FOLLOWERS

Monday, September 3, 2012

TAARIFA KWA UMMA (DSM) : WIZARA YA MALIASILI INAWATAKA WANANCHI KUWA MAKINI KATIKA ZOEZI INALOENDESHA LA KUANGAMIZA KUNGURU WEUSI KWA KUTUMIA SUMU YA SRC 1339.

          TAARIFA KWA UMMA

ZOEZI LA KUANGAMIZA KUNGURU WEUSI JIJINI DAR ES SALAAM

Wizara ya Maliasili na Utalii imewataarifu wananchi waishio katika jiji la Dar es Salaam kuchukua tahadhari wakati huu ambapo Wizara inaendesha zoezi la kuwaua kunguru weusi jijini kwa kutumia sumu tulivu iitwayo SRC 1339.

Ingawaje sumu hiyo haina madhara makubwa kwa binadamu, wananchi hasa watoto, wametakiwa kutocheza na mizoga ya kunguru ambao watakuwa wamekufa kutokana na sumu hiyo. Endapo mtu atakuwa ameishika mizoga hiyo anatakiwa anawe kwa sabuni.

Aidha wananchi wametakiwa wasitupe mabaki ya chakula kiholela maana kufanya hivyo ni kukaribisha kunguru katika sehemu husika.

Wizara, kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali, ilianza kuwaangamiza kunguru weusi jijini Dar es Salaam tangu mwezi Desemba mwaka 2010 chini ya mradi maalum unaofadhiliwa na Serikali, kwa kushirikiana na Balozi za Denmark na Finland, na Shirika la USAID la Marekani.

Tangu mradi huo uanze mwaka 2010 jumla ya kunguru 750,000 wameshaangamizwa kwa njia ya mitego maalum na sumu. Hata hivyo ndege hao bado wapo Dar es Salaam na wanaendelea kuleta kero jijini. Ndiyo maana zoezi la sasa linafanyika kwa njia ya operesheni ili kunguru wengi zaidi waweze kuuwawa. Tangu operesheni inayoendelea ianze tarehe 27 Agosti 2012 jumla ya kunguru 1,000 wameshaangamizwa.

Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa kikosi kazi ambacho kitahusika kuokota mizoga hiyo, kwa kuonyesha iliko. Pia wanatakiwa kutoa taarifa pale watapogundua kuwa kuna idadi kubwa ya ndege hao sehemu yoyote ili hatua za kuwangamiza ziweze kuchukuliwa.

Taarifa zipelekwe katika ofisi za Manispaa au kwa kupiga simu 0754 498957 (Wilaya ya Kinondoni), 0757 585 358 (Wilaya ya Ilala) na 0714 119200 (Wilaya ya Temeke).

[MWISHO]

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
1 Septemba 2012

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...