WITO WA KUKUSANYA MAONI YA WADAU KUHUSU OMBI LA TANESCO LA
KUPANDISHA BEI YA HUDUMA YA UMEME
Tarehe 9 Novemba 2011 Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (“EWURA”)ilipokea ombi la dharura toka Shirika la Umeme Tanzania (“TANESCO”) la kuidhinishiwa ongezeko la bei za huduma ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 ya bei ya sasa kama inavyonyeshwa katika Jedwali Na.1. Ombi husika limesajiriwa kwa Na. TR-E-11-012. Kulingana na Kifungu Na.19(2)(b) cha Sheria, Sura 414 ya Sheria za Tanzania, EWURA imeanza mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu uhalali wa ombi lililowasilishwa na TANESCO. TANESCO wamependekeza kuwa bei hizo zitaanza kutumika kuanzia tarehe 1 Januari 2012.
Jedwali Na.1: Bei ya sasa na bei iliyopendekezwa
Kundi na aina ya matumizi | vipengele | Bei ya sasa (TZS) | Bei mpya (TZS) | |
D1 | Matumizi madogo ya kaya | Gharama ya huduma kwa mwezi | 0 | 0 |
Bei kwa kila uniti (0-50kWh) | 60 | 153 | ||
Bei kwa uniti zaidi ya 50 kWh | 195 | 497 | ||
T1 | Matumizi ya kawaida | Gharama ya huduma kwa mwezi | 2,738 | 3,106 |
Bei kwa kila uniti (kVh) | 157 | 400 | ||
T2 | Msongo mdogo | Gharama ya huduma kwa mwezi | 10,146 | 25,875 |
Bei kila uniti (kVh) | 94 | 240 | ||
Mahitaji (demand) kwa (kVh) | 12,078 | 30,802 | ||
T3 | Msongo mkubwa | Gharama ya huduma kwa mwezi | 10,146 | 25,875 |
Bei kwa kila uniti | 84 | 212 | ||
Mahitaji (demand) (kVh) | 10,350 | 26,395 | ||
T5 | ZECO | Gharama ya huduma kwa mwezi | 10,146 | 25,875 |
Bei kila uniti (kVh) | 83 | 212 | ||
Mahitaji (demand) kwa kVA | 8,610 | 21,957 |
Kulingana na ombi lililowasilishwa, katika mwaka 2010 na 2011 Tanzania ilikuwa na hali mbaya ya mvua katika maeneo ya mabwawa na hivyo iliathiri uzalishaji wa umeme. Hii ilisababisha nchi kuwa na upungufu mkubwa wa umeme na kuathiri sio tu hali ya kifedha ya TANESCO bali pia uchumi kwa ujumla wake uliathirika. Ili kulimaliza tatizo hili, TANESCO ilisaini mkataba na IPTL kuzalisha Megawati 100 kwa kutumia mafuta mazito (HFO); ilisaini mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na Symbion LLC kuzalisha Megawati 112 kutumia gesi asilia na mafuta; na ilisaini Mkataba wa Kuuziana Umeme (PPA) na Aggreko kuzalisha Megawati 100 kutumia mafuta ya dizeli. Vilevile, TANESCO inatekeleza mradi wake wa Megawati 150 ambao utatumia gesi asilia pamoja na mafuta (dual fuel plant) na mradi mwingine wa Megawati 70 ambao utatumia mafuta mazito (HFO). Ukiacha miradi ya TANESCO ambayo itakamilika mwaka 2012, umeme unaozalishwa kupitia mikataba tajwa umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la mgao wa umeme hapa nchini. Hata hivyo, juhudi za kumaliza mgao wa umeme hapa nchini zimeongeza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji za TANESCO; na hivyo ombi la TANESCO kuongeza asilimia 155 ili kulipia gharama hizo. Kulingana na kifungu Na. 15(1)(3) cha Mwongozo wa Uwasilishaji Maombi ya Bei wa mwaka 2009 (Tariff Application Guidelines of 2009), waziri mwenye dhamana (kwa hali hii) wa Nishati na Madini, anatakiwa kutoa Hati ya Dharura (Certificate of Urgency) kwa EWURA ili ombi lililowasilishwa liidhinishwe haraka na sio kwa utaratibu wa kawaida. Tarehe 11 Novemba EWURA ilipokea Kibali cha Dharura toka kwa Waziri husika. Kwahiyo, EWURA imeanza mchakato wa kupitia ombi la dharura la TANESCO ambalo maamuzi yake yatatolewa kupitia Agizo la Muda (Provisional Order) baada ya kupata maoni ya wadau. Kwa mtazamo huo, EWURA inawakaribisha wananchi wote kuhudhuria na/ama kuwasilisha maoni yao katika mkutano wa kukusanya maoni ya wadau utakaofanyika tarehe 2 Disemba
2011 katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa unaotazamana na Chuo cha Usimamizi wa Fedha, Dar es Salaam kuanzia saa nne asubuhi. Wadau na wananchi wote kwa ujumla mnakaribishwa kuwasilisha maoni yenu kwa maandishi kuhusiana na ombi husika wakati wowote kabla ya saa 11:00 jioni siku ya Jumatatu tarehe 30 Novemba 2011. Wadau na wananchi wote kwa ujumla wanatakiwa kuzingatia tarehe na muda uliotajwa katika tangazo hili. Nakala ya maombi husika zinapatikana bure katika tovuti ya EWURA (www.ewura.go.tz), isipokuwa nyaraka za siri zilizowasilishwa EWURA na mwombaji kulingana na kifungu cha 25 cha Sheria, Sura 414.
Kwa maelezo zaidi tuandikie kwa anuani hapa juu.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji
No comments:
Post a Comment