HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI MHE. MCHUNGAJI PETER
MSIGWA, (MB) WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO
NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013.
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi rasmi ya Upinzani,nakushukuru kwa
kunipa nafasi hii ya kuwasilisha Maoni na Mapendekezo ya Kambi rasmi
rasmi ya upinzani bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2012/2013, kwa mujibu
wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(3) na (7) toleo la 2007.
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kutoa pole kwa msiba mkubwa
wa jirani yangu mama KISILO ambaye amefariki tar 7 Julai na kutokana na
majukumu ya kibunge nimeshindwa kuhudhuria mazishi, pia wananchi
waliopoteza maisha kutokana na ajali mbaya ya basi la Sabena iliyotokea
Tabora ,Mungu aziweke roho za marehemu mahala pema peponi.
Mheshimiwa Spika, Napenda nichukue fursa hii kuwakumbusha wapiga kura
wangu wa jimbo la Iringa mjini, Kama nilivyoapa kuilinda na kuitetea
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nitaendelea kusema ukweli bila
kujali cheo cha mtu,rangi,kabila wala dini yake kama maneno ya kiongozi
wa taifa la India marehemu Mahatma Ghandhi alivyowahi kutuasa akisema
maneno yafuatayo;
“….Many people especially ignorant people, want to punish you for
speaking the truth, for being correct for being you... Never apologize
for being correct or being years ahead of your time, if you are right
and you know it, speak your mind even if you are a minority of one, the
truth is still the truth”.
Kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi …Watu wengi hasa watu
wajinga,wanataka kukuadhibu kwa kusema ukweli,kwa kuwa sahihi,kwa kuwa
na msimamo binafsi,Kamwe usiombe radhi kwa kusema ukweli au kwa kuwa
mbele ya wakati. Kama upo sahihi na unafahamu hivyo sema, hata kama Ni
pekeyako, ukweli utabaki kuwa ukweli.
Mheshimiwa Spika,Dira ya Wizara hii ni kuhakikisha utunzaji endelevu wa
maliasili, utamaduni na Utalii na kuhakikisha ushirikishwaji wa jamii
zinazohusika, mashirika yasiyo ya kiserikali na kusimamia matumizi ya
maliasili kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mheshimiwa Spika, hali halisi imeendelea kuwa kinyume chake, Watanzania
ndani ya nchi hii, yenye utajiri mkubwa wa misitu na mbuga nyingi za
wanyama, milima na mabonde ya kuvutia, wameendelea kuwa maskini hata
baada ya miaka 50 ya uhuru wa nchi yao.
Mheshimiwa spika, pamoja na mambo mengine jukumu la wizara hii ni
kuandaa sera na mikakati ambayo itaongoza utunzaji endelevu wa
maliasili, utamaduni na mazingira. Kuinua na kuongeza aina ya vivutio
vya utalii na kuongeza mchango wa sekta hii kwa pato la taifa na
uingizaji wa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri wizara imeshindwa kusimamia sera na
mikakati ya kuendeleza maliasili, utamaduni na mazingira kama
iliyojiwekea, moja Wizara imeshindwa kuvutia watalii zaidi, pili
imeshindwa kulinda misitu na kuacha misitu ikiteketea, tatu imeshindwa
kulinda wanyamapori ambao wameendela kuibiwa na kuuwawa, nne idara ya
wanyapori imeendelea kudhoofishwa na kushindwa kutekeleza majukumu yake
kama inavyotakiwa hasa kutokana na Waziri mwenye dhamana kuacha nafasi
muhimu za maamuzi katika idara hii zikikaimiwa na watendaji mbalimbali
ambao wameshindwa kuwa na maamuzi hivyo kuleta urasimu usiokua na tija
kwa taifa, na tano Wizara kushindwa kutunza mlima Kilimanjaro ambao
theluji imeendelea kuyeyuka huku hakuna mkakati wa makusudi kuokoa mlima
huo.
2.0 SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu J.K. Nyerere aliwahi kusema, nanukuu; “Uhai wa
wanyamapori ni jambo linalotuhusu sana sote katika Afrika. Viumbe hawa
wa porini, wakiwa katika mapori wanamoishi, sio muhimu tu kwa ajili ya
kuajabiwa na kuvutia lakini pia ni sehemu ya maliasili yetu na pia ndio
mustakabali wa maisha yetu ya baadaye. Kwa kukubali dhamana ya
wanyamapori wetu tunatamka kwa dhati kwamba tutafanya kila tuwezalo
kuhakikisha kwamba wajukuu wa watoto wetu wataweza kufurahia urithi huu
mkubwa na wa thamani adimu.”
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM siyo tu imeshindwa kuwalinda
wanyama wake na vivutio vya asili bali pia imeshindwa kuwalinda raia
wake na kwenda kinyume kabisa na dhana ya Mwalimu Nyerere. Tangu
tulipopata uhuru,tumeshuhudia raia wengi kupoteza maisha kwa kuuwawa na
ajali mbalimbali ambazo zimesababishwa na Serikali dhaifu na zembe ya
CCM mfano meli za Mv Victoria, Mv Skagit,Mv Spice Islander, mabasi na
pikipiki na matukio mengine kadha wa kadha ambayo tukiyaorodhesha hapa
muda hautotosha. Kama vile haitoshi watanzania na dunia nzima
tumeshuhudia wanyama wakiporwa na kusafirishwa nje ya nchi, tembo
kuuwawa kwa kasi kubwa huku Serikali hii ikiendelea kukaa kimya na
kutokua na majibu wala mikakati hasa ya kukabiliana na ujangili.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utamaduni uliojengeka na serikali ya CCM
ya kutegemea misaada na kuwa ombaomba katika mataifa mbalimbali kinyume
na wosia aliotuachia hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba nchi
maskini haiwezi kuendelea kwa kutegemea misada kutoka nchi za nje,hali
hii imeendelea kulifanya Taifa kushindwa kulinda rasilimali zake na
kujikuta likiendelea na utamaduni wa kuomba hata vile tulivyojaliwa na
Mwenyezi Mungu kuwa navyo,mfano hivi karibuni Tanzania na Dunia nzima
imeshuhudia Waziri wa Maliasili na Utalii,Mh Balozi Hamis Kagasheki
akifurahia kupeana mikono na Balozi wa Uingereza akipokea Faru watatu
kutoka uingereza kana kwamba ni jambo la kujivunia huku Tanzania
ilipaswa kuuza na kugawa Faru kwa nchi hizo za kigeni.
Mheshimiwa spika, takwimu zinaonesha mwaka 2008 hadi mwaka 2012 Mei
taifa hili limekwisha poteza Tembo takribani 881,udhaifu huu wa
ulindaji wa wanyama hawa umetokana na serikali kutotambua umuhimu wa
kulinda rasilimali hizi na kuweka kipaumbele katika kuhakiki usalama wa
wanyama hao, kitu ambacho ni mshangao kwa mfugaji anaetegemea kupata
mazao pasipo kuwalisha mifugo wake.
Kambi rasmi ya Upinzani, inataka kujua serikali imechukua hatua gani
mpaka sasa kwa wale wote waliohusika kwa njia moja ama nyingine na vifo
vya wanyama hawa na kuliingizia taifa hasara kubwa.
2.1 WATUMISHI IDARA YA WANYAMAPORI
Mheshimiwa Spika , mahitaji halisi ya watumishi katika idara ya
wanyamapori ni watumishi 4,588 huku idara ikiwa na watumishi 1,044,hivyo
kufanya idara kuwa na upungufu wa watumishi 3,544 sawa na upungufu
wa asilimia 77, matokeo yake ni kupelekea askari mmoja alazimike
kufanya doria katika eneo la kilometa za mraba 159.75 badala ya kiwango
kinachokubalika kimataifa cha kilometa za mraba 25 kwa askari mmoja.
Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa ufafanuzi ni jinsi gani askari
hawa wanaweza kukabiliana na tatizo la ujangili katika hifadhi zetu za
wanyamapori? Na pia ni mkakati upi uliopo Serikali kukabiliana na
upungufu wa watumishi katika Idara ya Wanyamapori?
Mheshimiwa Spika, mtalaamu wa maswala ya ujangili wa kimataifa Dr Donald
Antony Mwitulubani wa idara ya Geografia ya chuo kikuu cha Dar Es
Salaam anasema katika mojawapo ya mada zake; “ Majangili hutumia udhaifu
uliopo katika taratibu za usafirishaji au uingizaji na kukosekana kwa
ushirikiano baina ya vyombo vya kutekeleza sheria kitaifa na
kimataifa,hutumia njia nyingi kuepuka kujulikana na kukamatwa,
hushirikiana na majangili wengine waliojizatiti zaidi kufanya ufisadi,
kutoa rushwa, kuingiza fedha chafu, madawa ya kulevya kumiliki na
kutumia silaha za moto”.
Ni dhahiri kwa maneno haya kuwa idadi ndogo ya askari iliyopo itaiwia
vigumu kuweza kukabiliana na majangili hawa kutokana na nguvu kubwa
walionayo na mitandao iliyopo pamoja na serikali kutokuwa na nia ya
dhati ya kukabiliana na ujangili uliokithiri.
