UTANGULIZI
Julai 13, 2012 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliwasilisha Maoni yake
kuhusu Mpango na Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa
mwaka wa fedha 2012/2013. Pamoja na mambo mengine, Maoni ya Kambi
yalihusu utaratibu wa uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Tanzania.
Maoni ya Kambi yalizua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge huku
wachangiaji wengi wakimtuhumu Msemaji wa Kambi kwa “kuidhalilisha”
Mahakama na/au “kuwadhalilisha majaji” (Gosbert Blandes-Karagwe CCM);
“kuwavunjia heshima majaji” (Naibu Spika Job Ndugai); kuwatukana na
kuwadhalilisha majaji (Murtaza Mangungu-Kilwa Kaskazini); “kuwa-offend,
kuwadhalilisha na kuwanyanyasa majaji” (Assumpter Mshama-Nkenge CCM);
“kufedhehesha Mahakama na majaji” (Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Frederick Werema).
Aidha, Msemaji wa Kambi alishambuliwa kwa kudaiwa kuwa mfitini na asiye
na akili timamu (Muhammad Chomboh- Magomeni CCM)); na “kujiamini kwamba
yeye anajua zaidi kuliko watu wengine wote” (Mangungu). Kwa upande wake,
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alilihakikishia Bunge
kwamba “... haijatokea hata siku moja katika nchi hii Rais akamteua Jaji
wa Mahakama Kuu bila kuzingatia mapendekezo yaliyopelekwa kwake na hii
Tume ya Uajiri wa Mahakama.” Zaidi ya hayo, “... labda Mheshimiwa Lissu
anamjua Jaji angalau mmoja na anaweza akamtaja aseme Jaji huyu ametolewa
tu mitaani na Mheshimiwa Rais, yupi hakuna… hawa majaji wote
walioteuliwa wamepitia mchakato huu wa kikao kizito sana cha watu ambao
ndiyo wenye sheria ya nchi hii.”
Baadaye Msemaji wa Kambi alitakiwa kufuta kauli yake kuhusu uteuzi wa
majaji usiofuata utaratibu uliowekwa na Katiba. Msemaji wa Kambi
alikataa kufuta kauli hiyo ambako Mwenyekiti wa Kikao alielekeza Msemaji
wa Kambi apelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
kwa hatua zaidi. Alichukua uamuzi huo ili masuala hayo yapatiwe
ufafanuzi ili wananchi wapate picha kamili na ya kweli kuhusu jambo hili
muhimu. Maelezo haya yana lengo la kutoa ufafanuzi huo.
Katika maelezo yake kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya BUnge,
Lissu alisema, “Nitajitahidi kwa kadri inavyowezekana kutoa ushahidi
unaothibitisha kwamba siyo tu kwamba utaratibu wa kikatiba katika uteuzi
wa majaji umekiukwa mara nyingi, bali pia majaji wengi walioteuliwa kwa
utaratibu wa nje ya Katiba wamekuwa hawana ‘uwezo, ujuzi na kwa kila
hali hawakufaa kukabidhiwa Madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu.” TATIZO LA MUDA MREFU
Kuna ushahidi mkubwa kuthibitisha kwamba kuna watu wameteuliwa kuwa
Majaji wa Mahakama Kuu “... wakiwa wamekaribia muda wao wa kustaafu
kwingineko katika utumishi wa umma (na) wanapewa ‘zawadi’ ya ujaji ili
kuwawezesha kupata mafao ya majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana
katika miaka ya karibuni.” Ni muhimu kuweka wazi hapa kwamba utamaduni
huu haukuanza baada ya Rais Jakaya Kikwete kuchaguliwa kuwa Rais, bali
ni tatizo la muda mrefu. Kwa mfano, marehemu Jaji Kulwa Masaba na Jaji
Madina Muro na majaji Stephen Ihema, Juxton Mlay, Augustine Shayo na
Vincent Lyimo waliteuliwa majaji wa Mahakama Kuu baada ya utumishi wa
muda mrefu kwingineko katika utumishi wa umma.
Majaji Masaba na Muro waliteuliwa huku wakiwa wagonjwa mahututi na – kwa
kadri ninavyofahamu - hawakuwahi kuandika hukumu hata moja kabla ya
mauti kuwafika! Jaji Lyimo aliteuliwa Machi 28, 2007 mwaka mmoja kabla
ya muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, ilipofika
Oktoba 26, 2007 Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo Phillemon Luhanjo
alimtaarifu Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete “... ameamua kusogeza mbele
muda wa kustaafu wa Mheshimiwa Jaji Vincent Kitubio Damian Lyimo kwa
miaka mitatu kuanzia Machi 28, 2008 siku ambayo angestaafu kwa lazima”!
Kwa upande wao, Majaji Ihema, Mlay na Shayo walijizolea umaarufu kwa
kuwa majaji wasioandika hukumu na hivyo kuwa wacheleweshaji wakubwa wa
kesi katika Mahakama Kuu. Jaji Ihema alitia fora kwenye jambo hili kiasi
kwamba Juni 16, 2003 Mwenyekiti wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mkoa wa Singida, Mzee Joram Allute, alilazimika kumwandikia Rais
Benjamin Mkapa maombi ya kumwondoa Jaji Ihema kama Jaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania “kwa uzembe na kukosa maadili.”
