MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA YA WIZARA YA ARDHI
MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA
HOTUBA YA WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MHESHIMIWA PROF. ANNA TIBAIJUKA (MB.), WAKATI WA UFUNGUZI WA MAONESHO YA KUADHIMISHA MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KUANZIA TAREHE 22 SEPTEMBA HADI 25 SEPTEMBA, 2011 KATIKA VIWANJA VYA MNAZI MMOJA, DAR ES SALAAM
Kaimu Katibu Mkuu, Ndg. Maria Bilia,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki,
Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam,
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
Wastahiki Mameya wa Manispaa zote za Dar es Salaam,
Ndugu Viongozi na Watendaji wa Halmashauri Nchini
Ndugu Viongozi wa Taasisi na Mashirika Mbalimbali
Wenyeviti wa Bodi Mbalimbali,
Wakurugenzi, Maafisa na Watendaji wa Wizara,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Ndugu Wadau wa Sekta ya Ardhi , Nyumba na Makazi, awali ya yote natoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha sisi wote kuwepo hapa siku ya leo. Nawashukuru kwa kuitika kuja kushiriki kwa kujionea yale ambayo yanayofanyika katika sekta ya Ardhi, Nyumba na Makazi nchini kwetu tangu tupate uhuru. Kufika kwenu hapa ni tafsiri sahihi ya kutambua kuwa hii sekta ipo kwa ajili ya watu, na ni watu wote; wazee, watoto na wanawake, wote ni wadau kwa sababu hakuna maisha pasipo makazi na hakuna maendeleo pasipo Ardhi. Ardhi, Nyumba na Makazi kwa ujumla ni mahitaji ya kwanza mtambuka katika kupanga shughuli au mkakati wowote wa maendeleo.
Ndugu Wananchi, Wizara yangu ilikuwa ikiunganishwa kimuundo na sekta mbalimbali tangu uhuru kama misitu, maji, madini na utalii hadi mwaka 2001 yalipofanyika mabadiliko na kuitwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mpaka sasa.
Pamoja na mabadiliko mbalimbali,Wizara yangu imekuwa na majukumu mbali mbali katika kuendeleza sekta mama ya ardhi nchini, yakiwemo kusimamia utekelezaji wa sera ya Taifa ya Ardhi, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi pamoja na Sheria zinazohusu sekta ya ardhi na nyumba, kusimamia na kufanya shughuli za upimaji ardhi na uandaaji ramani, kuendeleza makazi, kusimamia na kufanya shughuli za uthamini, kusimamia na kufanya shughuli za usajili wa hati za kumiliki ardhi, kupanga na kusimamia matumizi bora ya Ardhi, kufanya utafiti wa vifaa vya ujenzi wa nyumba bora, Kupanga na kusimamia maendeleo ya miji, kusimamia shughuli za upimaji ardhini na majini na kufanya utafiti wa vifaa vya ujenzi wa nyumba bora
Ndugu Wananchi, Maadhimisho ya Miaka Hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa upande wa Wizara yetu yanaanza rasmi leo tarehe 22 Septemba, 2011 na yanamalizika tarehe 25 Septemba, 2011. Hata hivyo, maadhimisho haya ambayo yanaendelea hadi Desemba yanalenga kutangaza mafanikio yaliyofikiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara tangu Desemba 1961 hadi sasa. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni kuwa “Tumethubutu kuwa na ardhi ambayo ni mtaji na ni mali, Tumeweza kuiendeleza na Tunazidi kusonga mbele katika kuendeleza ardhi yetu kwa manufaa ya Watanzania wote”
Ndugu wananchi, wakati leo tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, takwimu mbalimbali zinazotokana na tafiti zinazofanywa na taasisi za kimataifa zinaashiria kuwa katika bara la Afrika, Asia, Marekani ya Kusini (Latin America) na Carribeani tunahitaji mikakati ya ziada ili kuweza kukabiliana na suala la makazi kutokana na kasi ya kuongezeka kwa watu kuhamia mijini.
Mfano kufikia 2050 zaidi ya watu bilioni sita ambayo ni theluthi mbili ya wakazi wote duniani watakuwa wanakaa mijini.
Ripoti na maazimio ya Agenda ya Makazi, Azimio la Vancouver na makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuhusu Makazi, Azimio Na.56/206 vyote vinatahadharisha tuwe makini na mipango ya makazi.
Ili kufanisha haya tunahitaji kuwa na ushirikiano wa karibu katika kupanga matumizi ya ardhi ili kuweza kuendelea na matumizi mengine ya ardhi.
