FOLLOWERS

Friday, July 20, 2012

KEVINI YONDANI RUKSA KUKIPIGA YANGA

MLINZI WA KATIKATI WA YANGA KELVINI YONDANI ALIYESAJILIWA KUTOKA KWA WATANI WAO WA JADI SIMBA SC
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za wachezaji (ambayo katika uamuzi huu itarejewa kama ‘Kamati’) iliyokutana Julai 17 mwaka huu, baada ya kupitia mikataba na nyaraka zote zinazohusiana na mchezaji Kevin Yondani katika kujiridhisha juu ya hadhi yake ya usajili katika mashindano ya Kombe la Kagame kama zilivyowasilishwa mbele yake imefikia uamuzi ufuatao:-

1.   Kwa mujibu wa mapitio ya nyaraka zote zilizotajwa hapo juu na kufanyiwa upembuzi yakinifu, Kamati iliridhika pasi na shaka yoyote kuwa suala zima la mchezaji Kevin Yondani ni la kiutendaji, hivyo uamuzi wa Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na Klabu ya Simba kwa suala hilo la kiutendaji  kama Sekretarieti  ilivyofanya katika barua yake ya Julai 14 mwaka huu ulikuwa sahihi.

2.   Kamati ilibaini kuwa Mkataba wa mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba ulimalizika Mei 31 mwaka huu. Hivyo kwa taratibu za usajili mchezaji Kevin Yondani kuanzia Juni 1 mwaka huu alikuwa ni mchezaji huru.

3.   Aidha Kamati ilibaini kuwa Mkataba uliowasilishwa na Klabu ya Simba TFF ukiwa na maana ya kuongeza mkataba uliokuwepo TFF baina ya mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba uliwasilishwa TFF, Juni 7 mwaka huu ambapo ni kinyume cha utaratibu wa kuongeza mikataba ya wachezaji unaozitaka klabu kuwasilisha mikataba ya kuongeza muda wa mikataba ya wachezaji wao wakati mkataba halisi haujaisha muda wake. Hivyo mkataba huo kwa jicho la kisheria haupo.

4.   Hata kama kamati ingeuona mkataba huo katika jicho la sheria, bado mkataba huo una tatizo la kisheria hasa katika tarehe ambazo pande mbili husika ziliingia makubaliano hayo. 

Ukiuangalia mkataba huo unabainisha kuwa, wakati mchezaji Kevin Yondani aliingia makubaliano Desemba 23 mwaka jana, upande wa pili wa kimkataba ambao ni Klabu ya Simba inaonekana iliingia makubaliano hayo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Geofrey Nyange Kaburu, Desemba 23 mwaka huu. 

5.   Kisheria utata huu unaweza kuondolewa na pande husika tu kwa kurekebisha dosari hiyo kwa maridhiano kuweka saini katika mabadiliko hayo ili kuthibitisha mabadiliko hayo. 

Hivyo katika jicho la kisheria mkataba huo hauwezi kutumika kumzuia mchezaji huyo kwenda katika klabu anayoipenda wakati akiwa huru.

Kutokana na maelezo yote hapo juu, Kamati imeridhia hatua iliyochukuliwa na Sekretarieti ya TFF ya kumruhusu mchezaji Kevin Yondani kuichezea timu ya Yanga katika mashindano ya Kombe la Kagame 2012.



No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...