3.0 SHUGHULI ZA UWINDAJI
Mheshimiwa Spika, suala la uwindaji kwa kuzingatia sheria bado
limeonekana kuwa na mapungufu kwa upande wa Serikali katika kusimamia
kwa ukamilifu, sheria na taratibu zinataka DGO’s (District Game
Officers) kuwepo wakati wa kutekeleza shughuli ya uwindaji. Limejitokeza
tatizo la uwindaji kukiuka taratibu katika kitalu cha uwindaji cha
Loliondo pindi Mfalme wa Uarabuni anapokuwa akifanya uwindaji pasipo
kuwepo kwa game officers kwa maelezo ya taratibu za kiitifaki, ambapo
game officers wameshindwa kutoa maelekezo ya aina ya wanyama wa kuwindwa
hivyo kupelekea wanyama kuwindwa ovyo pasipo taratibu za kitaalamu
kufuatwa, kwa mfano wanyama wajawazito nk.
Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa kanuni ya tano ya Kanuni za ukamataji
wanyama inamtaka mmiliki wa kibali cha kukamata wanyama kuripoti kwa
Afisa Wanyamapori wa wilaya husika kabla na baada ya ukamataji kufanyika
kwa lengo la kumuonyesha eneo la ukamataji, kusimamia zoezi la
ukamataji na baadye kusaini na kuweka muhuri katika hati ya ukamataji
(capture permit).
Mheshimiwa Spika, hata hivyo,masharti ya kanuni hii yameonekana kupuuzwa
pale wanyama wanapokamatwa,mfano maafisa kutoka kikosi cha kuzuia
Ujangili arusha(KDU), maafisa kutoka TAWIRI, maafisa kutoka CITES,Arusha
na mwakilishi wa kampuni ya Gumbo Reptiles wamekua wakikamata bila
kutoa taarifa kwa mamalaka za wilaya za Monduli.
Mheshimiwa Spika,Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuthamini
mali za umma na sio kuendeleza utamaduni wa kigeni wenye kutumia
rasilimali zetu bila kufuata taratibu tulizojiwekea kama taifa. Pia,
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo ni hatua zipi za
kisheria zinazochukuliwa dhidi ya tuhuma hizi na mikakati yake katika
kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho kwa wavunjaji wa Sheria na Kanuni za
uwindaji nchini.
3.1 ELIMU YA UWINDAJI WANYAMAPORI.
Mheshimiwa Spika, Sera ya taifa katika uwindaji imeainisha suala la
kuweka kipaumbele cha uwindaji kwa wawekezaji wa ndani hivyo kutoa
kipaumbele kwa watanzania kushiriki katika uwindaji wa wanyamapori.
Suala la uwindaji linahitaji taaluma ya uwindaji na taarifa rasmi za
masoko, na kutokana na mahitaji hayo watanzania wengi kutokuwa na vigezo
vya kushiriki katika uwindaji huo,Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka
serikali kutoa elimu ya kutosha kwa watanzania ili kuwawezesha kushiriki
vema katika kukuza uchumi kwa kushiriki moja kwa moja katika shughuli
za uwindaji wa wanyamapori.
3.2 Kuongezeka kwa idadi ya vitalu vya uwindaji.
Mheshimiwa Spika,Katika kipindi kinachomalizika, idadi ya wanyama
ilikuwa kubwa zaidi kulinganisha na idadi ya sasa ambapo tafiti
mbalimbali zimeonyesha kuwa wanyama wamekuwa wakipungua kadiri siku
zinavyokwenda. Pamoja na ukweli huu idadi ya vitalu imeongezeka na
wakati huo huo idadi ya wanyama wanaoweza kuwindwa kwa mwaka
haijaongezeka ( quota setting) , hii ina maana kuwa wanyama wengi zaidi
watawindwa kutokana na wingi wa makampuni yalivyo na hivyo kwenda
kinyume kabisa na Sera ya Taifa ya uhifadhi wa wanyama pori.
Kambi ya Upinzani , inataka kujua vigezo vilivyotumika katika kuongeza
idadi ya vitalu bila kuzingatia uhalisia na uwepo wa wanyama.
Mheshimiwa Spika, Pia vitalu vingine vimegawanywa bila kuzingatia
ikolojia ya eneo husika na haswa wakati wa kuweka mipaka baina ya vitalu
hivyo, hii nayo ni tishio kwa ikolojia na wanyama wanaoishi eneo husika
lililogawanywa bila kuzingatia uhalisia huu wa kitaalamu kwa mfano
kugawa eneo la kuwinda Mamba au Viboko ambao wanakaa eneo moja la maji
kwa kampuni mbili tofauti wakati wanyama hawa wanahama kulingana na
msimu wa mwaka ni jambo la ajabu kabisa.
Kambi ya upinzani, tunataka kupata maelezo ya kina juu ya ugawaji huu
kama ulizingatia vigezo na kama sivyo nini msimamo wa serikali katika
hili kwa sasa.
3.3 Ugawaji wa Vitalu Kutokuzingatia Sheria ya Uhifadhi Wa Wanyamapori .
Mheshimiwa Spika,Hii inatokana na ukweli kuwa kwenye baadhi ya maeneo
ambayo vitalu vimegawanywa na kuongezwa na kugawiwa kwa makampuni
mbalimbali, kulienda kinyume na sheria ya uhifadhi wa wanyama pori
kifungu cha 16 (Wildlife Conservation Act 2009 No.5 of 2009)
Mheshimiwa Spika, Kwa mfano ugawanyaji wa vitalu vilivyopo eneo la Ziwa
Natron umeenda kinyume na kifungu 16 (4 na 5). Vifungu hivi vinatamka
wazi kuwa Waziri hatagawanya eneo kwanza kabla ya kushirikisha Serikali
za vijiji kwenye eneo husika na kutangaza maeneo hayo kwenye Gazeti la
Serikali, pamoja na kifungu hicho bado Waziri aligawanya eneo hilo
kutoka vitalu viwili vya awali hadi kuwa vinne bila kuzingatia takwa
hili la kisheria.
Mheshimiwa Spika,Athari kubwa ya jambo hili ni kuwa wakati Waziri
amegawa eneo hilo kwa kampuni tofauti ameshindwa kuzingatia ukweli kuwa
vijiji husika vilikuwa tayari vimeshasaini mikataba na kampuni ya
Wengert Windrose Safaris (WWS) na kuwa walishakubaliana kuanzishwa kwa
WMA kwenye eneo hilo na hivyo aligawanya eneo ambalo hakuwa na mamlaka
nalo kisheria kwa wakati huo .
Kambi ya Upinzani,inataka kupata majibu ni kwanini wizara inashiriki kuvunja sheria zilizotungwa na Bunge hili.
3.4 Mapungufu ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji kwa kipindi cha 2013-2018
Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 38(14) cha Sheria ya Wanyama Pori
kinamruhusu mtu yeyote aliyekwazwa na maamuzi ya Waziri kumwandikia
waziri kuomba uamuzi huo kupitiwa upya. Kama tujuavyo, wadau wengi
walioathirika na maamuzi ya waziri waliomba uamuzi wa Waziri aliyepita
kuangaliwa tena. Kifungu 38(15) kinaendelea kueleza kwamba baada ya
maombi ya kutazama upya maamuzi yaliyopita, Waziri atawasilisha maombi
hayo kwenye Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji kwa
ajili ya kupata maoni na mapendekezo ya Kamati. Baada ya kupokea maoni
na mapendekezo ya Kamati.
Mheshimiwa Spika,bado dhana ya utawala bora inashindwa kufikiwa na
Serikali katika kutekeleza majukumu yake katika wizara ya maliasili na
utalii hasa kwa kuendelea kuwa mgawaji wa maeneo ya vitalu vya uwindaji
wa kitalii kama ilivyopendekezwa kabla kuwepo na mamlaka tofauti
itakayotekeleza jukumu hilo kisheria na Wizara kubaki kuwa msimamizi wa
utekelezaji wa Sera.
Kambi ya upinzani, inaitaka Serikali kuona umuhimu wa kubaki kuwa
msimamizi wa utekelezaji wa Sera ili kuleta tafsiri sahihi ya utawala
bora kiutendaji katika swala la mgawanyo wa madaraka,hii itaweza walau
kuijengea heshima serikali hii dhaifu ya CCM ndani na nje ya nchi katika
kuwaletea wananchi mfumo sahihi wa utawala bora kwa kutenda.
3.4 Uwazi katika mchakato wa kutenga vitalu vya uwindaji
Mheshimiwa spika, Kifungu cha 38(11) cha Sheria ya Wanyama Pori
kinaeleza kwamba mchakato wa kutenga na kugawa vitalu vya uwindaji
utakuwa wa wazi, unaoweza kuhojiwa, wenye kuzingatia haki, usawa na wa
maridhiano. Waziri hakuweza kutoa sababu kwa wadau ni kwanini wadau
walinyimwa vitalu walivyokuwa wameomba. Wakati wadau walipoomba taarifa
kuhusu vitalu vya uwindaji waliambiwa kwamba taarifa hizo ni za siri.
