FOLLOWERS

Monday, July 16, 2012

TSH 250M ZADAIWA KUIBIWA KATIKA BENKI YA KKKT KUPITIA ATM MASHINE

WATEJA zaidi ya 50 wa Benki ya Uchumi Commercial Bank Ltd (UCB) ya Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wanasakwa na polisi kufuatia wizi wa karibu Sh250 milioni.
Vyanzo vya kuaminika vilidokeza kuwa ingawa taarifa zilizofunguliwa polisi na menejimenti ya UCB zinaonyesha kiasi kilichoibwa ni Sh224 milioni, lakini kinaweza kufikia Sh250 milioni kadri uchunguzi unavyoendelea.

Benki hiyo iliyoanzishwa mwaka 2005 baada ya kupatiwa leseni namba CBA 00031 na Benki kuu ya Tanzania (BoT), inamilikiwa na Watanzania wapatao 330,000 ambao ni waumini wa dayosisi hiyo.
Habari za uhakika zilizolifikia Mwananchi zilisema wizi huo ulifanyika baada ya kuparanganyika kwa mfumo wa kompyuta uliounganishwa na mashine za ATM.
Taarifa nyingine zilisema wizi huo ulitokana na baadhi ya wateja kuusoma mfumo wa kompyuta hiyo na kugundua kuwa kuna nyakati za usiku huchanganyikiwa na kutoa salio lisilo sahihi la wateja.
“Kilichotokea ni kuwa kuna watu walivujisha siri kuwa nyakati za usiku sana ukichomeka kadi kwenye hiyo ATM inatoa pesa hovyo hovyo hata kama hauna salio la kutosha”kilidokeza chanzo chetu.
Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa wateja wa benki hiyo wapatao 50 walijihusisha na wizi wa fedha hizo kupitia ATM hiyo na tayari polisi imeanzisha uchunguzi maalumu wa kuwasaka.
Habari hizo zimedai kuwa baada ya kugundulika kwa dosari katika mfumo huo wa kompyuta za ATM katika benki hiyo, baadhi ya wateja walianzisha kuchukua fedha muda mfumo huo unapoharibika. “Sio pesa zilizoibwa mara moja hapana yaani unakuta leo anatoa 500,000 kesho hivyo hivyo na ilikuwa ni wateja tofauti tofauti waliokuwa wamegundua siri hiyo”alidokeza mtumishi mmoja wa UCB.
Baadhi ya wanasheria walidai zipo changamoto nyingi katika kesi za aina hiyo hasa katika kuthibitisha kama wakati mtuhumiwa anatoa fedha hizo katika ATM,alikuwa amekula njama ya kutenda kosa hilo.
Meneja mkuu wa Benki hiyo, Angela Moshi alipoulizwa alikiri kuwapo kwa tukio hilo, lakini akasema hakuwa katika nafasi nzuri ya kulielezea kwa vile alikuwa akielekea kanisani kwa ajili ya ibada.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...