TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete ameishukuru kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom
kwa kuchangia katika mradi wa kuhifadhi mbwa mwitu katika hifadhi ya
Taifa ya Serengeti, mradi unaojulikana kama Vodacom Foundation Serengeti
Wild Dogs Conservation Project, kwa dola za Marekani 450,000 kwa
kipindi cha miaka mitatu.
Rais
ametoa shukrani hizo Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom hapa nchini Bw.
Rene Meza, Ikulu Dar-Es-Salaam, walipokutana jana jioni, Ijumaa Agosti
31,2012
"Napenda kutoa shukrani zangu kwa Vodacom kwa msaada huu mkubwa, tunashukuru kwa jitihada zenu kubwa katika hili" Rais amesema.
Naye
Mtendaji Mkuu wa Vodacom amemhakikishia Rais kuwa kampuni yake
itaendelea kushirikiana na serikali katika miradi mbalimbali ya
maendeleo, elimu na Afya.
“Tunajisikia
faraja sana kuwa miongoni mwa washirika wa mradi huu. Ni heshima kwetu
na tuko makini nao, tunataka kuendelea na mradi huu" Bw, Rene Meza
amemhakikishia Rais.
Tayari
mbwa mwitu kumi na Moja, wamerudishwa mbugani siku ya Alhamisi Agosti
30, 2012 baada ya kuhifadhiwa kwenye boma maalumu la mradi huo, katika
eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani
Mara.
Wadau
wengine walioshiriki na kufanikisha zoezi hilo ni pamoja na Idara ya
Wanyamapori, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCCA), Frankfurt Zoological Society , Grumeti Fund na
Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Kuachiwa
kwa Mbwa Mwitu hao 11 walioondolewa katika msitu wa Samunge wilayani
Loliondo ni mojawapo ya juhudi za kurudisha tena makundi ya wanyama hao
katika mbuga hiyo maarufu duniani. Hivi sasa kuna makundi 11
yanayofuatiliwa, manane yakiwa Loliondo na matatu katika Hifadhi ya
Ngorongoro, yakifanya jumla ya Mbwa Mwitu 200.
Mtafiti
wa Magonjwa ya Wanyama kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyama (TAWIRI)
Dkt. Ernest Mjingo, alimwambia Rais Kikwete kwamba katika Hifadhi ya
Serengeti makundi ya Mbwa Mwitu yalikuwa yakionekana kwa wingi, lakini
sasa yametoweka na mara ya mwisho Mbwa Mwitu wawili walionekana mwaka
1998.
Mtafiti
huyo alisema Mbwa Mwitu wamekuwa wakitoweka kutokana na kuuawa kwa sumu
na wananchi baada ya kula mifugo yao na kuugua magonjwa mbalimbali kama
kichaa cha mbwa.
Dkt.
Mjingo alisema baada ya kuachiwa Mbwa Mwitu hao, waliovishwa collar
maalumu zenye redio, juhudi zitaendelea ili kupata makundi sita yenye
Mbwa Mwitu takriban kumi kila moja, ikiwa ni hatua endelevu ya muda
mrefu ya kuhakikisha uwepo wa wanyama hao mbugani humo.
Mbwa
Mwitu ni miongoni mwa wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka duniani.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika Bara la Afrika kuna Mbwa Mwitu
wanaofikia 8,000 na Tanzania pekee inakadiriwa kuwa wanyama hao 3,500
katika mbuga mbalimbali nchini. Katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
walitoweka kabisa kabla ya juhudi hizi za kuwarejesha kuanza.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
1 Septemba, 2012
No comments:
Post a Comment