Hii sio haki kwa mujibu wa kifungu 38(11) cha Sheria ya Wanyama Pori
ambacho kinamtaka Waziri kusimamia mchakato huo kwa uwazi kadiri
iwezekanavyo ili kudumisha utawala bora. Kambi rasmi ya Upinzani
inahoji uwazi wa Waziri katika kutoa taarifa kwa wadau hasa wale
waliokosa kwa kigezo cha unyeti wa taarifa hizo huku sheria ikitaka
mchakato huo kuwa ni wa uwazi.
3.5 Idadi ya Wanyama katika Eneo la Uwindaji
Mheshimiwa Spika, Sheria inamtaka Waziri kutoa taarifa za kina na ramani
zinazoonesha eneo la uwindaji na mipaka yake kwa vipindi vya uwindaji
baada ya Sensa ya Wanyama itakayokuwa imefanywa na Wizara. Kifungu cha
44(1) cha Sheria ya Wanyamapori kinaeleza kwamba kwa madhumuni ya
kumshauri Mkurugenzi namna ya kuanzisha eneo la uwindaji, Waziri atateua
kamati ya wajumbe wenye ujuzi na uzoefu wa masuala ya Usimamizi wa
Wanyamapori. Kamati hii haikuundwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani imeona kuwa jambo hili
lilisababisha ugawaji holela wa vitalu vya uwindaji na kuacha maeneo
mengine bila wanyama. Udhaifu huu umesababisha wadau kutegemea sensa ya
wanyama iliyofanywa na mipaka ya vitalu vya uwindaji iliyofanya na watu
binafsi kwa uzoefu wao. Kambi rasmi inaitaka Serikali, kwa kupitia
waziri wake kutoa majibu juu ya usimamizi wake katika kuhakikisha Sheria
zinafatwa, na ni vipi ugawaji wa vitalu haukuhusisha kamati kama Sheria
inavyoainisha hivyo kufanya zoezi hili la ugawaji wa vitalu kuwa
batili.
Mheshimiwa Spika, Waziri alifanya maamuzi lakini maamuzi hayo kwa kiasi
kikubwa hayakuzingatia maoni na mapendekezo ya Kamati. Hii ilithibitika
kutoka katika taarifa iliyopita iliyosomwa na kamati ya Bunge ya Ardhi
Maliasili na Mazingira. Ikitokea wadau hawa ambao hawakuridhika wakaamua
kuupinga uamuzi wa Waziri wa kugawa vitalu vya uwindaji kwa kipindi cha
2013-2018 kama ulivyokiuka kifungu 38(16), Serikali itashindwa vibaya
na itasababisha matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kulipa fidia
kampuni husika.
3.6 Utafiti na Maendeleo ya Maeneo ya Uwindaji
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa kifungu cha 37 cha Sheria ya Wanyama
Pori Waziri alitakiwa kuagiza usimamizi wa mazingira na ukaguzi wa
miradi ya mazingira au shughuli mbalimbali zinazofanywa katika vitalu
mbalimbali vya uwindaji. Ukaguzi huo haukufanywa na Waziri kama Sheria
ilivyomtaka.
Mheshimiwa Spika,Zaidi ya hilo, Kanuni ya 3(1) inasema kwamba,
Mkurugenzi ataanzisha maeneo katika Hifadhi za Wanyama Pori, maeneo
tengefu ya wanyama pori na maeneo mengine nje ya maeneo yanayolindwa ili
yageuzwe kuwa vitalu vya uwindaji ili mradi kwamba vitalu vya uwindaji
vilivyotengwa katika maeneo ya usimamizi wa Wanyama Pori vitaidhinishwa
pamoja na Mpango wa Kanda wa Usimamizi wa Rasilimali au Mpango Mkuu wa
Usimamizi wa maeneo husika ya Wanyama Pori. Mipango hii ya usimamizi wa
rasilimali wa Kanda na Mpango Mkuu wa Usimamizi haijatekelezwa na Waziri
kama kifungu cha 34(2) cha Sheria kinavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa kifungu 38 (10) cha Sheria ya Wanyama
Pori, mambo yote yanayohusu madaraja , ukubwa na ubora wa vitalu vya
uwindaji yameainishwa katika kanuni.
Taarifa hizi zilitolewa chini ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za 2010
kwa njia ya jedwali dogo kwa kuonesha tu namba ya daraja na vitalu vya
uwindaji vilivyokuwa katika madaraja hayo. Waziri hakueleza ni kwanini
madaraja kadhaa ya vitalu vya uwindaji yalitengwa maalumu kwa kipindi
cha uwindaji kutoka 2013 -2018. Taarifa pekee iliyotolewa ilihusu ukubwa
wa kitalu cha uwindaji lakini taarifa ya sababu za kuchagua kitalu cha
uwindaji na ukubwa wake hazikutolewa.
3.8 Ajira Kutolewa kwa wageni kutoka nje ya Nchi.
Mheshimiwa Spika,Kutokana na kukosekana kwa wataalamu waliobobea kwenye
sekta hii nchini mwetu ,kumesababisha nafasi nyingi za ajira kutolewa
kwa wataalamu kutoka nje ya nchi na hivyo vijana wa kitanzania wenye
sifa stahiki wanajikuta wanakosa fursa za kupata ajira za kitaalamu
kwenye sekta hii na kubakia na ajira za kawaida kama kuwinda na
kuhifadhi tuu .
Mheshimiwa Spika, Hali hii inapelekea fedha nyingi za kigeni kulipwa na
kupelekwa nje ya nchi na hivyo kulikosesha taifa fedha za kuendeleza
miradi mingine mbalimbali na hali hii imesababishwa na ukosefu wa vyuo
vya kutoa elimu ya juu kwenye masuala ya uwindaji nchini mwetu.
Mheshimiwa Spika, Umakini wa kimataifa umeelekezwa kwa wanyama wa
Tanzania kwa sababu ya uhifadhi wa bioanuai, lakini hapa kwetu Tanzania
suala katika usimamizi wa wanyamapori limeendelea kuwa ni tatizo kubwa
hivyo kuendelea kudhoofisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa Kipindi cha miaka ya 1990 Wizara ya
Maliasili na Utalii Tanzania ilifanya tathmini ambayo ilihitimisha
kwamba,“Ni muhimu kwa uhifadhi wa wanyamapori hapo baadaye kwa hapa
Tanzania wananchi waishio pamoja na wanyamapori wapatiwe mafao ya moja
kwa moja yatokanayo na wanyama”.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na gharama hii na uwezo wake wa kiuchumi kwa
taifa na jumuia za vijijini zilizo jirani na maeneo ya hifadhi ya
wanyamapori, sekta ya wanyamapori haijaweza kuendelezwa kufikia uweza
wake kikamilifu kutokana na matatizo yafuatayo:
Kutokuwepo kwa Sera ya Wanyamapori iliyo wazi.
Kushindwa kwa uhifadhi wanyamapori na kushindana na namna nyingine za matumizi ya ardhi, hasa katika jamii za vijijini.
Kutokuwepo kwa mwamko juu ya uhifadhi wa wanyamapori miongoni mwa
wapangaji wa mipango na maafisa wenye mamlaka, na hivyo basi, suala la
ardhi na wanyamapori kupewa uzito mdogo sana wakati wa upangaji mipango.
Kuongezeka kwa ujangili kwa kasi kubwa na biashara isiyo halali
kunakosababishwa na udhaifu katika utekelezaji wa Sheria na Sera
zilizopo.
Mheshimiwa Spika, Katika mabadiliko yanayotokea ya kiikolojia, kiuchumi
na kijamii katika muktadha wa kitaifa na kimataifa,Kambi rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuimarisha sekta ya wanyamapori kwa
kuzingatia yafuatayo;
Kuweka sera madhubuti za uendeshaji wa shughuli za wanyamapori, na
kushiriki kikamilifu katika uendeshaji na usimamizi wa rasilimali za
wanyamapori nchini kote.
Kuweka na kuwezesha kuwepo kwa mazingira halali na ya kisheria
yatakayoziwezesha jamii za vijijini na sekta binafsi kushiriki katika
shughuli kwenye mapori ya akiba.
Kuweka utaratibu endelevu utakaosimamia na kuhakikisha kwamba
kunaendelea kuwepo maeneo yaliyohifadhiwa ambapo wanyamapori na maeneo
mengine ya asili yataendelea kuhifadhiwa.
Kupiga vita matumizi haramu ya wanyamapori.
Kuwawekea wafanyakazi wa idara ya wanyamapori kanuni za maadili ya kazi zao.
Kuanzisha mfumo wa utunzaji wa habari zinazohusu wanyamapori.