Hata hivyo Wizara ya Ardhi inajivunia mafanikio yaliyofikiwa katika sekta hii. Wizara ilianza kama Idara ya Ardhi na Upimaji mwaka 1957 ikiwa na idadi ndogo ya watumishi na majukumu machache sana. Iliendelea kukua na kubadilishiwa majukumu na jina kubadilika mara kwa mara kama mtakavyoona katika vipeperushi vilivyogawanywa. Leo tunaposheherekea miaka 50 ya uhuru, majukumu ya Wizara na Sekta ya Ardhi kwa ujumla yameongezeka na idadi ya watumishi imeongezeka sana hadi kufikia zaidi ya watumishi 1400 na bado hawatoshi kukidhi mahitaji yote ya Wizara na Halmashauri.
Ndugu wananchi, wakati Tanzania Bara inapata Uhuru wake mwaka 1961 Sekta ya Ardhi ilikuwa haichangii kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa. Hii ilitokana na sabau kwamba ardhi ilikuwa haijaandaliwa mipango wala kupimwa. Hivi sasa maeneo mengi ya mijini yamepimwa na pato la taifa kutokana na ardhi limeongezeka kutoka Shilingi 650,000,000 kwa mwaka 1995/96hadi kufikia jumla ya Shilingi Bilioni 15.6 kwa mwaka 2010/11. Natoa wito kwa wananchi kupima maeneo yao ili kuongeza mapato yao binafsi na hata ya Taifa letu. Ardhi iliyopimwa ni mali na ni mtaji kwani inajulikana kwa urahisi kwa vile ina vielelezo vya kumilikiwa na mtu au asasi katika mfumo wa hati.
Ndugu wananchi, napenda kuwaeleza kuwa, umiliki wa ardhi kwa kuandikishwa ulianza toka wakati wa utawala wa Mjerumani . Hadi tunapata uhuru, watu waliokuwa wanamilikishwa ardhi kwa kusajiliwa walikuwa ni wageni peke yao. Wananchi walianza kumilikishwa ardhi baada ya uhuru ambapo mpaka sasa jumla ya miliki 739,712 za ardhi zimetolewa. Aidha, Wizara imeanzisha mpango wa kupima mipaka ya vijiji ambapo vijiji 11,260 vilipimwa na kutoa vyeti 7,510. Mpango huo uliwezesha kupima mashamba ya wananchi na kutoa hatimiliki za kimila. Hadi sasa jumla ya hati miliki za kimila 157,968 zimetolewa katika wilaya mbalimbali nchini. Utoaji wa vyeti vya vijiji unaendelea na vijiji vyote vilivyopimwa mipaka yake vitapata vyeti kabla ya kilele cha maadhimisho tarehe 9 Desemba 2011.
Ndugu wananchi, wakati tunapata Uhuru, Mwaka 1961, jumla ya hati 14,448 za kumiliki ardhi zilikuwa zimesajiliwa. Hati hizo zilikuwa zimetolewa katika maeneo ya kati ya miji na maeneo ya mashamba makubwa ya mkonge, kahawa, na chai yaliyokuwa yanamilikiwa na wageni. Baada ya Uhuru hadi sasa, kuna jumla ya hati milki 379,000 zilizosajiliwa na kutolewa kwa wananchi. Aidha, ili kurahisisha utoaji wa hati ofisi za Usajili zimeongezeka kutoka moja iliyokuwepo wakati wa Uhuru hadi kuwa na Ofisi za Usajili za Kanda 6 zilizoko Dar es Salaam, Mwanza, Moshi, Dodoma, Mbeya na Mtwara.
Ndugu wananchi, huduma za upimaji ardhi hapa nchini zilianza toka miaka ya 1890. Ili kiumarisha fani hii, Serikali ilianzisha Halmashauri ya Wapima ambapo hadi sasa jumla ya wapima ardhi 225 wamesajiliwa. Pia, kwa kushirikiana na Halmashauri nchini, jumla ya viwanja 900,000 na mashamba 20,883 vilipimwa katika miji mbali mbali nchini. kwa kutumia mfuko wa upimaji na mradi wa viwanja mijini. Mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 iliyopita ni pamoja na kubadilisha mfumo wa utayarishaji ramani kutoka analojia kwenda dijitali, kutumia picha za satelaiti badala ya picha za anga kuhuisha ramani, kuanzishwa kwa vituo 5 vya upimaji wa moja kwa moja kwa kutumia satelaiti na kuweka alama mpya 1,327 za msingi za upimaji ardhi, kukamilisha upimaji wa mipaka ya eneo la kiuchumi katika Baharini (EEZ). Aidha, wizara imeanzisha kanda 5 za ukaguzi na uidhinishaji wa kazi za upimaji.
Hadi mwaka 2010 ramani zote zilikuwa zinaidhinishwa Dar es Salaam. Ili kurahisha upimaji wizara ina mango wa kuanzisha Kituo cha kupokea picha za satellite hapa nchini kitakachojengwa mjini Dodoma.
