Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM
Makala hii nimeshaichapisha mara kadhaa katika hii blogu yangu, na
imewahi kuchukuliwa na kuchapishwa na mitandao mingine pia. Nimeona
niiweke tena hapa.
--------------------------------
Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi
katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia
jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama
wa Taifa.
Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima
ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo
mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika
uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:
Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi
ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya
Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi
wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua
Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM.
Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)
Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:
Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha
Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza
kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala
ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza
tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama
kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au
ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa
kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao.
Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote
za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na
bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki
kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya
kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi!
(Ukurasa 66)
Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi
wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni
mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.
(KWA HISANI YA HAPA KWETU BLOG)
|
No comments:
Post a Comment