FOLLOWERS

Tuesday, September 4, 2012

SERENGETI BOYS WAONDOKA KUELEKEA MBEYA KWA AJILI YA KAMBI

Timu yetu ya taifa ya vijana wa umri wa chini ya miaka kumi na saba (U.17) Serengeti Boys, wameondoka leo asubuhi kwenda mkoani Mbeya kuendelea na maandalizi ya kufuzu fainali za vijana zitazofanyika nchini Morocco mwaka 2013. Timu yetu imepangiwa kupambana na timu ya taifa ya vijana wa Misri (Egypt) katika hatua inayofuata, pambano hilo linatarajia kufanyika Oktoba 2012. Timu yetu ilipata ushindi baada ya timu ya vijana ya Kenya kujitoa kwenye michuano hii.

Timu imekwenda mkoani Mbeya kwa mwaliko wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wilaya ya Mbeya Mjini (MUFA), ikiwa huko chama hicho kitaihudumia kwa malazi, chakula na huduma nyingine ndogondogo. Timu inategemea kupangiwa michezo kadhaa ya majaribio na timu kabambe za mkoani humo ikiwemo Mbeya City, Tanzania Prisons na timu za kombaini.

Shirikisho la  Mpira wa Miguu nchini linapenda kutumia fursa hii kuishukuru na kuipongeza MUFA, kwa kuonyesha mfano unaostahili kuigwa na wadau wengine, wa kushirikiana katika maandalizi ya kuziandaa timu zetu za taifa. Kitendo hicho kinaonyesha kuguswa, uwajibikaji, uzalendo na ukomavu katika kutatua matatizo kwa vitendo na sio kwa lawama bila suluhisho.

Shirikisho pia linaishukuru benki ya NMB kwa kutoa msaada wa jezi seti moja na fedha sh. Millioni tano, zilizowezesha vijana hawa kupata posho zao za kambi na kusafiri kwenda Mbeya. Itakumbukwa kuwa benki ya NMB imekuwa na mchango mkubwa sana katika maendeleo ya soka ya vijana kwa muda mrefu sasa. Kwa kipindi cha miaka sita (2006-2010) iliyopita ilidhamini mafunzo ya makocha wanaojihusisha na program za maendeleo ya vijana nchini, vilevile ilitoa mipira ya program za vijana kwa vyama vya mikoa. Hivyo tunaishukuru kwa kuthamini mchango wao huo na kwa kuendelea kutoa msaada ili kuhahakisha inalinda mafanikio ya program hizo.

Shirikisho linapenda kuwaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia kuwaandaa vijana wetu hawa pekee waliobaki kwenye mashindano. Mafanikio ya timu yetu ya taifa (Taifa Stars) siku za usoni yanategemea sana msingi bora wa vijana hawa. Hivyo ni vema tukashirikiana kama walivyojitokeza MUFA na NMB.

Husiti kueleza bayana kuwa kama si wadau wa kambi ya vijana ilikuwa inavunjika, na baada ya kurudi Mbeya kama hakutakuwa na wadau wengine watakaojitokeza basi uwezo wa kuendelea na kambi ya maandalizi kwa vijana wetu utakuwa finyu mno.

Shirikisho lina imani kuwa wakazi wa Mbeya watatoa ushirikiano wa hali ya juu wakiongozwa na Chama cha Mpira cha Mkoa (MREFA), kwa Serengeti Boys ili kufanikisha maandalizi hayo.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...