Mzee Allute alikuwa na kesi kwa Jaji Ihema ambapo Jaji huyo ‘alikalia’
uamuzi kwa zaidi ya miaka minne hadi aliponyang’anywa faili la kesi hiyo
na kukabidhiwa Jaji mwingine aliyeandika uamuzi ndani ya wiki tatu!
Mwezi mmoja kabla ya barua ya Mzee Allute kwa Rais Mkapa, mawakili wake
walikuwa wamemwandikia Jaji Mkuu Barnabas Samatta kulalamikia
ucheleweshaji wa uamuzi wa kesi hiyo. Mawakili hao walidai: “Hadhi na
heshima ya Mahakama inaporomoka vibaya kama inachukua zaidi ya miaka
mitatu kwa Jaji kutafakari na kutoa uamuzi kwa jambo jepesi kama maombi
ya pingamizi.” Licha ya malalamiko haya dhidi yake, Jaji Ihema alipatiwa
mkataba wa ajira wa miaka miwili mara baada ya kustaafu mwaka 2005. MAJAJI WA MIKATABA
Agosti 2, 2005 Jaji Kiongozi Hamisi Msumi alitoa taarifa kwa majaji wote
wa Mahakama Kuu kwamba Jaji Ihema alikuwa amepewa mkataba mpya baada ya
kustaafu kama Jaji wa Mahakama Kuu. Taarifa hiyo ilimfanya Jaji Bernard
Luanda, wakati huo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba,
kuhoji ‘Uhalali Kikatiba kwa Majaji Kufanya Kazi kwa Mkataba Baada ya
Kustaafu.’ Katika taarifa yake kwa Jaji Kiongozi Msumi, Jaji Luanda
alisema kwamba “... suala la majaji kupewa mikataba ... linaenda kinyume
na Katiba.” Jaji Luanda alifafanua: “Kwa kuwa Jaji amestaafu, basi
kiapo chake nacho kimeondoka. Kwa bahati mbaya hawaapishwi ili washike
kazi hizo za ujaji.... Ni hoja yangu kwamba Majaji waliostaafu na kupewa
mikataba si Majaji kwa mujibu wa Katiba.”
Msimamo wa Jaji Luanda uliungwa mkono mwaka mmoja baadaye na Jaji wa
Rufaa, Augustino Ramadhani wakati huo akiwa Kaimu Jaji Mkuu. Katika
‘Mawazo Kuhusu Vifungu Vinavyohusu Mahakama na Majaji’ aliyomwandikia
Jaji Mkuu Samatta na kunakiliwa kwa Majaji wa Rufaa wote, Jaji Ramadhani
alisema kwamba “... sio sahihi kwa Jaji Mkuu kustaafu na kupewa mkataba
wa kuendelea na wadhifa huo kupindukia umri wa miaka 65 (ambao ndio
umri wa kustaafu kwa lazima kwa Jaji wa Rufaa na Jaji Mkuu).” Baadaye
Jaji Luanda aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wakati Jaji Ramadhani alikuja
kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Kauli ya Kambi kwamba kuna ukiukaji mkubwa wa Katiba kuhusiana na uteuzi
wa majaji inaungwa mkono na nyaraka za ndani ya Serikali na hasa Ofisi
ya Rais, Ikulu yenyewe. Desemba 6, 2007, mkutano kuhusu ajira ya majaji
waliostaafu ulifanyika Ikulu, Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Katibu
Mkuu Kiongozi Luhanjo. Wajumbe wengine walikuwa pamoja na Mwanasheria
Mkuu Johnson Mwanyika na Naibu wake Sazi Salula, Katibu Mkuu Utumishi
George Yambesi, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Sophia Wambura na Susan
Mlawi wa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri.
Kwa mujibu wa Kumbukumbu za Mkutano huo, “kwa utaratibu unaotumika sasa,
baadhi ya Majaji wanaofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa Ibara ya
110(1) kwa Majaji wa Mahakama Kuu na Ibara ya 120(1) ya Katiba
wanaongezewa muda wa kuendelea na utumishi wao kwa mkataba baada ya wao
kuwasilisha maombi rasmi.” Baada ya mjadala juu ya jambo hili, wajumbe
wa mkutano walikubaliana kwamba “utaratibu wa kuongeza muda kwa njia ya
mkataba unakiuka masharti ya Katiba na kuleta mkanganyiko kama Majaji
hao wanastahili kulipwa mshahara au pensheni au vyote kwa pamoja.”
