FOLLOWERS

Thursday, November 10, 2011

MAONI HAYA YA ASASI ZA KIRAIA YAMEZINGATIWA KATIKA MSWAADA MPYA WA KATIBA??

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya katiba na sheria mheshimiwa Pindi Chana.

MAPENDEKEZO YA MASHIRIKA YA KIRAIA JUU YA MUSWADA WA SHERIA YA MAPITIO YA KATIBA, 2011.
Mapendekezo ya Jumla
1. Matumizi ya lugha ya kiingereza katika muswada: Mbali ya ukweli kwamba karibu asilimia themanini ya watanzania (80%) huongea na kuelewa vyema kiswahili, mswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba umeandikwa kwa lugha ya kiingereza. Matumizi ya lugha ya kiingereza na masuala ya kiufundi wa kisheria katika muswada unawafanya watanzania walio wengi, kushindwa kushiriki kikamilifu katika kuuelewa muswada na hatimaye kutoweza kutoa mapendekezo yao.
PENDEKEZO: Tunapendekeza ya kwamba muswada uandikwe katika lugha ya taifa yaani Kiswahili.
2. Vyombo vya utungaji katiba: Muswada wa Sheria ya mabadiliko ya katiba hauelezi juu ya ushirikishwaji wa vyombo rasmi vya utungaji katiba. Katika kifungu kinachoelezea tafsiri ya maneno yaliyotumika katika muswada, kifungu hicho cha 3 kinatamka “vyombo vya kikatiba” humaanisha, kwa madhumuni ya sheria hii, Rais, Bunge Maalum la katiba au Bunge la Jamhuri ya Muungano”. Tafsiri hiyo ina maana ya kwamba, vipo vyombo viwili tu vya utungaji katiba navyo ni Rais na, aidha Bunge maalum au Bunge la Jamhuri ya Muungano.
PENDEKEZO: Tunapendekeza viwepo vyombo vya mchakato wa kuwa na katiba mpya navyo ni;-
§ Tume ya kupokea mapendekezo ya katiba mpya
§ Bunge maalum la katiba
§ Mkutano wa kitaifa wa katiba
§ Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
§ Kura ya maoni ya wananchi juu ya katiba
Ni vyema kwa vyombo hivi kutamkwa katika muswada na majukumu yake kuainishwa ipasavyo.
3. Muswada umempa Rais mamlaka makubwa mno: Katika muswada huu, Rais amepewa mamlaka zaidi. Rais anayo mamlaka ya kuunda Tume na kuteua wajumbe, kutoa hadidu za rejea kwa Tume, kumteua katibu wa Sekretarieti ya Tume, kupokea taarifa na tathmini, kuunda Bunge maalum la katiba bila ya kujali uwepo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopo.
4. Muswada wa Sheria ya mabadiliko ya Katiba una mapungufu na haufai: Kwa mfano, ukiangalia jina la muswada huu yaani Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011, jina hilo haliakisi utungwaji wa katiba mpya bali ni kufanyia mabadiliko ya katiba iliyopo wakati huu. Mathalani, hakuna malengo mahsusi ya muswada huu. Hali Kadhalika, kumekuwepo na kurudiwa rudiwa kwa vifungu katika muswada kwa mfano angalia kifungu cha 9 na 17. Vile vile, vipo vifungu vinavyoleta mkanganyiko kama kifungu cha 23(3) na 26, pia soma kifungu cha 6 na 19. Kuna makosa zaidi ya arobaini (40) katika muswada wenye vifungu 31 tu.
5. Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba haujazingatia hitaji la umma wenye kutaka katiba mpya: Ukisoma kifungu cha 9(2), muswada hautoi nafasi ya umma kushiriki kikamilifu katika kujadili na kupendekeza juu ya Muungano wa Tanzania, mamlaka ya Rais, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mengineyo, mambo ambayo ni kati ya yale ya msingi wa madai ya kuandikwa upya katiba.
6. Makosa ya jinai na vitisho visivyo vya lazima ndani ya muswada: Muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba umeweka vitisho kwa wananchi ambao wanaweza kuhoji masuala na au mwenendo wa tume kama ilivyo katika kifungu cha 20 na 28(2) na (3). Hii ni kinyume kabisa na misingi ya haki na uhuru wa kujieleza kwani katika mchakato kama huu ni lazima kutakuwa na ukinzani wa mawazo. Hivyo basi, sheria inatakiwa kulinda uhuru wa mawazo na watanzania watakaotoa mawazo yao mbele ya tume. Hii itawezesha watu wengi zaidi kushiriki katika mchakato huu wa kihistoria wa uandikaji wa katiba mpya bila woga wala hofu.
7. Muswada hauweki ukomo wa muda: Muswada hauweki ukomo wa mchakato kupata katiba mpya. Tunapendekeza muswada uweke muda ambao kila mchakato unaotajwa katika katiba utahitimishwa pamoja na muda wa kuhitimisha mchakato wa uandikaji katiba mpya ili wananchi waweze kujiandaa, kufuatilia na kushiriki kila hatua ya mchakato huu muhimu.
Kutokana na mapungufu yote hayo, tunapendekeza mambo yafuatayo yafanyike
(a) Muswada utafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya taifa ili kuruhusu ushiriki mpana zaidi wa wananchi katika mijadala
(b) Muswada usambazwe kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, taasisi za umma, serikali za mitaa ili wananchi waweze kujua maudhui ya muswada huu
(c) Majadiliano ya muswada yafanywe katika kila jimbo la uchaguzi yakiongozwa na wabunge ili kukusanya maoni ya wananchi kutoka katika kila jimbo
(d) Tume ya kukusanya maoni iwe huru, iteuliwe na kamati maalumu ya Bunge, hadidu za rejea ziwe ndani ya muswada huu na taarifa ya tume na pendekezo la katiba vipelekwe kwenye bunge la katiba (Constituency Assembly).
(e) Iandaliwe rasimu nyingine ya muswada ili kutoa fursa kwa ajili ya wananchi wengi zaidi kutumia uhuru wao wa kutoa mawazo kushiriki na vyombo vya kutunga katiba kwa mujibu wa mamlaka watayopewa na wananchi.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...