Chama cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA kimeacha historia ambayo ni
vigumu kufutika katika uzinduzi wa operesheni Sangara kanda ya kati
uliofanyika Ifakara-Kilombero jana.
Katika mkutano huo ulikusanyika umati mkubwa kuwahi kushuhudiwa katika wilaya hiyo kwa miaka ya karibuni.
Akihutubia maelfu kwa maelfu ya wananchi katika mkutano huo jana, ikiwa
ni sehemu ya Operesheni Sangara awamu ya pili, Kiongozi mkuu wa upinzani
nchini ambaye pia ni Katibu mkuu wa CHADEMA Dk.Wilbroad Slaa
aliyeambatana na viongozi wakuu wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa
Taifa, Freeman Mbowe, alisema kuwa Serikali ya CCM imekuwa na kiburi cha
kuwatisha wanaotaka kutetea maslahi ya wananchi huku ikifungia hata
vyombo vya habari kama Mwanahalisi.
“Serikali ina nguvu ya kuvifungia vyombo vya habari kwa sheria dhalimu
ya magazeti ya mwaka 1977, lakini kamwe haitaweza kuzuia kina Dr Slaa
kupiga kelele'' alisema kiongozi huyo. Dk. Slaa ambaye alikuwa
akishangiliwa kwa nguvu na halaiki hiyo huku anga likihanikizwa kwa
kelele za RAIS....RAIS...RAIS...., aliongeza kuwa, kuanzia sasa CHADEMA
itaanzisha mapambano kwa ajili ya haki ya Watanzania.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe alisema umati uliokusanyika
unaonesha namna wakazi wa Kilombero walivyomthamini aliyekuwa mbunge wa
viti maalumu, marehemu Regia Mtema.
Mbowe aliomba jina la uwanja wa Ifakara libadilishwe na kuitwa Uwanja wa
Ukombozi, na kwamba hali hiyo iwe chimbuko la ukombozi kwa Mkoa wa
Morogoro.
Aliwataka wakazi wa Kilombero kuacha kulalamika na badala yake wachukue hatua kwa kuachana na CCM na kujinga na CHADEMA.
Katika mkutano huo maelfu ya wananchi walijiunga na CHADEMA wengi wao
wakiwa ni kutoka CCM.Mara baada ya mkutano huo baadhi ya watu
walionekana wakifuta machozi huku wakisema wanaamini bado siku chache tu
CHADEMA kuingia madarakani na kukomboa watanzania kiuchumi.
Mbali na Dk. Slaa na Mbowe, viongozi wengine waliokuwa katika msafara
huo ni Joshua Nassar (Arumeru Mashariki), Tundu Lissu (Singida
Mashariki), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Hamad Yusuph (Naibu Katibu
Mkuu Zanzibar), Suzan Kiwanga (Viti Maalumu), Joyce Mukya (Viti Maalumu)
na wengine wa makao makuu. Source: Majira/Tanzania Daima/Nipashe |
No comments:
Post a Comment