Matokeo ya mkutano wa Ikulu ilikuwa ni kuundwa kwa ‘Kikundi Kazi kwa
Ajili ya Kuchambua na Kushauri Kuhusu Ajira ya Majaji Baada ya Kustaafu’
chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kikundi Kazi
kiliwasilisha Taarifa yake Machi 7, 2008. Katika Taarifa yake Kikundi
Kazi kinakubaliana na msimamo wa kikatiba kwamba “kwa kuzingatia Ibara
za 110 na 120 za Katiba inaonekana wazi kuwa suala la ajira za mikataba
kwa Majaji ambao wamekuwa wakifanya kazi za Jaji baada ya kufikia umri
wa kustaafu ni kinyume cha Katiba.” Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, hadi
mwezi Machi 2008, “... walikuwepo Majaji wawili ... wa Mahakama ya
Rufani na Majaji tisa ... wa Mahakama Kuu, ambao wapo katika ajira za
mkataba, na Jaji mmoja ... wa Mahakama Kuu aliyeongezewa muda wa ajira
kwa mujibu wa masharti ya Katiba....”
Hii ina maana kwamba, kulikuwa na Majaji kumi na moja ambao walikuwa
wanafanya kazi kinyume cha Katiba na – kwa maneno ya Jaji wa Rufaa
Luanda – hawakuwa Majaji kwa mujibu wa Katiba! Aidha, kwa mujibu wa
ushahidi wa nyaraka hizi, kulikuwa na Jaji mmoja tu ambaye alikuwa
ameongezewa muda wa ajira ya ujaji kwa mujibu wa Katiba. Katika
mapendekezo yake, Kikundi Kazi hakikumung’unya maneno:
“Mikataba iliyopo hivi sasa iko kinyume cha Katiba.... Hii ina maana
kwamba Majaji hao wanafanya kazi ya Jaji kinyume cha Katiba, hivyo kazi
zote ambazo wamezifanya na wanaendelea kuzifanya wakiwa chini ya ajira
mpya za mikataba hazina uhalali wowote kisheria. Kazi hizo ni sawa kama
vile zimefanywa na mtumishi mwingine yeyote asiye na madaraka ya Jaji.
Hivyo basi, Rais ashauriwe kuifuta mikataba hiyo mara moja kwa vile ina
madhara makubwa kwa jamii na katika uteuzi wa Majaji wapya kuchukua
nafasi zao. Majaji waliofutiwa mikataba waendelee na pensheni zao kama
kawaida.”
Miaka minne imepita tangu Kikundi Kazi kiwasilishe mapendekezo yake
Ikulu lakini hakuna hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo hayo.
Aidha, licha ya msimamo wa majaji Luanda na Ramadhani kuwa na umri wa
takriban miaka saba, utaratibu wa uteuzi wa majaji wastaafu haujaachwa
na mamlaka husika ya uteuzi. Ajira ya sasa ya Jaji Kiongozi Fakih Jundu
iko katika kundi hili la watu wasiokuwa Majaji kwa mujibu wa Katiba. JAJI KIONGOZI FAKIH JUNDU
Jaji Kiongozi Fakih Jundu aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Rais
Mkapa mwaka 2003. Julai 29, 2009, Jaji Jundu wakati huo akiwa Jaji
Mfawidhi wa Kanda ya Iringa, alitoa taarifa ya kustaafu kwa mujibu wa
sheria. Hata hivyo, mara baada ya kutoa taarifa hiyo, Jaji Jundu siyo tu
alipewa mkataba wa ujaji kwa miaka mitatu, bali pia alipandishwa cheo
na kufanywa Jaji Kiongozi.
Kama hiyo haitoshi, inasemekana sasa kwamba Jaji Kiongozi Jundu
ameongezewa mkataba mwingine tena wa miaka miwili kuendelea kuwa Jaji
Kiongozi kuanzia Julai 29, 2012! Huu ni ukiukaji wa Katiba. Kwanza, kwa
mujibu wa Taarifa ya Kikundi Kazi, “... umri wa kustaafu wa Jaji
Kiongozi ni miaka sitini.... Hivyo, iwapo Rais atamuongezea Jaji
Kiongozi muda wa kufanya kazi, hatamuongezea kama Jaji Kiongozi.”
Kwa maana nyingine, kama ilikuwa makosa kikatiba kumpa Jaji Jundu
mkataba wa ajira kama Jaji wa kawaida, ilikuwa makosa makubwa zaidi
kikatiba kumpandisha cheo na kumfanya Jaji Kiongozi wakati
alikwishafikisha umri wa kustaafu wa Jaji Kiongozi! Pili, kwa utamaduni
uliozoeleka Tanzania, majaji wamekuwa wanaongezewa kipindi kimoja cha
miaka miwili ili wamalizie kesi walizokuwa nazo hadi muda wao wa
kustaafu unawadia. Kwa msimamo wa kikatiba ulioelezwa na Jaji wa Rufaa
Luanda, Jaji Mkuu Ramadhani na Kikundi Kazi, siyo sahihi kwa Jaji
Kiongozi Jundu kustaafu na kupewa mkataba wa kuendelea na wadhifa huo
kupindukia muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa Katiba!