Ndugu wananchi, upangaji na uendelezaji wa miji ulianza toka enzi ya ukoloni. Wakati tunapata Uhuru, kulikuwepo na Miji 31. Baada ya miaka 50 kuna Miji rasmi 118, Vituo vya biashara (Minor Settlement/trading Centres) zaidi ya 200 .Kati ya Miji hiyo Majiji ni 5, Manispaa 18, Miji 6 na Miji midogo 95. Aidha, katika miaka ya sitini Mji uliokuwa na Mpango Kabambe ni Dar es Salaam pekee, Miji mingine ilikuwa na Mipango ya kina (Planning Schemes). Hivi sasa Miji ya Mikoa 19 imeandaliwa Mipango ya muda mrefu (Master Plans) na Miji midogo 48 imeandaliwa Mipango ya muda mfupi (Interim Land Use Plans). Sambamba na hilo kuna Mipango ya Uendelezaji Upya ya Makazi (Redevelopment Schemes) ambayo imeandaliwa katika miji mikuu ya Mikoa 17 (Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mbeya, Mwanza, Moshi, Iringa, Sumbawanga, Lindi, Mtwara, Kigoma, Morogoro, Singida, Shinyanga, Musoma, Tabora na Songea) kwa nchi nzima. Mipango ya kina ya Mipango ya Miji iliyoandaliwa nchi nzima kuanzia mwaka 1960 hadi 2011 ni 4,363 ambayo imeweza kuzalisha viwanja 1,802,015 kwa matumizi mbalimbali ya Miji. Juhudi za kuendelea kupanga zitapanuliwa mpaka ngazi ya kijiji ili kuleta ufanisi katika matumizi endelevu ya ardhi nchini.
Ndugu wananchi, kutokana na ongezeko kubwa la watu katika miji yetu, ujenzi wa makazi umekuwa ukienda kwa kasi kubwa kulinganishwa na kasi ya upangaji miji. Hali hii imesababisha ongezeko kubwa la makazi holela mijini. Katika jitihada za kuboresha makazi nchini, ulianzishwa Mpango wa kurasimisha ardhi na nyumba. Hadi Juni 2011, jumla ya nyumba 301,961 zilitambuliwa kwenye maeneo yaliyojengwa bila kupangwa katika miji ya Mwanza, Dar es Salaam, Moshi, Dodoma na Tanga. Kati ya nyumba zilizotambuliwa, jumla ya leseni 92,565 zilitolewa. Ili kukabiliana na tatizo hili, Serikali itaongeza juhudi za kupanga miji na kuwezesha upatikanaji wa makazi yaliyopangwa mjini kukidhi mahitaji. Natoa wito kwa wananchi kacha kujenga kwenye maeneo yasiyopimwa.
Ndugu wananchi, maendeleo ya nyumba yanajumuisha upatikanaji wa ardhi, miundombinu, upatikanaji wa fedha, upatikanaji wa vifaa vya ujenzi na nguvu kazi. Hali ya nyumba na upatikanaji wa miundombinu imebadilika sana tangu mwaka 1961. Kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita tangu kupata uhuru, Serkali imekuwa na sera stahiki ya uwezeshaji (enabling approach) wananchi kujijengea nyumba, kuwahakikishia milki salama, kurekebisha na kujenga miundombinu katika makazi yaliyojengwa bila kuzingatia mipango miji lakini ambayo hayakuendelezwa kwenye maeneo hatarishi kimazingira. Licha ya ongezeko kubwa la watu mijini kutoka watu takriban laki 4.5 mwaka 1961 walikuwa wanaishi mijini hadi watu wanaokadiriwa kuwa milioni 15 leo hii. Sera hii imeepusha tatizo la kuwa na watu wasio na makazi kabisa.
Kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa wananchi wameweza pia kuchangia katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, umeme, elimu, afya na uondoshaji wa maji taka na taka ngumu. Kutokana na juhudi za pamoja leo hii, asilimia 77 ya kaya zilizopo mijini zinapata maji kutoka kwenye vianzo salama (bomba au kisima).
Serikali imeweza pia kuboresha hali ya makazi kwa kujenga miundombinu, barabara, mifereji ya maji ya mvua, umeme, maji na mfumo wa uondoshaji wa taka katika miji mbalimbali, ukiwemo ule wa Urban Sector rehabilitation Project uliotekelezwa katika miji ya Arusha, Moshi, Morogoro, Tanga, Mbeya, Iringa na Mwanza. Mradi mwingine ni ule wa Community Infrastructure Upgrading Programme unaondelea kutekelezwa Jijini Dar es Salaam katika makazi 30 tofauti ambao unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 200,000. Serikali inaendelea kuboresha sera na sheria ili kuimarisha mazingira ya kuwezesha wananchi kuwa na nyumba na makazi bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuvutia benki za biashara na vyombo vingine vya fedha kutoa mikopo ya nyumba.