3.9 UWINDAJI, UFISADI NA UKIUKWAJI WA SHERIA ZA MATUMIZI YA ARDHI
Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema kwenye hotuba ya Ardhi leo tunarudia
tena kuwa, Kwa muda mrefu sasa Ardhi ya Tanzania imegeuzwa shamba la
bibi na kikundi cha mafisadi! Kambi ya upinzani imeshuhudia mkataba
ulioingiwa baina ya kampuni za Uranium resourses PLC , Western
Metals Limited na Game frontiers of Tanzania Limited . Mkataba ambao
umetengenezwa na kampuni ya kitanzania ya REX ATTORNEYS. Na ulisainiwa
tarehe 23.3.2007.
Mheshimiwa Spika, Mkataba husika,ambao vipengele vyake vinaainisha
kwamba unatakiwa uwe wa SIRI unaihusu kampuni ya uwindaji, inayofahamika
kwa jina la Game frontiers of Tanzania Limited inayomilikiwa na Bwana
Mohsin M. Abdallah na ndugu Nargis M. Abdallah . Kampuni hii ya
uwindaji, imeingia mkataba na kampuni mbili za kigeni, za kufanya
utafiti wa uchimbaji wa madini ya Uranium katika kijiji cha Mbarang’andu
kwa malipo yafuatayo:-
Malipo ya $ 6,000,000/- za kimarekani, ambazo zitalipwa kwa awamu mbili
ya malipo ya $3,000,000. Malipo ya kwanza yatafanyika pale uzalishaji
wa urani takapoanza.
Malipo ya $ 250,000/- baada ya kampuni za madini kukamilisha utafiti wa
madini ya urani na kupata kibali cha uchimbaji wa madini.
Malipo ya $ 55,000 kila mwaka kama fidia ya kushindwa kufanya biashara
na usumbufu unaotokana na shughuli za machimbo kwenye kitalu! Malipo
hayo yatafanyika kila tarehe 31 Machi.
Malipo ya $ 10,000 kwa vijiji vitakavyoathiriwa na utafiti huo wa
urani. Malipo ambayo yametokana na makubaliano baina ya kampuni ya
uwindani na kampuni za madini!
Mheshimiwa spika,Nimepitia sheria za uhifadhi wa wanyamapori, The
wildlife Conservation Act, 1974 (Sheria ya zamani) na Sheria mpya The
wildlife Concervation Act, Act no 5 of 2009. Sheria hizi zinamruhusi mtu
aliyekuwa na leseni ya uwindaji, kuwinda wanyama tu! Tena wale
alioruhusiwa katika leseni ya uwindaji!
Mheshimiwa spika, Halikadhalika, Sheria ya ardhi, ya Mwaka 1999, Sheria
namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya ardhi ya vijiji, sheria namba 5 ya
mwaka 1999 inatamka bayana kwamba ardhi inajumuisha vitu vyote vilivyo
juu ya ardhi na chini ya ardhi isipokuwa madini au mafuta, Na kwa mujibu
wa sheria za Tanzania linapokuja suala la madini, umiliki unatoka kwa
mtu binafsi na kurudi serikalini! Na ni Serikali kupitia wizara ya
Nishati na Madini ndio pekee yenye mamlaka ya kutoa leseni ya kutafuta
madini kwa kampuni za madini!
Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge
lako tukufu uhalali wa mkataba kati ya Game Frontiers na Uranium
Resourses PLC na Western Metals! Ni sheria ipi inayoipa kampuni ya
uwindaji haki ya kualika kampuni ya nje kwenye eneo ambalo haina umiliki
kufanya utafiti na hatimaye kuchimba madini hatari kama urani? Nini
mustakabali wa watanzania wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka mbunga
hiyo ambao wanaishi maisha yao ya kila siku pasipo kujua kama kuna
utafiti wa madini hatari ya urani unaoendeshwa kwa siri kubwa? Ni
serikali ya aina gani, yenye uwakilishi mpaka ngazi ya kitongoji na
usalama wa taifa mpaka ngazi za chini kabisa za utawala inashindwa
kuyaona haya?
Kambi ya Upinzani, Tunasisitiza kuwa, kwa kuwa Kampuni hii ya Game
Frontiers Tanzania Limited imevunja sheria za nchi na ni kinyume na
leseni waliyopewa ya kuendesha shughuli za uwindaji ni wakati sasa wa
waziri wa Maliasili na Utalii atangaze kuifutia leseni ya uwindaji leo
na sio kesho ili iwe fundisho kwa wengine .
4.0 TAARIFA ZA WATUMISHI WA SERIKALI KUHUSIKA NA UJANGILI.
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo taarifa za baadhi ya watumishi wa serikali
kuhusika katika matukio ya ujangili katika hifadhi za taifa na taarifa
za uchunguzi kuzifikia mamlaka za serikali pasipo kuzifanyia kazi huku
watumishi hawa ambao ni askari polisi wakitumia magari ya Serikali na
magari yao binafsi kusindikiza misafara iliyobeba mizigo ya nyara za
Serikali. Kambi rasmi ya Upinzani inahoji ukimya wa Serikali pale
uchunguzi unapothibitisha ushiriki wa baadhi ya watumishi katika
ujangili ambapo pamoja na wahusika kufahamika kwa majina bado kumekuwa
na udhaifu na ulegelege katika kuwachukulia hatua za kinidhamu na
kisheria.
Mheshimiwa Spika, Taarifa kuhusu kupewa dhamana kwenye mahakama ya
Serengeti - Mugumu kwa mtuhumiwa aitwaye Bryson Baloshigwa Naftali,
mkaazi wa kijiji cha Busunzu, wilaya ya Kibondo, mkoa wa Kigoma ambaye
anathibitika kuwa ni kiongozi mkuu wa mtandao wa ufadhili wa uwindaji
faru na biashara haramu ya meno ya tembo katika maeneo ya hifadhi za
Serengeti,Katavi, Tarangire, Ziwa Manyara, Hifadhi ya Ngorongoro pamoja
na Mapori ya Akiba kama Ugalla, Rungwe, Moyowosi, Maswa. Kambi rasmi ya
Upinzani ina taarifa na ushahidi kuwa nyara zinazopatikana huzisafirisha
nje ya nchi kwenda Burundi, Uganda na kwingineko ambapo mtuhumiwa
amejitengenezea mtandao mkubwa ulioenea hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Mtuhumiwa huyo alikamatwa tarehe 11.06.2012 kwa kesi
namba MUG/IR/1330/2012 akiwa kwenye kituo cha Polisi cha Kibondo, baada
ya kufikishwa Mugumu,alilegezewa masharti ambapo mtuhumiwa huyo pamoja
na mwenzake Kama Yohana Tika (mpigaji Tembo maarufu mkoani Kigoma na
muwakilishi mkuu wa Bryson katika ujangili) walifunguliwa kesi tofauti
na tuhuma zao ambayo ni kuazimisha silaha, kesi ambayo ina urahisi wa
kupata dhamana,na wengine kufunguliwa kesi ya ujambazi kutumia silaha
“armed robbery”, kwa baadhi ya washirika wake wasio na ushawishi wa
fedha.
Mheshimiwa Spika,Kambi rasmi ya Upinzani inasikitishwa na utendaji wa
mamlaka za serikali na serikali yenyewe,pamoja na kuwepo kwa taarifa
hizi Serikali imeendelea kuwaacha huru watuhumiwa hawa bila kuchukua
hatua madhubuti na kuendelea na kuzimaliza maliasili za nchi hii.
Mheshimiwa Spika ulegevu huu wa Serikali ukiambatana na mazingira ya
rushwa ulithibitika mnamo tarehe 09.07.2012 mtuhumiwa Bryson
alipochukuliwa rumande, kwa kibali maalum “removal order” na kufikishwa
Mahakamani kisha kupata dhamana, na inasemekana kuwa alitakiwa
kurudishwa Kigoma kwa gharama za Serikali kama alivyoletwa hapo Mugumu
kwa escort ya Polisi. Kwa kawaida mtuhumiwa huyo alipaswa kufikishwa
mahakamani tarehe 15/7/2012 kwa kesi yake kutajwa kwa mara nyingine
kufuatia taratibu za kimahakama.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani, inaitaka Serikali kutoa majibu kama
watuhumiwa na ujangili wanafikishwa na kuondolewa pasipo kufuata
taratibu za kisheria na kuwaachia huru,na huu ndio uthibitisho kwa
watanzania jinsi tulivyo na Serikali iliyojaa rushwa na yenye kufumbia
macho vitendo vikubwa vya rushwa hivyo watanzania kupoteza matumaini na
kukosa imani na vyombo vyao vya dola hasa Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, vilevile kumekuwepo kwa taarifa za majangili wa
utafutaji masoko wa nyara za Serikali, wasambazaji wa silaha za
kivita,wafadhili wa ujangili wenye wawakilishi wao na kufanya kazi ya
kusambaza sumu ya kuulia wanyama,bunduki na risasi. Kambi rasmi ya
Upinzani inahoji pamoja na taarifa hizi kuwepo upande wa serikali kwa
majina na aina ya silaha zinazomilikiwa na watuhumiwa hawa na
kutozifanyia kazi,serikali itoe majibu ni mkakati gani uliopo kama sio
Serikali inahusika katika ujangili huu?