Nyongeza hii ya pili ya mkataba wa Jaji Kiongozi Jundu imewafanya watu
wanaojiita ‘Watumishi wa Mhimili wa Mahakama’ kumwandikia Msajili wa
Mahakama ya Rufani ya Tanzania kulalamikia jambo hilo. Kwa mujibu wa
barua yao, ambayo pia ilinakiliwa kwa Mwanasheria Mkuu na Jaji Mkuu,
watu hao wamesema yafuatayo kuhusu Jaji Kiongozi Jundu: “Sisi watumishi
wa Mahakama tunafahamu udhaifu mkubwa kiutendaji alionao Jaji Kiongozi
wetu wa sasa. Kimsingi hamudu madaraka haya. Ipo mifano mingi ya udhaifu
wa Jaji Jundu. Mfano alimhamisha hakimu kutoka kituo chake cha kazi
kama adhabu kwa vile hakimu huyo alitoa maamuzi ambayo yeye
hakuyafurahiya kwenye ile kesi maarufu ya kibaragashia. Ni busara za
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, ndizo zilizomsaidia hakimu huyo.” JAJI THOMAS MIHAYO
Thomas Bashite Mihayo aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Oktoba
8, 2003. Januari 16, 2006 Jaji Mihayo alitoa notisi ya kustaafu kwa
mujibu wa Katiba kuanzia Juni 8, 2006 atakapokuwa ametimiza umri wa
miaka sitini. Hata hivyo, Machi 8 ya mwaka huo, Jaji Mihayo alitaarifiwa
na Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete alikuwa amempa “... mkataba wa miaka
miwili kuanzia Juni 9, 2006.” Mkataba huo ulifikia mwisho wake Juni 8,
2008. Hata hivyo, Jaji Mihayo alipatiwa mkataba mwingine tena wa mwaka
mmoja ulioanzia Juni 9, 2008 hadi Juni 8, 2009 na baada ya hapo
hakupatiwa mkataba mwingine.
Inaelekea Jaji Mkuu Ramadhani alisahau msimamo wake wa awali kuhusu
ajira za mikataba kwani ndiye aliyependekeza Jaji Mihayo “... apewe
mkataba mwingine wa mwaka mmoja...” Na wala si Jaji Mihayo pekee
aliyepatiwa au kuongozewa mkataba katika mazingira tatanishi kama haya.
Kwa mujibu wa nyaraka za Idara Kuu ya Utumishi, Jaji Donasian Mwita
alipatiwa mkataba wa ujaji Juni 28, 2004. Mkataba huo wa miaka miwili
ulianza kutumika Julai 1, 2004. Vile vile, Jaji Joseph Masanche alisaini
mkataba wa aina hiyo hiyo na Idara Kuu ya Utumishi ulioanza kutumika
kuanzia Machi 7, 2006. MAADILI YENYE SHAKA
Msemaji wa Kambi hakuzungumzia masuala yanayohusu maadili ya majaji.
Hata hivyo, kutokana na mjadala uliojitokeza ndani na nje ya Bunge
kutokana na hotuba yake, ushahidi umepatikana unaoonyesha kwamba baadhi
ya majaji wameteuliwa bila ya kwanza kuwafanyia uchunguzi juu ya maadili
yao. MAJAJI KASSIM NYANGARIKA NA ZAINAB G. MURUKE
Kassim Nyangarika alikuwa wakili wa kujitegemea na wakili mwenza wa Jaji
Kiongozi Jundu kabla ya uteuzi wake kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka
2003. Kama wakili, Bwana Nyangarika aliwahi kumwakilisha mlalamikaji
katika kesi ya Peter Muti dhidi ya CIELMAC Ltd., Kesi ya Madai Na. 314
ya 2003 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni. Katika
kesi hiyo mteja wa wakili Nyangarika alishinda.
Hata hivyo, kufuatia rufaa dhidi ya uamuzi huo, Mahakama Kuu ilifutilia
mbali mwenendo wa kesi hiyo baada ya kugundua kwamba Wakili Nyangarika
alikuwa amefanya vitendo vyenye kuashiria uvunjifu mkubwa wa maadili.
Kwa mfano, Mahakama Kuu iligundua kuwa Wakili Nyangarika alimwelekeza
hakimu – kwa kutumia ‘kipande cha karatasi cha rafu na kilichoandikwa
kirafiki’ - namna ya kuendesha kesi hiyo. Mahakama Kuu iligundua makosa
makubwa zaidi ya hilo. Kwa mujibu wa Jaji Kalegeya, “... kulikuwa na
mawasiliano yasiyokuwa rasmi kati ya Mahakama na Wakili.” Jaji Kalegeya
alikuta ushahidi wa uwezekano mkubwa kwamba Wakili Nyangarika ndiye
aliyeandaa uamuzi wa Mahakama katika kesi hiyo. Aidha, Mahakama Kuu
iligundua kwamba Wakili Nyangarika “... aliielekeza Mahakama kutokutoa
uamuzi kwa tarehe iliyopangwa badala yake aliielekeza itoe uamuzi huo
tarehe nyingine.”
Kwa mujibu wa Jaji Kalegeya, kama kilichoonyeshwa katika mawasiliano ya
Wakili Nyangarika na Mahakama ya Wilaya kilikuwa cha kweli basi “...
utoaji haki katika Mahakama hiyo uko katika hatari kubwa kama sio jina
la Mahakama yote, kitu kinachohitaji marekebisho ya haraka.” Kwa sababu
hiyo, Jaji Kalegeya alielekeza kwamba “mamlaka husika zichukue hatua za
kufichua ukweli kuhusu barua ya Wakili Nyangarika ya tarehe 18/03/2004.”