Ndugu wananchi, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ni Shirika la kwanza kuanzishwa nchini baada ya uhuru wa Tanganyika 1962. Shirika lilianzishwa kwa lengo la kuwapatia wananchi makazi bora kutokana na Serikali kuthamini makazi bora kuwa ni jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu. Katika kipindi cha miaka 50, Shirika limejenga jumla ya nyumba 17,168 za makazi, upangishaji na majengo ya ubia na sekta binafsi katika maeneo mbalimbali nchini. Katika kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano ijayo, Shirika lina mpango wa kujenga 15,000
Ndugu wananchi, katika jitihada za kutatua migogoro ya ardhi na nyumba, Serikali ilitunga Sheria ya mahakama za Ardhi iliyowezesha kuundwa kwa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 39 katika ngazi ya Wilaya na Mkoa. Hadi sasa, umeanzishwa mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi na nyumba kuanzia ngazi ya kijiji. Kuanzishwa kwa mabaraza haya kumewezesha mashauri ya ardhi na nyumba kushughulikiwa kwa muda mfupi, kusikilizwa na kuamliwa. Toka Mabaraza haya yaanzishwe mwaka 2004, jumla ya mashauri yaliyoamuliwa ni 39,000 kati ya mashauri 54,760 yaliyofunguliwa. Idadi hii ni kubwa ukilinganishwa na mashauri yaliyowahi kuamuliwa hapo awali.
Ndugu wananchi, ili kuwa na matumizi ya ardhi endelevu mijini na vijijini, Serikali iliunda Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi mwaka 1983. Tangu Tume ilipoundwa, imewezesha uaandaaji wa wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya 38 nchini. Aidha katika kipindi hicho, Tume kwa kushirikiana na Halmashauri za vijiji imefanikisha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 1,000 katika wilaya 78 kwenye mikoa 20 ya Tanzania bara. Pia Tume imeandaa Mpango wa Taifa wa matumizi ya ardhi kwa miaka 30 ijayo, ambao unabainisha matumizi ya ardhi kwa kila kipande cha ardhi nchini. Mpango huu unagusa sekta zote zinazotumia ardhi kama vile maji, barabara, kilimo, mifugo, mali asili, nishati na madini n.k
Ndugu wananchi, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50. Sekta ya ardhi na nyumba inakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo ni chachu ya mafanikio ya sekta katika miaka 50 ijayo. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wananchi na wadau kuhusu Sheria, Kanuni na Miongozo kuhusu masuala ya Ardhi, kuwepo kwa migogoro mbalimbali ya ardhi inayokwamisha kuwapa wananchi hati za kumiliki maeneo yao, kasi ndogo ya kuanzisha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ilikinganishwa na idadi ya Wilaya ambazo zinahitaji huduma hii, kuwepo kwa ongezeko la ujenzi holela mijini ambapo asilimia zaidi ya sabini ya makazi mijini wanaishi katika maeneo yasiyopimwa, riba kubwa ya asilimia 17-18 inayotozwa na vyombo vya fedha vinavyotoa mikopo ya nyumba, kunakosekana vivutio vya kushawishi sekta binafsi kuwekeza kwenye sekta ya nyumba na kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi na hivyo kufanya gharama za ujenzi kuwa juu n.k.
Ndugu wananchi, ili kukabiliana na changamoto hizo wizara inayo mikakati na mipango thabiti ambayo itatekelzwa. Mipango hiyo inapatikana kwenye vipeperushi mbalimbali vilivyosambazwa na katika mpango ya serikali wa miaka mitano.
Ndugu wananchi, naona niishie hapa na niwaalike kuungana nasi katika maonesho haya ili muone kazi za wizara na mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia. Kwa nafasi hii naomba kuwashukuru tena kuungana nasi katika siku hii ya ufunguzi. Lengo la juhudi zote hizi ilikuwa ni kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu uendelezaji wa miji, nyumba na dhana ya ardhi ni mtaji kutoka katika hali ya mtaji mfu kwa la kupunguza umasikini wa mtanzania mmoja mmoja hadi katika kuchangia pato la taifa.
Sasa kwa heshima na taadhima naomba nifungue rasmi maonesho haya na niwakaribishe wote kutembelea mabanda na kujifunza mambo mbalimbali ya sekta ya ardhi. Kauli Mbiu ya Kitaifa ya maadhimisho haya ni “Tumethubutu kuwa na ardhi ambayo ni mtaji na ni mali, Tumeweza kuiendeleza na Tunazidi Kusonga Mbele katika kuendeleza ardhi yetu kwa manufaa ya watanzania wote.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment