuwa
havikudhuliwa na mlipuko wa bomu hilo, lakini sehemu nyingine za mwili
wake zimesambaratika vibaya.
Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kupitia Rais
wake Kenneth Simbaya tayari umetuma wawakilishi mkoani Iringa kwa
ajili ya kulifanyia uchunguzi wa kina tukio hilo na utatoa msimamo wake
Jumatano.
Na Jukwaa la Wahariri Tanzania kwa kupitia Katibu wake, Neville Meena
umahidi nao kutoa tamko baada ya kupata taarifa za kina kuhusiana na
tukio hilo.
IPC kwa upande wake inaendelea kushiriki uratibu wa msiba na kwa
kushirikiana na wanahabari wote wa mkoa wa Iringa inaendelea kupokea
michango mbalimbali kutoka kwa wasamalia wema.
Waandishi wa habari, viongozi wa serikali na taasisi binafsi wameeendelea kutoa rambirambi zao kupitia uonngozi wa IPC. Taarifa hii ni kwa hisani ya
Frank Leonard, Iringa.mmiliwa mtandao wa www.frankleonard.blogspot.com |
No comments:
Post a Comment