Hukumu na maelekezo ya Jaji Kalegeya yalitolewa tarehe 22 Julai, 2005.
Miezi saba baadaye, Wakili Nyangarika aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania!
Wakili mwingine mwenye maadili ya mashaka yanayofanana na ya Jaji
Nyangarika ambaye pia ameteuliwa Jaji Mahakama Kuu ni Zainab Muruke.
Kama wakili, Zainab Muruke alimwakilisha Stephen Hill Forwood ambaye
alikuwa amepatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka
miwili bila faini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu. Baadaye
kampuni ya mawakili ya Z.G. Muruke & Co. Advocates iliwasilisha Hati
ya Mapitio (Memorandum of Review) katika Mahakama hiyo hiyo ikiomba
Bwana Forwood abadilishiwe hukumu.
Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Kabuta na tarehe 26
Julai, 2004, Bwana Forwood akabadilishiwa adhabu kuwa faini ya shilingi
20,000 au kifungo cha miaka miwili. Jambo hili liliripotiwa kwa Jaji
Kiongozi ambaye aliamuru uchunguzi ufanywe uliopelekea kushushwa cheo
cha Hakimu Mkazi Kabuta. Jaji Kiongozi pia aliamuru Wakili Muruke atoe
maelekezo ya ushiriki wake katika sakata hilo. Hiyo ilikuwa tarehe 14
Desemba, 2004. Mwaka mmoja na miezi miwili baadaye, Zainab Muruke
aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. MAJAJI PELAGIA B. KHADAY NA PATRICIA FIKIRINI
Bi. Pelagia B. Khaday ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliyeteuliwa
mwaka 2009. Kabla ya uteuzi huo Bi. Khaday alikuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kabla ya hapo alikuwa Hakimu Mkazi
Mkuu na Msajili wa Wilaya, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha. Agosti 12,
2004, alipewa taarifa ya kusimamishwa kazi kama Msajili wa Wilaya na
kuhamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na ‘uzito wa
shutuma’ zilizotolewa dhidi yake kwa Jaji Mkuu.
Taarifa hiyo iliandikwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha
Edward Rutakangwa, kwa maelekezo ya Jaji Mkuu na ilieleza kwamba Bi.
Khaday alikuwa anatuhumiwa kwa “kuwashinikiza au kuwashawishi baadhi ya
mahakimu mkoani Arusha kushughulikia au kuamua kwa upendeleo mashauri
yaliyowahusu ... jamaa au rafiki zake”; na “kuwaandalia sababu za rufaa
baadhi ya washitakiwa waliotiwa hatiani na mahakama za mahakimu hapa
mkoani.”
Kabla ya kumsimamisha Bi. Khaday kazi, Jaji Mfawidhi Rutakangwa alikuwa
amemteua Mheshimiwa Jacob Somi, wakati huo akiwa Msajili wa Mahakama Kuu
Kitengo cha Ardhi, kuwa Afisa Uchunguzi (Enquiry Officer) ili
kuchunguza tuhuma dhidi ya Bi. Khaday. Taarifa ya Uchunguzi wa Awali ya
Afisa Uchunguzi Somi inasema kwamba Bi. Khaday alikuwa amelalamikiwa na
mahakimu kwa kuwashinikiza ili watoe maamuzi ya kesi zilizokuwa
zinawakabili jamaa au marafiki zake.
Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, Hakimu Mkazi Elvin Mugeta “alikiri
kuwa-approached na Bi. Khaday ili atoe hukumu ya upendeleo kwa mshtakiwa
Richard Bareto ambaye inasadikiwa kuwa ni jamaa wa rafiki yake wa
karibu.” Ijapokuwa Bi. Khaday alikanusha kufanya hivyo, Afisa wa
Uchunguzi Somi aliridhika kwamba “Bi. Khaday alikuwa amejiwekea
utaratibu, kama alivyodai mwenyewe, wa kuwasiliana na Mahakimu kwa lengo
la kuwafahamisha pamoja na mambo mengine malalamiko yaliyokuwa
yakimfikia dhidi yao ili kuwanusuru wasiharibikiwe.”
Hata hivyo, Afisa Uchunguzi Somi aliridhika kwamba “utaratibu huu
ulikuwa kero kwa mahakimu pale alipoutumia kwa kushinikizwa na jamaa
zake na/au rafiki zake kwa lengo la kupata maamuzi ya upendeleo. Kitendo
cha kumtoa mahakamani Hakimu kwa lengo la kutaka kujua hatima ya
mshtakiwa Bareto aliyekuwa asomewe hukumu siku hiyo, ni mfano wa
matumizi mabaya ya utaratibu huo.”