Mheshimiwa Spika, usalama wa tembo uko hatarini kutokana na serikali
kutochukua hatua dhidi ya ujangili wa tembo pamoja na taarifa za
ujangili huo kuwepo serikalini na viongozi wa CCM kushiriki katika
ujangili na kulindwa, mfano Mzee Lazaro ambaye ni Mwenyekiti wa CCM
Wilaya ya Karatu, Yeye anamiliki silaha aina ya Rifle .375 akiwa ni
mshirika wa mtandao wa ujangili kwa kuwepo vielelezo kuwa anashirikiana
na BRYSON BALOSHINGWA ambaye Serikali imeendelea kumlinda. Kambi rasmi
ya Upinzani inataka Serikali kwa kupitia Waziri husika kuwaeleza
watanzania je ni sera ya Serikali ya CCM katika kufumbia macho masuala
yanayotishia ustawi wa taifa kwa kuwalinda majangili wakiwemo viongozi
wa CCM kama ambavyo tumetaja hapo juu ? Kwani pamoja na Serikali ya CCM
kuwa na taarifa hizi bado imeendelea kuonyesha udhaifu wake katika
kuchukua hatua za kisheria.
4.1 Utambuzi wa Majangili
Mheshimiwa Spika, pamoja na Bunge kukaa hapa na kupitisha bajeti za
kuwezesha utendaji katika idara na Serikali, pamoja na idara kutimiza
majukumu yake ya kuhakiki upatikanaji wa majangili ili wachukuliwe hatua
bado zoezi hilo limeshindwa kufanyiwa kazi na Serikali. Hii ni dhahiri
kwa Serikali ya CCM kuhusika na ubadhilifu wa maliasili za nchi hii na
kuwahadaa wananchi kuwaletea maisha bora huku wakijinufaisha wenyewe na
viongozi wake wa CCM hususani Mzee Lazaro ambaye ni Mwenyekiti wa CCM
Karatu amabaye ametajwa katika orodha ya majangili wa tembo.
Mheshimiwa Spika ,Kambi rasmi ya upinzani inatoa rai kwa serikali
kuruhusu TAKUKURU kuchunguza mazingira haya ya rushwa ikizingatiwa
mgawanyo usio sawa Duniani umeonekana kuleta historia ya kuvuruga amani
katika baadhi ya nchi,hivyo kufumbia macho vitendo hivi vitahatarisha
amani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, katika moja ya ahadi na utekelezaji wake Serikali
iliahidi kuimarisha vituo vya doria katika eneo la KIA Nangurukuru na
West Kilimanjaro. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kusimamia
utekelezaji wa sheria za utumishi wa umma na kuwezesha wafanyakazi
kuheshimu mali za umma kwa kuzingatia wafanyakazi wa umma ndio hutumia
fursa ya utumishi wao kuweza kuhujumu maliasili za nchi.
Mheshimiwa Spika,kukua kwa mtandao wa ujangili ulioenea karibu nchi
nzima na kushamiri kwa usafirishaji wa nyara na silaha haswa za kivita
na risasi za moto kupitia njia za maeneo ya Biharamulo,Kibondo,Kasulu,
Kahama,na Urambo,Geita na Mpanda. Hii haihatarishi tuu usalama wa
wanyama pia amani katika nchi kufuatia umiliki huu kuwa haramu.Kambi
rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa tamko juu ya hatua
itakazochukua kukomesha ujangili kwa kutumia taarifa zilizopo ili iwe
fundisho kwa wengine na kuiweka nchi katika mazingira yaliyo salama.
5.0 USALAMA WA FARU
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa na ulinzi wa wanyamapori katika
hifadhi, mwenendo wake unaendelea kutoleta matumaini kwa baadhi ya
wanyama kuendelea kutoweka kwa kasi. Idadi ya faru waliokuwapo kwenye
hifadhi miaka ya 1969 iliyokadiriwa kuwa kati ya 150 hadi 250 ilipungua
hadi kufikia faru 20 miaka ya 1980. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa
TANAPA, Allan Kijazi, anasema, faru wa mwisho kuonekana katika hifadhi
hiyo eneo la Pangalo ilikuwa ni mwaka 1985, huku faru wengine wote
wakiteketezwa kwa kuuawa na majangili, ambapo idadi ya sasa ni 19
ikijumuishwa na watatu walioongezwa kutoka Uingereza na kufika Tanzania
Juni 17, 2012.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inasikitishwa na kauli ya
Waziri Kagasheki alipokua akipokea Faru watatu kutoka Uingereza katika
uwanja wa KIA kwamba majangili wanao mtandao mkubwa, wanazo pesa
nyingi,swali ni je, hivi Serikali haina uwezo kifedha na kimtandao
kuhakikisha inapambana na majangili hao ambao licha ya kuwa na mtandao
mkubwa na uwezo kifedha pia wanazo silaha nzito za kivita?
Mheshimiwa Spika, Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia kiongozi wa
uingereza wakati huo Winston Churchill,aliwahi kusema “In every age
there comes a time when a leader must come forward to meet the need of
the hour, therefore ,there is no potential leader who does not have an
opportunity to make a positive difference in the
society.Tragically,there times when a leader does not rise to the hour.
Katika tafsiri isiyo rasmi;
“Katika kila dahari hufika wakati anajitokeza kiongozi mwenye uwezo wa
kuitikia mahitaji ya wakati huo. Hivyo kila kiongozi mwenye uwezo anayo
fursa ya kuleta mabadiliko katika jamii. Kwa bahati mbaya kuna wakati
amabapo kiongozi anashindwa kuitikia mahitaji ya wakati”.
Mheshimiwa Spika, inauma, inakera, inasikitisha na inaudhi kuona uongozi
wa serikali ya CCM umeshindwa kuitikia hitaji la wakati huu ambalo ni
kuwalinda wanyama wetu kwa gharama yoyote.Kambi rasmi ya Upinzani
inachelea kuamini nguvu za majangili kuizidi Serikali,kama si Serikali
kushirikiana na majangili,hivyo kuitaka Serikali kupitia shirika la
hifahi za taifa TANAPA kuhakikisha usalama wa wanyamapori kwani ni
wakati mwafaka kwa serikali kuamka na kuweka mipango madhubuti
inayotekelezeka ya kuhakikisha ulinzi unaimarishwa dhidi ya faru na
wanyama wengine wakiwamo tembo kwa kuishirikisha jamii inayoishi
kuzunguka hifadhi zetu.
Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo Serikalini za ufuatiliaji wa tukio la
kuuwawa kwa faru wawili (jike na mtoto) katika hifadhi ya Serengeti na
taarifa hizi kuifikia menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa tarehe
17/5/2012. Uchunguzi ulibaini makundi maalumu mawili; Kundi la kwanza
linahusisha wafanyabiashara, baadhi ya watumishi wa idara mbali mbali za
Serikali kama vile Polisi, na Idara ya Wanyamapori (Game Reserves na
Game scouts – watumishi wa Halmashauri) wanaoishi katika baadhi ya
Wilaya hizo. Kundi la pili ni la Majangili/majambazi ambao hupatiwa
silaha (bunduki), risasi na uwezeshwaji kifedha toka kwenye kundi la
kwanza na baada ya kufanikisha, mazao yatokanayo na ujangili na
ujambazi, huyauza au kugawana na wawezeshaji wao.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inahoji pamoja na Serikali kuwa na
taarifa hizi ni hatua zipi zilizochukuliwa kwa usalama wa hifadhi za
taifa? Pia kuitaka Serikali kuheshimu rasilimali za nchi hii na
kuwatendea haki watanzania kwa kuhakiki katika Serikali kulinda
rasilimali kwa manufaa ya watanzania.
6.0 SITISHO LA USAFIRISHAJI WANYAMA NJE YA NCHI.
Mheshimiwa Spika, katika zoezi la kusitisha usafirishaji wa wanyama nje
ya nchi Serikali iliendelea kufanya maamuzi yasio na tija kwa uchumi wa
kitanzania kufuatia zoezi hilo kuhusisha biashara ya ndege wa aina zote
na wale waharibifu kama kunguru, Ngedere, Tumbili na Reptilia, maamuzi
haya yamepelekea kupoteza mapato ya serikali ambayo kwa mwaka 2008/2010
Serikali ilikusanya shilingi 408,724,551.00 hadi biashara inafungwa kwa
kipindi cha mwaka 2011 Agosti 18, Serikali ilikua imekusanya shilingi
154,083,480.00.
Mheshimiwa Spika, haya ni maamuzi mabovu kwa Serikali yasiyozingatia
athari katika uchumi wa nchi huku Serikali ikiendelea kutumia pesa
nyingi kuteketeza wadudu waharibifu ambao wangeweza kutupatia mapato
pamoja na kukuza ajira.Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inathubutu kusema
utamaduni huu unazidi kukomaa na kuota mizizi kutokana na maamuzi ya
kukurupuka yaliyofanywa na Serikali ya CCM. Hivyo, Kambi rasmi ya
Upinzani, tunaitaka Serikali kurejea upya maazimio hayo na kuruhusu
wadudu waharibifu waendelee kuuzwa nje badala ya kuteketezwa.
