AZIMIO LA ARUSHA NA SIASA YA TANU JUU YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA
Imetolewa na Idara ya Habari,
TANU, Dar es Salaam, 1967
SEHEMU YA KWANZA
Imani ya Tanu
SIASA YA TANU NI KUJENGA NCHI YA UJAMAA, MISINGI YA UJAMAA
IMETAJWA KATIKA KATIBA YA TANU, NAYO NI HII
Kwa kuwa TANU inaamini:-
(a) Kwamba binadamu wote ni sawa;
(b) Kwamba kila mtu anastahili heshima;
(c) Kwamba kila raia ni sehemu ya Taifa na anayo haki ya
kushiriki sawa na wengine katika Serikali tangu ya Mitaa, ya
Mikoa hadi Serikali Kuu;
(d) Kwamba kila raia anayo haki ya uhuru wa kutoa mawazo
yake, ya kwenda anakotaka, wa kuamini dini anayotaka na
wa kukutana na watu mradi havunji Sheria;
(e) Kwamba kila mtu anayo haki ya kupata kutoka katika jamii
hifadhi ya maisha yake na ya mali yake aliyonayo kwa
mujibu wa Sheria;
(f) Kwamba kila mtu anayo haki ya kupata malipo ya haki
kutokana na kazi yake
(g) Kwamba raia wote kwa pamoja wanamiliki utajiri wa asili
wanamiliki utajiri wa asili wa nchi hii ukiwa kama dhamana
kwa vizazi vyao;
(h) Kwamba ili kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakwenda
sawa Serikali lazima iwe na mamlaka kamili juu ya njia
muhimu za kuukuza uchumi; na
(i) Kwamba ni wajibu wa Serikali, ambayo ni watu wenyewe,
kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi ya Taifa ili
kuhakikisha usitawi wa raia wote na kuzuia mtu kumnyonya
mtu mwingine au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine
na kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani
na siasa ya watu wote kuwa sawa.
MADHUMUNI YA TANU
Kwa hiyo basi, makusudi na madhumuni ya TANU yatakuwa kama
hivi yafuatavyo:-
(a) Kuudumisha uhuru wa nchi yetu na raia wake;
(b) Kuweka heshima ya mwanadamu kwa kufuata barabara
kanuni za Tangazo la Ulimwengu la Haki za Binadamu.
(c) Kuhakikisha kwamba nchi yetu inatawaliwa na Serikali ya
watu ya kidemokrasia na ya kisoshalist;
(d) Kushirikiana na vyama vyote vya siasa katika Afrika
vinavyopigania uhuru wa bara lote la Afrika;
(e) Kuona kwamba Serikali inatumia mali yote ya nchi yetu kwa
kuondoshea umaskini; ujinga na maradhi;
(f) Kuona kwamba Serikali inasaidia kwa vitendo kuunda na
kudumisha vyama vya ushirika;
(g) Kuona kwamba kila iwezekanapo Serikali inashiriki hasa
katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu;
(h) Kuona kwamba Serikali inatoa nafasi zilizo sawa kwa wote,
wake kwa waume, bila kujali rangi, kabila, dini au hali;
(i) Kuona kwamba Serikali inaondoa kila namna ya dhuluma,
vitisho, ubaguzi, rushwa na upotofu;
(j) Kuona kwamba Serikali ya nchi yetu inasimamia barabara
njia kuu za kuzalisha mali na inafuata siasa ambayo
itarahisisha njia ya kumiliki kwa jumla mali za nchi yetu;
(k) Kuona kwamba Serikali inashirikiana na dola nyingine katika
Afrika katika kuleta Umoja wa Afrika.
(l) Kuona kwamba Serikali inajitahidi kuleta amani na salama
ulimwenguni kwa njia ya Chama cha Umoja wa Mataifa.
SEHEMU YA PILI
SIASA YA UJAMAA
(a) Hakuna Unyonyaji:
Nchi yenye Ujamaa kamili ni nchi ya wafanyakazi: haina
ubepari wala ukabaila. Haina tabaka mbii za watu: tabaka ya
chini ya watu wanaoishi kwa kufanya kazi, na tabaka ya juu ya
watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi. Katika nchi ya Ujamaa
kamili mtu hamnyonyi mtu, bali kila awezaye kufanya kazi
hufanya kazi, na kila mfanya kazi hupata pato la haki kwa kazi
aifanyayo na wala mapato ya wafanyakazi mbali mbali
hayapitani mno.
Katika nchi ya Ujamaa kamili watu peke yao ambao huishi
kwa jasho la wenzao, na ni haki yao kuishi kwa jasho la wenzao
ni watoto wadogo, wazee wasiojiweza, vilema na wale ambao,
kwa muda, Jumuiya imeshindwa kuwapatia kazi yo yote ya
kujipatia riziki kwa nguvu zao wenyewe.
Nchi yetu ni nchi ya Wakulima na Wafanya kazi, lakini sin
chi ya Ujamaa kamili. Ina misingi ya ubepari na ukabaila na
vishawishi vyake. Misingi hii ya ubepari na ukabaila yaweza
ikapanuka na kuenea.
(b) Njia kuu za uchumi ni chini ya wakulima na wafanya
kazi:
Namna ya pekee ya kujenga na kudumisha ujamaa ni
kuthibitisha kuwa njia kuu zote za uchumi wa nchi yetu
zinatawaliwa na kumilikiwa na Wakulima na Wafanyakazi
wenyewe kwa kutumia vyombo vya Serikali yao na Vyama
vyao vya Ushirika. Pia ni lazima kuthibitisha kuwa Chama
kinachotawala ni Chama cha wakulima na wafanyakazi.
Njia kuu za Uchumi ni: kama vile ardhi, misitu, madini,
maji, mafuta na nguvu za umeme; njia za habari, njia za
usafirishaji; mabenki, na bima; biashara na nchi za kigeni na
biashara za jumla; viwanda vya chuma, mashini, silaha, magari,
simenti, mboleo; nguo, na kiwanda cho chote kikubwa
ambacho kinategemewa na sehemu kubwa ya watu katika
kupata riziki zao au kinachotegemewa na viwanda vingine;
mashamba makubwa na hasa yale yanayotoa mazao ya lazima
katika viwanda vikubwa.
Baadhi ya njia hizi na nyingine zisizotajwa hapa hivi sasa
zinamilikiwa au kutawaliwa na Serikali ya Wananchi.
(c) Kuna Demokrasi:
Nchi haiwi ni ya Ujamaa kwa sababu tu njia zake kuu au
zote za uchumi hutawaliwa na humilikiwa na Serikali. Sharti
Serikali iwe inachaguliwa na kuongozwa na Wakulima na
Wafanya kazi wenyewe. Serikali ya Makaburu wa Rhodesia au
Afrika ya Kusini ikitawala au kumiliki njia zote za uchumi, hiyo
itakuwa ni njia ya kukomaza Udhalimu siyo njia ya kuleta
Ujamaa. Hakuna Ujamaa wa kweli pasipo na Demokrasi ya
No comments:
Post a Comment