Afisa Uchunguzi Somi hakupata uthibitisho wa madai ya Bi. Khaday
kuwaandalia sababu za rufaa washtakiwa waliotiwa hatiani. Hata hivyo,
kwa mujibu wa Taarifa yake, “... sikuridhishwa na utaratibu wake wa
kupeleka nakala ya hukumu kwa Bi. Mushi na kumtaka aisome ili kuona kama
kuna uwezekano wa mshtakiwa Hussein Ramadhani Kitema kukata rufaa
Mahakama Kuu baada ya kufungwa jela na Bw. Mugeta.” Afisa Uchunguzi Somi
alipendekeza kwamba Bi. Khaday – “ambaye ni mtumishi wa Mahakama kwa
kipindi kisichopungua miaka 20...” - apewe nafasi ya kujirekebisha.
Baada ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi, Jaji Mfawidhi
Rutakangwa alimteua Mh. Samuel Karua, Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo
cha Kazi, kuwa Investigation Officer. Tarehe 23 Februari 2007,
Investigation Officer Karua aliwasilisha Taarifa ya Uchunguzi wake kwa
Jaji Mkuu. Taarifa ya Investigation Officer Karua ilimkosha Bi. Khaday
kwa tuhuma zote dhidi yake.
Hata hivyo, Taarifa ya Investigation Officer Karua ina maeneo mengi
yanayoleta mashaka. Kwanza, kama Investigation Officer Karua mwenyewe
alivyosema, shahidi muhimu katika uchunguzi wake alikuwa Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mushi. Vile vile, shahidi huyu alikuwa ‘star witness’ katika
uchunguzi wa awali mbele ya Afisa Uchunguzi Somi na ndiye aliyetoa
ushahidi wa yeye na mahakimu wengine kuingiliwa katika kazi zao na Bi.
Khaday.
Hata hivyo, mbele ya Investigation Officer Karua, shahidi huyu muhimu
alikana kila kitu alichokisema mbele ya Afisa Uchunguzi Somi. Kwa kiasi
kikubwa, Investigation Officer Karua aliitumia about turn hii kumkosha
Bi. Khaday dhidi ya tuhuma zote zilizokuwa zinamkabili. Cha kushangaza
ni kwamba Investigation Officer Karua hakujiuliza na hakumuuliza shahidi
huyu sababu za kukana ushahidi wote alioutoa mbele ya Afisa Uchunguzi
Somi.
Je, alirubuniwa au kutishwa ili amsaidie Hakimu na mtumishi mwenzake
katika Mahakama ya Tanzania asifukuzwe kazi? Kama sio hivyo, je, ni
sababu zipi zilizomfanya shahidi huyu muhimu kubadili ushahidi wake kwa
kiasi hicho? Je, ushahidi alioutoa shahidi huyu mbele ya Afisa Uchunguzi
Somi ulikuwa wa uongo? Na kama ulikuwa wa uongo, ushahidi wake wa pili
kwa Investigation Officer Karua ni wa kweli kiasi gani mpaka kumfanya
Investigation Officer Karua kutamka kuwa shahidi huyu ‘anaweza ... kuwa
anasema ukweli.’
Inaelekea Investigation Officer Karua, Hakimu Mkuu Mkazi mwenye uzoefu
wa miaka mingi katika Mahakama, alifanya kazi yake kwa mtazamo wa
kimahakama zaidi badala ya kutumia mtazamo wa kiupelelezi na/au
kiuchunguzi ambayo hasa ndiyo ilikuwa kazi yake katika uchunguzi wa
tuhuma dhidi ya Bi. Khaday. Kwa mtazamo wa kimahakama, ukweli kwamba
shahidi muhimu kama Hakimu Mkazi Mfawidhi Mushi alikana ushahidi wake wa
awali mbele ya Afisa Uchunguzi Somi ilikuwa inatosha kumfutia Bi.
Khaday hatia yote. Kwa mtazamo wa kiupelelezi/kiuchunguzi, about turn ya
shahidi huyu ingemfanya Investigation Officer Karua kuchunguza zaidi
sababu za kigeugeu hicho.
Pili, Investigation Officer Karua hakuipa uzito wa kutosha Taarifa ya
Afisa Uchunguzi Somi. Kwa mfano, Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi – yenye
kurasa 14 zilizochapwa - imeelezewa katika Taarifa ya Investigation
Officer Karua kwa aya moja tu! Kwa sababu hiyo, ni vigumu kukubaliana na
Investigation Officer Karua kwamba Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi
‘ilikuwa muhimu sana’ wakati umuhimu huo haujafafanuliwa wala kuelezewa
hata kidogo katika Taarifa yake.
Aidha, Investigation Officer Karua alitakiwa kueleza sababu za
kutofautiana na Afisa Uchunguzi Somi kwamba Bi. Khaday alikuwa anakera
mahakimu kwa kuwasiliana nao baada ya kushinikizwa na ndugu au rafiki
zake ili wapatiwe upendeleo katika kesi zilizokuwa zinawakabili.
Investigation Officer Karua hakufanya hivyo. Vile vile, Investigation
Officer Karua hakuona ajabu wala kujiuliza kama ilikuwa ni kitu cha
kawaida kwa Bi. Khaday kumleta Richard Bareto – mshtakiwa aliyehusishwa
na shinikizo la Bi. Khaday kwa Hakimu Mkazi Mugeta – kama shahidi wake
wa utetezi.
