FOLLOWERS

Friday, August 10, 2012

SIMULIZI : Nilikula nyama za ndugu zangu wa damu 19 (Sehemu ya Kwanza)

Jina langu ni Esther, kwa sasa nina umri wa miaka 22. Nimeokoka na Ninampenda Yesu, na ningependa nitoe ushuhuda wa namna “Nilivyokula Nyama za ndugu zangu wa damu 19″. Ni ngumu sana kuamini ukweli huu lakini namshukuru sana Mungu kwa kunipa ujasiri kwa kulizungumzia hili mbele ya watu.
Simulizi yangu inaanzia hapa, “Nilizaliwa Sumbawanga Mkoani Rukwa miaka 22 iliyopita nikiwa kama Mtoto pekee katika familia yetu ingawa wazazi wangu walikuwa wakiishi Dar maeneo ya Tegeta. Mama yangu alipokuwa mjamzito wa Mimba yangu, ilimlazimu kusafiri kuelekea Sumbawanga kwa Wazazi wa Baba yangu yaani Bibi na Babu yangu ili akajifungulie huko kwa Maana kwa hapa Dar es saalam hatukuwa na ndugu yeyote ambaye angeweza kumuhudumia Mama pindi atakapojifungua, na Baba yangu asingeweza kushinda nae pale nyumbani kwani alikuwa amejiajili yeye mwenyewe hivyo wangekosa hela ya kula.
Wakati Mama yangu anasafiri kuelekea Sumbawanga, ujauzito wangu ulikuwa ni wa Miezi 8. Hivyo mwezi 1 baadae nikazaliwa nikiwa Mwenye afya njema kabisa. Ilikuwa ni furaha kwa kila mmoja kuona Mama amejifungua Salama na mtoto pia niko Salama. Kwa furaha waliyokuwa nayo Baba yangu na Mama yangu walipendekeza Jina langu niitwe Esther jina ambalo ni la Bibi yangu mzaa Baba. Bibi alifurahi sana na kumuahidi Mama yangu kuwa atakuwa rafiki yangu wa karibu sana kwa maana nimepewa jina lake.
Mama yangu aliishi pale kwa Bibi na Babu yangu kwa muda wa kama Miezi 3 hivi, hivyo nikiwa na  Umri wa miezi 2 Mama yangu alirudi jijini Dar es salaam ili kuungana na Baba tena. Maisha yao hayakuwa mabaya sana wala mazuri sana, mana waliishi kwenye chumba kimoja cha kupanga na swala la chakula pia halikuwa likiwapa shida sana kwani wote walivumiliana kwa kila hali.
Nikiwa na Umri wa Mwaka 1 na miezi kadhaa, Mama yangu aliugua ugonjwa wa Kansa ya Kizazi jambo lililomfanya atokwe na damu nyingi sana sehemu za siri. Baba alijitahidi kwa hali na mali ili aweze kurudisha afya ya Mama katika hali nzuri lakini cha kusikitisha ni kwamba kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo hali ya Mama ilizidi kwa Mbaya.
Ilipita kama Miezi 8 hivi toka Mama apate ugonjwa huo, na tarehe 21 July 1992 Mama yangu alifariki akiwa nyumbani kwetu maeneo ya tegeta. Lilikuwa ni pigo kubwa sana kwa Baba yangu kwani kipindi hicho nilikuwa na Umri wa kama Miaka 2 na miezi kadhaa hivi hivyo alifikiria sana ni kwa namna gani ataweza kunilea.
Maiti ya Mama yangu ilipelekwa hospitali huku Baba akifanya mazungumzo na Mwenye nyumba ili Msiba ufanyike pale kwake. Kwa kuwa mwenye nyumba alikuwa ni mtu muelewa na aliishi vizuri sana na wazazi wangu hivyo alimkubalia msiba ufanyike pale huku Baba akikusanya Michango mbalimbali ili kuweza kusafirisha Maiti ya Mama yangu mpaka mkoani Mbeya kwani ndipo wazazi wa Mama yangu walikokuwa wakiishi.
Michango ilikusanywa na hatimaye Maiti ya Mama yangu lipenzi ikasafirishwa hadi Mkoani Mbeya kwa ajili ya Kuagwa na Wazazi wake na pia kufanya mazishi. Ilichukua kama siku 2 kwa kumilika kwa zoezi zima la kuaga pamoja na kumzika Mama yangu toka tulipofika Mbeya.
Baada ya Msiba kuisha Baba aliaga na kunichukua Mimi tukaenda wote mpaka Sumbawanga kwa Bibi na Babu yangu mzaa Baba. wakati wa kuondoka kuelekea Sumbawanga Bibi mzaa Mama yangu alimsihi sana baba aniache niwe nakaa pale kwao mana kulikuwa na Watoto wengine wawili wa mama yangu mkubwa ambaye alifariki miezi mitano iliyopita.
Baba yangu aligoma kuniacha pale kwa madai kuwa angeongeza mzigo kwa Bibi na babu yangu hivyo akaamua kunipeleka kwa Bibi na Babu mzaa baba. Tulifika kule salama na kupokelewa vizuri, na wote walianza kulia kwa msiba uliotokea. Baadae majonzi yaliisha na Mazungumzo kuhusu mimi yalianza siku ya pili yake kwani Baba alitaka kuwahi kurudi Dar kwani alidai kuwa vitu hakuviacha vizuri wakati akisafiri na msiba kuelekea Mbeya.
Bibi yangu aliafikiana na Baba yangu kwamba nianze kuishi pale kwao na alimuhakikishia Baba kwamba asiwe na wasiwasi kwani kila kitu kitakuwa sawa tu. Wakati wote wa kikao Babu yangu alikuwa kimyaaa huku akimuangalia tu baba kwani wakati huo afya ya Babu yangu haikuwa nzuri sana kutokana na Uzee aliokuwa nao wakati huo. Mwisho wa kikao Babu alimwambia Baba yangu jambo moja tu, “Jikaze huo ndio uanaume”.
Baada ya Kikao hicho baba yangu aliniacha mikononi mwa Bibi na yeye akasafiri kurudi Dar na kuahidi kuja tena wakati mwingine.
Pale kijijini, Ilinichukua muda kidogo kuzoea mazingira yale kwani yalikuwa tofauti na ya Dar na pia ilinilazimu kutafuta marafiki wapya wa kucheza nao kwani pale nyumbani nilikuwa nikiishi Mimi, Bibi na Babu yangu.
Nikiwa na Umri wa Miaka 7 nilianza darasa la kwanza, kwani Baba alikuja kushughulikia maswala hayo ya shule na baadae akarudi tena Jijini dar. Miezi michache baada ya kuanza shule, siku 1 usiku sana nilishangazwa na ujio wa Bibi yangu  chumbani kwangu. Wakati huo nilikuwa nimelala tu kitandani ila usingizi ulikuwa umekatika kwa muda hivi.
Nilishangaa kuona ameingia chumbani kwangu pasipo mimi kumfungulia mlango, na baada ya muda kidogo aliniamsha na kuniambia kwamba kuna sehemu anataka twende wakati ule. Niliogopa sana na kumuomba bibi tumuamshe Babu ili twende nae mana ilikuwa ni usiku sana. Bibi alinikatalia kumuamsha Babu na kunilazimisha twende peke yetu.
Je! Nini kitaendelea? Ni wapi Bibi yake Esther anataka kwenda na Esther usiku wote ule? Na kwanini hataki waende na Babu yake Esther? Usikose muendelezo wa Simulizi hii ya Kusisimua ambayo naamini utajifunza kitu juu ya namna Nguvu ya Mungu ifanyavyo kazi.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...