Mheshimiwa Spika, zoezi la kudhibiti kunguru weusi katika maeneo ya
Kibaha,Morogoro na jiji la Dar Es Salaam kwa kutumia sumu aina ya DRC
1339 pamoja na mitego limeonekana kushindwa kwa kiasi kikubwa
ikizingatiwa wingi wa kunguru hawa kuendelea kuwepo,Kambi ya Upinzani
inaitaka serikali kulitafutia ufumbuzi makini kwa wakati kuondoa kero
hii kwa kuruhusu wauzwe nje na wauzaji wasizuiliwe kuwakamata na
kuwauza.
7.0 SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI.
Mheshimiwa Spika, Wakati Mhe.Waziri anazindua bodi ya ushauri ya Wizara
ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Jijini Dar Es Salaam alithibitisha
kuwa Tanzania inafilisiwa na viongozi wetu, kwa maana kuwa kuna
ubadhirifu mkubwa wa mapato yanayotokana na maliasili zetu. Alisema
nanukuu.... “jamani idara ya wanyamapori ina fedha nyingi, lakini
zinaliwa na watu kwa maslahi binafsi na kama fedha hizo zingekuwa
zinapelekwa serikalini kama inavyotakiwa, nchi hii kwa sasa ingefika
mbali, mimi naogopa hata kutaja kiasi cha fedha hapa hadharani” .
Mheshimiwa Spika, Kwa nukuu hiyo toka kwa Waziri Mwenye dhamana, ni
dhahiri kuwa sekta hii inauwezo mkubwa sana wa kuchangia kiasi kikubwa
katika pato la Taifa na kiasi kingine kuachwa ili sekta iweze
kujiendesha na kutengeneza mazingira ya kuwavutia wawekezaji wengi
zaidi. Kambi rasmi ya Upinzani inataka kujua je ni mkakati gani ambao
Waziri ameuandaa wa kubana mianya ya upotevu wa mapato uliokuwa
unaendelea katika sekta hiyo? Na ni hatua gani za kisheria zimechukuliwa
kwa watu wote waliohusika na ubadhirifu wa mapato kama ambavyo Waziri
alibaini?
Mheshimiwa Spika,Ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za
serikali iliainisha upotevu wa pesa kwa kiwango cha shilingi 874,853,564
kutokana na kufanyika kwa maamuzi ya upendeleo kwa kutoa kiwango cha
chini cha mrahaba kwa mauzo ya misitu.Hii ni uthibitisho wa kutosha wa
kutoendelea kwa sekta ya misitu ikizingatiwa wenye mamlaka katika
usimamizi wa rasilimali misitu wameshindwa kuzingatia maadili ya
utumishi na sheria na kujilimbikizia mali kwa kupindisha taratibu za
kiutendaji.
Mheshimiwa Spika,Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuchukua
hatua thabiti za kuzuia upotevu huu kwa kuzingatia kuwa rasilimali za
taifa hili zinapaswa kunufaisha watanzania wote na sio kikundi cha watu
wachache ambao wamepewa dhamana ya kusimamia rasilimali hizo kwa niaba
yetu sote.
Mheshimiwa Spika, ahadi ya Serikali katika mwaka 2011/2012 ilitangaza
kuendelea kupitia na kuboresha Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu pamoja
na Programu za Misitu na Nyuki ili ziendane na wakati pamoja na kufanya
tafsiri ya Kanuni za Misitu na Nyuki kutoka lugha ya Kiingereza kwenda
Kiswahili na kusambaza nakala 4,500 kwa wadau mbalimbali. Kambi rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuliambia Bunge hili mchakato huo umefikia
wapi ? Na je wadau wameshirikishwa kwa kiasi gani mpaka sasa?
Mheshimiwa Spika, Serikali ilizungumzia swala la kuongeza wingi na
ubora wa mazao ya nyuki, ila utekelezaji wake hauoneshi dhamira ya
Serikali katika kuongeza wingi na ubora wa mazao yatokanayo na nyuki kwa
kutowekea mkazo katika uendelezaji wa shughuli za ufugaji nyuki kwa
vitendo, na hasa katika kuongeza uhamasishaji kwa jamii kushiriki katika
masuala ya misitu na ufugaji nyuki kwa kutoa elimu ya utunzaji na
matumizi bora ya rasilimali za misitu na nyuki kwa kufanya huduma za
ugani na kusambaza majarida na vipeperushi.
Kambi ya upinzani , inaitaka serikali kuacha kutoa matamko kila siku na badala yake sasa wafanye kwa vitendo.
7.1 WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU (TFS)
Mheshimiwa Spika, kutokana na matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi
kuendelea kushika kasi na kwa kuzingatia tatizo hilo kuendana na uvunaji
wa misitu kwa kasi, hivyo wakala wa huduma za misitu pamoja na ahadi ya
kuandaa mipango ya usimamizi wa hekta milioni 1.36 za misitu ya hifadhi
ya uzalishaji (Misitu ya Asili na Mashamba 16 ya miti ya kupanda)
kufuatana na mipango kazi ilivyopitishwa,Kambi rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kueleza mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa na kutoa
mwongozo wa jinsi itakavyokabiliana na tatizo la uvunaji wa misitu
unaoendelea kwa kasi.
Mheshimiwa Spika, moja ya matatizo katika usimamizi wa misitu ya hifadhi
Tanzania ni pamoja na kutokua na mipaka iliyohakikiwa na kuainishwa
rasmi,pia kutokuwepo kwa wasimamizi wa hifadhi hizo za misitu,Kambi
rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa majibu ya utekelezaji kwa
kurejea ahadi yake hapa bungeni kupitia waziri husika juu ya kuhakiki
mipaka, kuchora ramani na kutayarisha mipango ya usimamizi na
kuhakikisha hifadhi zitakazohakikiwa zinapangiwa mameneja ili kuimarisha
usimamizi.
7.2 MFUKO WA MISITU TANZANIA
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa ahadi ya Serikali Katika Mpango kazi wa
mwaka 2011/2012, Mfuko wa Misitu Tanzania ulitenga takribani Shilingi
500,000,000.00 kuwezesha jamii kuanzisha na kuendesha miradi midogo ya
jamii ambayo ni rafiki wa mazingira pamoja na uanzishaji wa vitalu vya
miti na upandaji miti katika mashamba ya vikundi na watu binafsi. Kambi
rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa maelezo ya kuthibitisha jamii
ngazi ya vijiji zinanufaika na miradi hii ikizingatiwa mfumo uliotumika
katika utoaji wa fedha zilizotengwa haukumlenga mwananchi wa chini na
kuwanufaisha wachache katika asasi za kiraia hivyo kutofikia lengo la
Serikali.
8.0 MIPAKA YA HIFADHI
Mheshimiwa Spika, moja ya vipaumbele katika ilani ya CCM ni kuwezesha
jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kunufaika na rasilimali za
wanyamapori na misitu. Aidha,hali ilivyo kwa jamii inayozunguka hifadhi
ni tofauti na ilivyoazimiwa katika mipango ya mgawanyo wa rasiliamali
hizo na kuendelea kuwaneemesha wachache huku wananchi wakiendelea kuwa
maskini,mfano utanuzi wa mbuga ya Mpanga, wilayani Njombe kwa kuwatoa
wananchi wa vijiji vilivyo karibu katika maeneo bila kulipwa fidia ya
mashamba yao na maeneo yaliyokua malisho ya mifugo yao ni dhahiri
uwekezaji huo hauna manufaa kwa wananchi wanaozunguka hifadhi na
uendelea kuongeza lindi la umasikini uliokithiri
Mheshimiwa Spika,kumbukumbu za bunge zinaonesha kuwepo kwa tatizo katika
meneo mengi juu ya kero za maeneo yenye hifadhi na mapori tengefu
,Mbunge wa Njombe magharibi mwaka 2009 februari alipokua akichangai
bajeti ya Wizara alisema “Hoja yangu hapa ni juu ya uhai wa Wanyama na
Uhai wa Wananchi, wanaoishi katika maeneo husika, kwenye jimbo langu
katika Kata ya Luduga, Wilaya Njombe na pia Kata ya Wangama, Wilaya
Njombe, wananchi wangu wanaishi kwa wasiwasi na mateso makubwa, juu ya
kuongeza mipaka ya hifadhi ya Kipengere Mpanga Game Reserves. Mipaka ya
zamani haina matatizo. Naomba kauli ya Serikali juu ya tatizo hili; ni
lini ufumbuzi wa kudumu utafanyika?”.
Mheshimiwa Spika,majibu ya Serikali yalikua hivi , “Napenda kusema
kwamba pori la akiba la Mpanga Kipengere, limeanzishwa kisheria kwa
tangazo la Serikali la namba 483 la mwaka 2002 wakati zoezi la kuweka
mipaka lilithibitika kwamba kuna baadhi ya vijiji vimo ndani ya hifadhi.
Ili kutatua tatizo hilo Serikali itashirikiana na wadau kupitia upya
mipaka hiyo ili kuhakikisha kuwa maeneo ya vijiji husika yanakuwa nje ya
pori husika” .