Tatu, Investigation Officer Karua hakutoa sababu za maana za kutochukua
ushahidi wa mahakimu wengine waliodaiwa kushinikizwa na Bi. Khaday.
Katika aya moja tu iliyowahusu mahakimu hao, Investigation Officer Karua
alisema kwamba siku ya kutoa ushahidi wao kwake, watu hao “...
walishikilia msimamo wa kauli walizotoa mbele ya Bwana Somi ... na baada
ya tafakuri ya muda ... mashahidi hawa waliachiwa.”
Mbele ya Afisa Uchunguzi Somi, mashahidi hawa wawili, Hakimu Mkazi Msumi
na Hakimu Mkuu wa Wilaya Mlay, walikuwa wamesema kwamba “... huko nyuma
(Bwana Msumi) aliwahi kuitwa na mlalamikiwa baada ya wadhamini
walioshindwa kukidhi masharti ya dhamana ... kumpelekea malalamiko ya
kukataliwa dhamana, maelezo ambayo hayakuwa na ukweli wowote.” Aidha,
kwa mujibu wa Afisa Uchunguzi Somi, “... katika hali isiyokuwa ya
kawaida Bw. Mlay, PDM hakuwa tayari kueleza kilichomsibu hadi kujiengua
katika usikilizaji wa kesi ambayo Bi. Mushi alidai ilikuwa inamkabili
rafiki yake wa karibu na Bi. Khaday.” Investigation Officer Karua
hakuona sababu yoyote ya kufuatilia ushahidi wa mahakimu hawa wawili!
Nne, Investigation Officer Karua anakubali kwamba hali ilikuwa tete
katika Kituo cha Arusha: “Inaelekea mtuhumiwa alikuwa na mahusiano
mabaya na baadhi ya mahakimu.” Kama hivyo ndivyo ilivyokuwa,
Investigation Officer Karua alikuwa na wajibu wa kuchunguza chanzo cha
mahusiano hayo mabaya, hasa kwa vile kulikuwa sio tu na tuhuma bali pia
ushahidi wa mahakimu husika kwamba Bi. Khaday alikuwa anawaingilia
mahakimu katika kazi zao. Hakufanya hivyo. Badala yake Taarifa ya
Investigation Officer Karua inaonekana kama jitihada za kumkosha Bi.
Khaday dhidi ya tuhuma nzito za ukosefu wa maadili ya kimahakama.
Jitihada hizi zilifanikiwa kwani miaka miwili baada ya Taarifa ya
Investigation Officer Karua, Bi. Khaday aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania.
Na wala siyo Bi. Khaday pekee aliyeneemeka na taarifa hiyo. Bi. Patricia
Fikirini, ambaye Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi inamwelezea kama mmoja
wa mahakimu waliosikiliza kesi ya mfanyabiashara maarufu wa Arusha,
Justin Nyari iliyokuwa chanzo cha tuhuma dhidi ya Bi. Khaday –
alihusishwa na tuhuma dhidi ya Bi. Khaday kwa maneno yafuatayo: “...
Kama mtawala ... (Bi. Khaday) ... alisema aliwahi, tena kwa nia njema,
kumweleza Bi. Fikirini ... kuhusu uvumi kwamba mume wake alikwenda
gerezani na kuchukua mamilioni ya fedha kwa Bw. Nyari na hivyo kumshauri
awe mwangalifu zaidi”! Katika uteuzi wa majaji uliofanywa na Rais
Kikwete mwezi Juni mwaka huu, Bi. Patricia Fikirini naye ameteuliwa kuwa
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wapo wanaoweza kusema kwamba Bi. Khaday hakupatikana na hatia yoyote na
kwa hiyo haikuwa makosa kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Aidha,
inaweza kudaiwa kwamba Bi. Fikirini hajawahi kutuhumiwa kwa kosa lolote
la maadili na kwamba ‘uvumi’ pekee hautoshi kumnyima mtu mwenye sifa
haki ya kuteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu. Kwa wenye hoja za aina hii jibu
langu ni kwamba kiwango cha ‘sifa maalum’ kinachotakiwa na Katiba kwa
mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ni mtu ambaye “... kwa kila hali
anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu....” Kiwango hiki
ni cha juu kiasi kwamba kutokuwa na hatia pekee haitoshi kumfanya
mhusika kuwa ‘kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa
Mahakama Kuu.’ Kwa maoni yangu, mtu aliyeundiwa uchunguzi wa kimaadili
au ambaye kuna uvumi unaomhusisha na rushwa ‘hafai kwa kila hali’
kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu. Majaji Khaday na Fikirini
wapo kwenye kundi hili. JAJI ALOYSIUS MUJULIZI
Jaji Aloysius Mujulizi alikuwa miongoni mwa watu ishirini walioteuliwa
Majaji wa Mahakama Kuu mwezi Februari, 2006. Kabla ya uteuzi wake, Jaji
Mujulizi alikuwa wakili wa kujitegemea katika kampuni ya mawakili ya
Ishengoma, Masha, Magai & Mujulizi Advocates (IMMMA) ya Dar es
Salaam. Kampuni hii ya mawakili ndiyo iliyoshiriki katika kuanzishwa kwa
kampuni iitwayo Deep Green Finance Co. Ltd. mnamo tarehe 18 Machi 2004.
IMMMA Advocates vile vile walikuwa mawakili wa Tangold Ltd.
Makampuni haya mawili yanatuhumiwa kutumika kupitishia mabilioni ya
fedha zilizoibiwa Benki Kuu ya Tanzania kati ya mwaka 2005 na 2006. Kwa
mfano, katika kipindi kifupi cha miezi minne kati ya Agosti 1 na Desemba
10, 2005 kampuni ya Deep Green Finance ilipokea jumla ya shilingi
10,484,005,815.39 kutoka akaunti ya kulipia madeni ya nje (EPA)
iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania. Katika kipindi hicho hicho, kampuni ya
Tangold Ltd. ililipwa dola za Marekani 13,736,628.73 kutoka kwenye
akaunti hiyo ya EPA. Nyaraka zilizowasilishwa BRELA na mawakili wa IMMMA
Advocates na kusainiwa na Gavana wa Benki Kuu wa wakati huo Daudi
Ballali tarehe 20 Mei 2005 zinaonyesha kwamba Tangold Limited ilikuwa
kampuni ya kigeni kutoka Jamhuri ya Mauritius. Haya yote yalitokea
wakati Jaji Mujulizi akiwa wakili mwenza wa IMMMA Advocates. ‘SIFA MAALUM’ ZENYE SHAKA JAJI WA RUFAA MBAROUK SALIM MBAROUK
Mbarouk Salim Mbarouk aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wa Mahakama ya
Rufani ya Tanzania mwaka 2008. Kabla ya uteuzi huo Jaji Mbarouk alikuwa
Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar. Sifa za mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa
Rufaa zimeainishwa katika ibara ya 118(3) ya Katiba: “Majaji ... wa
Rufani watateuliwa na Rais, kwa kushauriana na Jaji Mkuu, kutoka
miongoni mwa watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu
... zilizoainishwa katika Ibara ya 109 ya Katiba au kutoka miongoni mwa
watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa
mujibu wa sheria zinazotumika Zanzibar na wamekuwa na sifa hizo kwa muda
usiopungua miaka kumi na tano.”
Kwa mujibu wa Ibara ya 94(3) ya Katiba ya Zanzibar, 1984, “mtu hatoweza
kuteuliwa kuwa Jaji au Kaimu Jaji wa Mahkama Kuu mpaka awe na shahada ya
Sheria ya Chuo Kikuu kinachotambuliwa au Chuo cha aina hiyo; au awe au
amewahi kuwa Jaji wa Mahkama zilizofanana na hii kwa kesi zote za jinai
na madai katika Tanzania au sehemu yoyote ya Jumuiya ya Madola au
Mahkama ya Rufaa kutoka Mahkama hizo; au awe Mwanasheria wa Zanzibar au
Tanzania kwa kipindi kisichopungua miaka saba; au awe na uzoefu wa Jaji
au mwanasheria kwa pamoja usiopungua miaka saba.” Jaji Mbarouk
hajatimiza hata moja ya masharti hayo ya Katiba ya Zanzibar. Jaji huyu
hana shahada yoyote ya sheria inayotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya
Tanzania kama inavyotakiwa na Ibara ya 109(7) ya Katiba. Jaji huyu ana
stashahada ya juu ya sheria (Post Graduate Diploma in Law) ya Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha
nchini Uingereza.
Uteuzi wa Jaji Mbarouk kuwa Jaji wa Rufaa ulileta minong’ono mingi
katika taaluma ya sheria kiasi kwamba marehemu Wakili Leopold Kalunga
anasemekana kufungua shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania kutaka
uteuzi huo utenguliwe. Hata hivyo, Wakili Kalunga alifariki kabla ya
shauri lake kusikilizwa na kwa hiyo liliondolewa mahakamani. Aidha,
monong’ono hiyo ilimfanya Jaji wa Rufaa Mbarouk kujiunga na Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania ambako bado ni mwanafunzi hadi ninapoandika Addendum
hii. MAJAJI ‘WALIOTOLEWA MITAANI’
Katika Maoni ya Kambi tulidai kwamba “... sasa watu wanateuliwa kuwa
Majaji wa Mahakama Kuu ambao hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi
wa Mahakama na - kwa sababu hiyo - hawajafanyiwa vetting yoyote na
mamlaka hiyo ya kikatiba....” Ukiacha uteuzi wa Jaji wa Rufaa Mbarouk
ambao haubanwi na masharti ya Ibara ya 109(1) na 113(1)(a) ya Katiba,
majaji wengine waliotajwa kwenye Addendum hii hawakupendekezwa na Tume
ya Utumishi wa Mahakama. Majaji wengine ambao pia hawajawahi
kupendekezwa na Tume hiyo ni pamoja Fatuma Massengi, Mary Sumari, Imani
Mkwawa-Aboud na Sekela Mushi.
Last edited by palalisote; 18th August 2012 at 13:56.
(CHANZO : JAMII FORUMS)
|
No comments:
Post a Comment