Mheshimiwa Spika, pamoja Serikali kutozingatia ahadi yake na
kutozingatia sheria ya Ardhi ya vijiji Na.5 ya 1999, na kutothamini
umuhimu wa wananchi wake katika kutumia ardhi,Serikali imeruhusu TANAPA
kuongeza mipaka ya mbuga ya mpanga pasipo kuzingatia sheria ya
ubadilishaji wa matumizi ya ardhi kwa kubadili mipaka ya maeneo ya
vijiji mfano kijiji cha Imalilo chenye usajili NA:350,Kata ya Wangama
wilayani Njombe kuwa mbuga ya Mpanga pasipo kufuata taratibu ikiwa ni
pamoja na kuwashirikisha wananchi katika mkutano mkuu wa kijiji na
kuendelea kuwanyanyasa wananchi wa maeneo hayo pamoja na kutoza faini ya
shilling laki tatu pindi waingizapo mifugo katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuzingatia
sheria katika kubadili matumizi ya ardhi kwa kuzingatia manufaa ya umma
kama sheria inavyoelekeza na sio kuendelea na utamaduni wake wa sasa wa
kuwanyanyasa na kuwadhulumu wananchi ardhi yao na kuwaacha bila kujua la
kufanya.
9.0 SEKTA NDOGO YA UTALII
Mheshimiwa Spika,Kambi rasmi ya Upinzani ilitoa maelezo kwa Serikali
katika kipindi cha bunge cha mwaka 2011/2012 kuhusu ya Wakala wa
Usafirishaji Watalii, kifungu cha 58 kifungu kidogo cha (1) na (2), cha
Sheria ya Utalii ya mwaka 2007, kwa ujumla wake vinaelekeza kwamba
shughuli za uwakala wa kusafirisha watalii na kuongoza watalii mlimani
zifanywe na Watanzania tu, Pia, kifungu cha 3 cha Sheria ya TANAPA ya
mwaka 2003, kinaielekeza TANAPA kushughulika tu na Wakala wa Utalii
aliyeandikishwa na mwenye leseni (za TALA) na ambaye ni mwanachama wa
chama kinachoshughulika na masuala ya utalii.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kwa
kuzingatia maslahi ya mtanzania katika shughuli za utalii kutoa maelezo
ya utekelezaji wa sheria hii na usimamizi wake.Aidha hali ilivyo
inaonyesha kampuni nyingi za kigeni zinafunguliwa hapa nchini kwa mbinu
ya ubia kati ya wageni na watanzania wakati wenye kampuni hizo wanakuwa
ni wageni, na hivyo wageni wanapata mwanya wa kufanya biashara ya utalii
mlimani na faida kubwa inabaki nje badala ya kubaki kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza bunge ni
hatua gani Serikali imechukua kuhakikisha Sheria ya Utalii ya mwaka
2007 inasimamiwa kwa manufaa ya Watanzania, ikiwa kampuni za wageni
zilizokuwa zikifanya uwakala wa safari za mlimani bado zinaendelea
kufanya kazi hiyo, licha ya sheria kutaka ifanywe na watanzania pekee?
Na je, Serikali imechukua hatua gani dhidi ya kampuni za kigeni
zinazoendelea kutumia mbinu ya kuingia ubia watanzania katika kufanya
biashara ya utalii ya kupeleka watalii mlimani, ikiwa faida kubwa
iliyopaswa kuwa ya watanzania inaendelea kwenda nje na kunufaisha
kampuni hizo.
Mheshimiwa Spika ,Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye vivutio vingi vya
watalii duniani, ikiwa ni pamoja na hifadhi za wanyama, mlima
Kilimanjaro, fukwe za bahari na kadhalika. Vivutio hivi vina mchango
mkubwa katika ukuaji wa sekta ya utalii na uchumi wa taifa kwa ujumla
lakini havijatangazwa kwa kiasi inavyostahili hivyo kuchangia katika
uingiziaji mdogo na usioridhisha wa pato la utalii ukilinganisha na nchi
jirani .
Mheshimiwa Spika, Sekta ya utalii Tanzania inategemea zaidi wageni
kutoka nje ya nchi kitu ambacho kinaifanya sekta kuwa hatarishi kwa
mabadiliko yanayotokea duniani,ikizingatiwa kuwa kushuka katika
uchangiaji wa pato la taifa pale utokeapo msukosuko wa uchumi duniani
pamoja na jitihada hafifu za Serikali katika kuhamasisha utalii wa
ndani. Vilevile Sekta ya utalii pia inakabiliwa na vikwazo mbalimbali
vikiwemo upungufu wa ujuzi katika nyanja za ufundi, uongozi na
ujasiriamali wa ndani katika sekta ya utalii wa kisasa, miundombinu duni
na huduma duni za kusaidia watalii (afya, fedha, bima, teknolojia ya
mawasiliano na kadhalika).
Mheshimiwa Spika , Kambi rasmi ya Upinzani inaona ni dhahiri vikwazo
hivi vimeifanya Tanzania kushindwa kutumia kikamilifu fursa zilizopo
katika sekta ya utalii, ambazo zingechangia kwa kiasi kikubwa katika
kukuza Pato la Taifa, hivyo Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kutengeneza mazingira yatakayo ruhusu utalii usio tegemezi hivyo ili
kukuza utalii asilia,utalii tamaduni, utalii michezo na utalii
makongamano/mikutano.
Mheshimiwa Spika, vilevile kikwazo kingine kikubwa katika utalii ni
idadi ndogo ya hoteli isiyoweza kukidhi mahitaji ya wageni, mpaka sasa
Tanzania tuna hoteli na camping sites 167 tu. Kiasi hiki ni kidogo sana
ukilinganisha na idadi ya watalii wanaojaribu kufanya booking ya kuja
kutaIii Tanzania wanaambiwa nafasi zimejaa, na hii inawafanya baadhi ya
wenye hoteli kujipangia bei wanavyotaka na kuufanya utalii Tanzania
uonekane ni gharama. Aidha kumekuwepo na malalamiko pamoja na tuhuma
kuhusu baadhi ya watalii wa ndani hasa wenye ngozi nyeusi kutopewa
huduma za malazi na chakula na kuwepo kwa utoaji kipaumbele kwa
watanzania wenye asili nyeupe, hizi ni shutuma nzito za ubaguzi wa rangi
ambapo Serikali inatakiwa kutoa majibu ya kina kuhususiana na shutuma
hizi.
Kambi rasmi ya Upinzani inapenda kuishauri Serikali kutoa nafasi na
vipaumbele kwa makampuni ya ndani yenye uwezo wa kuendesha sekta ya
utalii kwa ufanisi na weledi. Kwa mfano katika mkoa wa Iringa kuna
makampuni ambayo yameonyesha nia ya kuwekeza katika biashara za malazi
na kukuza utalii kama MR Hotel, Tananka LtD, Hilltop Hotel, Kalenga
Hotel, Embakassy Hotel, Mfugale (muekezaji anayejenga hoteli ya nyota
tano), na familia ya Hanspop ambayo inajenga hoteli na shughuli za
uwindaji pamoja na makampuni mengine mengi ambayo yamekuwa yakifanya
biashara hii toka awali. Hii ni mifano ya watanzania ambao wameonesha
nia na dhamira ya kukuza utalii hasa hasa ukizingatiwa kuwa utalii wa
nyanda za juu kusini, hususani hifadhi ya taifa ya Ruaha inahitaji
kutangazwa na kuliongezea taifa letu mapato.
10.0 BODI YA UTALII TANZANIA (TTB)
Mheshimiwa Spika, mambo ya msingi ambayo bodi ya utalii inahitaji
kuyafanya ni pamoja na kuhakiki uendelezaji wa sekta ya utalii nchini.
Hali ilivyo sasa sekta ya utalii imeendelea kukua zaidi katika mikoa ya
kaskazini mwa nchi.Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kupitia wizara ya
maliasili na utalii kuandaa mpango yakinifu wa kuweza kutekeleza
uendelezaji wa utalii kwa kuutangaza katika mikoa ya kusini na mashariki
pamoja na maeneo ya pwani. Pia tunaishauri Serikali kupitia bodi hii
kuendeleza mpango mkakati wa uhifadhi katika kupunguza msongamano wa
kitalii kwenye korido ya mikoa ya kaskazini pekee na kuvutia utalii
katika mikoa mingine yenye vivutio tosha.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi iliyo kwenye viwango vya chini katika
uendelezaji wa utalii wa ndani. Aidha, pamoja na kuwepo kwa program
mbalimbali za kuhamasisha utalii wa ndani lakini bado elimu hii
haijafanikiwa kuwafikia watanzania wengi kutembelea vivutio mbalimbali
nchini na kukuza utalii wa ndani. Kambi rasmi ya Upinzani bungeni
inaitaka bodi ya utalii kushirikiana na wadau wa utalii kuendeleza elimu
ya uhamasishaji utalii wa ndani ili kuweza kubadili mitazamo ya
watanzania na kuwawezesha katika kubadilika, kuthamini na kutumia bidhaa
za utalii asilia.
11.0 MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO.
11.1 Manunuzi ya Huduma Bila Mkataba Halali
Mheshimiwa Spika,Tatizo la kutokuwepo kwa mikataba halali kati ya
Taasisi za Umma na watoa huduma na wauzaji bidhaa limeendelea kuwa
kikwazo katika utekelezaji wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka
2004,Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ambapo Mamlaka ilifanya
biashara na wamiliki wa hoteli za kitalii na watoa huduma mbalimbali
bila ya mkataba,Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kusimamia
sheria ili kuepuka mazingira kama haya yaliyo na harufu za rushwa.
Mheshimiwa Spika,katika taarifa ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu
za serikali ilibainisha kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro
ilifanya malipo kabla ya kupokea mali (advance payment) ya kiasi cha
Shilingi milioni 643.76 kwa Toyota Tanzania Ltd mwezi Aprili, 2008 kwa
ajili ya ununuzi wa magari,Katika kiasi kilichotolewa magari yenye
thamani ya Shilingi milioni 471.3 yaliletwa mnamo tarehe 15 Agosti 2008
na mengine yenye thamani ya Shilingi milioni 137.9 tarehe tarehe 30 Juni
2010,Hivyo kiasi cha shilingi milioni 34.4 kati ya fedha zilizolipwa
kwenye fedha za awali hazijarejeshwa kwenye mamlaka takribani miaka
mitano sasa.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
hesabu za Serikali inaainisha kuwa hakuna makubaliano juu ya jinsi fedha
zitakavyorejeshwa,Huu ni uvunjifu wa sheria za usimamizi wa fedha za
umma ambapo imeelezwa wazi kwamba fedha zisilipwe kwa wauzaji wa bidhaa
au huduma kabla ya kupokea mali na kama makubaliano ya mkataba
yanaruhusu basi ni muhimu zirejeshwe ndani ya kipindi cha miezi 12.
Mheshimiwa Spika, Kama muuzaji au mtoa hudhuma atashindwa kutimiza
wajibu wake, kinyume cha hapo adhabu kali inapaswa kutolewa. Kambi rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa majibu ya jinsi inavyoshughulikia
suala hili mpaka sasa na imechukua hatua gani.
11.2 Bodi za Wakurugenzi wa NCAA Kuingilia Kazi za Menejimenti.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani ilihoji katika hotuba yake ya
mwaka 2011/2012, pia taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za
serikali amethibitisha wajumbe wa bodi ya mamlaka ya hifadhi ya
ngorongoro wakijihusisha katika utendaji wa kazi za menejimenti. Kitendo
hiki ni kasoro kubwa na inapunguza uhuru wa menejimenti kutoka kwa bodi
na inaleta migongano ya kimaslahi kati ya pande hizi mbili taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali ilithibitisha namna
ambavyo bodi ya wakurugenzi ilivyojihusisha mara kadhaa katika maonyesho
ya kimataifa ya utalii katika kipindi kati ya Julai, 2010 na Juni,
2011.
Mheshimiwa Spika, Hali hii ni kinyume na utawala bora na waraka wa Ikulu
No. SHC/B.40/6/21 wa tarehe 28/03/1994 aya ya 3 na 5. Utaratibu huu
huathiri kazi za bodi za usimamizi kwa kuwa zitakuwa zimegawanyika
kimtazamo na kimaslahi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Kambi rasmi ya Upinzani kuishauri serikali
na kuhakikisha tume ya kuchunguza bodi ya Ngorongoro ikiwemu mwenyekiti
wa bodi ambaye ni makamu mwenyekiti wa CCM taifa Mh Pius Msekwa, sasa ni
zaidi ya siku mia tatu sitini na tano na robo yani mwaka, tume hiyo
imeshindwa kuleta ripoti ya uchunguzi ili ifanyiwe kazi,na bado serikali
imeendelea kujiita serikali sikivu.
Mhjeshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaamini itakapotokea
kutotekelezwa majukumu ya kiutendaji yaliyotolewa kwa wajumbe wa bodi,
Wajumbe wa Bodi hawatakuwa na nguvu ya kufuatilia na kudai maelezo juu
ya kushindwa kufikiwa kwa malengo hayo, na hivyo bodi itabaki kufanya
maamuzi yanayolinda maslahi yao katika utendaji wa mamlaka husika na huu
sio utawala bora.
11.3 Kukosekana kwa Miongozo ya Utendaji wa Bodi ya mamlaka ya Ngorongoro.
Mheshimiwa Spika,Miongozo ya utendaji wa bodi (charter) ni maandiko
yanayowaelekeza wajumbe wa bodi kwenye Shirika na mwelekeo wake na
ambayo inafanya kazi kama mwongozo wa kiutendaji wa bodi kwa kutoa
taarifa juu ya muundo wa bodi na utendaji ikiainisha kazi na majukumu ya
wajumbe wa bodi. Pia, inajumuisha miongoni mwa mambo mengine kanuni za
maadili ikiwemo sera ya migongano ya kimaslahi, sera ya uhudhuriaji wa
vikao vya bodi, mwongozo wa kutathmini kazi za bodi, miongozo ya
kutathmini utendaji wa mkurugenzi mkuu, historia za wajumbe wa bodi,
kalenda ya bodi na mpango kazi wake,
Mheshimiwa Spika,Kambi rasmi ya Upinzani inaamini ukosefu wa mwongozo
huu yaweza kueleweka kuwa bodi husika haina mwelekeo katika kuendeleza
malengo ya mamlaka hivyo kujali maslahi binafsi kama ilivyothibitishwa
katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali ya
mwaka 2010/2011. Taarifa hiyo imebaini mamlaka ya hifadhi ya
Ngorongoro(NCAA) haikuandaa mwongozo wa bodi (Board Charter) na hivyo
kujiweka katika mashaka ya kukosa mwongozo wa utendaji kazi.
12.0 Hitimisho.
Mheshimiwa Spika, nimalizie hotuba yangu kwa maneno ya baba wa taifa
Mwl.Nyerere aliyoyasema 1962 kuwa “Watu walio hatari sana ni wale ambao
wanafikiri kuwa wa najua Kila kitu, wala hawana haja ya kujifunza zaidi.
Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia Mendeleo. Sababu moja iliyotuzuia sisi
waafrika kuendelea ni majbu rahisi kwa matatizo makubwa. Shamba letu
Kama halikutoa mavuno ya kutosha, jibu lilikuwa wazi: au limelogwa au ni
amri ya Mungu. Watoto wetu walipokuwa wagonjwa Damian, jibu lilikuwa
rahisi: au wamerogwa au ni amri ya Mungu. Nyumba ilipopigwa radi
ikaanguka, jibu lilikuwa rahisi uchawi au amri ya Mungu”.
Mheshimiwa Spika, Majibu ya namna hii huzuia binadamu kupata sababu za
kweli za matatizo yao, yanazuia akili kutafuta njia za kweli na za
uhakika za kuyaondoa matatizo hayo.
Siku hizi, tumeanza kutumia Majibu
mengine ya rahisi, mambo yakienda mrama, badala ya kutumia akili zetu na
kutafuta sababu za kweli, tunawalaumu wazungu,au wahindi,au ukoloni,au
ukoloni mpya au vibaraka n.k. Lakini yafaa akili ifikie jibu hilo baada
ya uchunguzi wa kweli, sio uvivu wa kutumia akili. Uvivu wa kutumia
akili unaweza kutufanya tutumie dawa kuondoa matatizo ambayo si dawa
hata kidogo. Nikienda kwa daktari anitibu maradhi yangu, natazamia kuwa
kazi yake ya kwanza ni kujua hasa sio kwa kubahatisha naumwa nini, kazi
yake ya pili ni kujua sababu ya ugonjwa wangu. Daktari asipoujua ugonjwa
wangu na sababu zake huwezi kujua dawa yake. Akinipa dawa nikapona
atakuwa kaniponya kwa Bahati tu, kwa desturi daktari wa namna hiyo
haweza kumponya mgonjwa, na udaktari wake ni wa hatari sana.
Mheshimiwa Spika, Kadhalika chama ambacho nia yake ni kuwa daktari wa
matatizo ya jumuiya hakinabudi kiwe na tabia ya kujua matatizo yenyewe,
sababu ya matatizo hayo na dawa yake.
Ni wakati muafaka kwa serikali
kuhakikisha inatambua matatizo yaliyopo katika wizara hii na kutafuta
tiba vinginevyo serikali kuwa wazi mbele ya watanzania kuwa imeshindwa
na kukiuka kile alichokiamini baba wa taifa kwa serikali, ni vema
Waziri awe wazi kama ameshindwa kutatua matatizo haya ndani ya Wizara
aseme ili aweze kupatiwa dawa stahiki .
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya kambi ya upinzani naomba kuwasilisha.
.............................
Mchungaji Peter Msigwa
Mbunge wa Iringa Mjini
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani
Wizara ya maliasili na Utalii
|
No comments:
Post a Comment