Waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, mheshimiwa Mizengo Peter Pinda |
WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda ameunda Kamati Maalum ya mawaziri sita kusaidia
mchakato wa marekebisho ya Bajeti ya Serikali ambayo mjadala wake
utahitimishwa kesho.Kuundwa kwa kamati hiyo kunazifanya kamati
zinazoifanyia kazi Bajeti ya 2012/2013 kufikia tatu.
Ijumaa iliyopita wabunge wa CCM waliunda kamati ndogo kwa ajili ya
kusaidi pamoja na mambo mengine kuangalia vyanzo vingine vya mapato na
kuona iwapo bajeti ya maendeleo inaweza kuongezwa, kukidhi kiu ya
wabunge.
Kamati nyingine ni ile ya Fedha na Uchumi ya Bunge ambayo tayari imetoa
maoni yake bungeni kuhusu Bajeti, lakini ikabainisha kuwapo kwa kasoro
kadhaa ambazo zinapaswa kurekebishwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi alikiri kuundwa kwa kamati hiyo, lakini akakataa kutoa taarifa
za kina kuhusu suala hilo kwa maelezo kwamba huo ni utendaji wa kawaida
wa shughuli za Serikali.
“Sidhani kama hiyo ni habari kubwa ya kwenda kwenye public (kwa umma).
Kwanza siyo kamati ya mawaziri, haiwezi kuwa hivyo, na huo ni utendaji
wa kawaida wa ndani ya Serikali maana sisi tuna mambo mengi
tunafanya,”alisema Lukuvi na kuongeza:
“Kamati za utekelezaji wa shughuli za Serikali ziko nyingi sana na siyo
tu za Bajeti. Kwa hiyo ndio maana nakwambia hilo ni jambo dogo sana
ambalo mimi sidhani kama linahitaji kutangazwa, kama lingekuwa hivyo
mimi ningekuwa wa kwanza kutaka kulizungumzia,” alisema.
Kazi ya Kamati
Habari ambazo Mwananchi limezipata zinasema kwamba kamati ya mawaziri
nayo inafanya kazi ya kubuni vyanzo vingine vya mapato ya Serikali, ili
kufidia pengo la baadhi ya kodi ambazo zinatarajiwa kufutwa kutokana na
shinikizo la wabunge.
Miongoni wa kodi hizo ambazo huenda zikafutwa wakati Waziri wa Fedha,
Dk William Mgimwa atakapohitimisha Bajeti yake kesho, ni ile
inayopendekezwa kuongezwa kwenye muda wa maongezi ya simu na ile ya
inayopendekezwa kutozwa kwa waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda.
Kadhalika, kamati hiyo ya mawaziri imepewa jukumu la kuona iwapo
itaweza kushauri uwezekano wa kuongezwa Bajeti ya sasa ya maendeleo
kutoka asilimia 30 inayopendekezwa na Serikali, jambo ambalo pia
limekuwa likipigiwa kelele na wabunge wengi.
“Hatuwezi kufumua Bajeti nzima ila kusema kweli ni kwamba lazima
kutakuwa na mabadiliko mengi, tatizo kubwa ambalo linatuumiza vichwa,
tunajiuliza kama tunaweza kupata hiyo nyongeza ya hizo fedha za
maendeleo walau Sh500 bilioni,”alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Taarifa zaidi zimewataja wajumbe wanaounda kamati hiyo ambayo ilifanya
kikao chake cha kwanza juzi kuwa ni Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk
Mgimwa, Lukuvi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel
Sitta.
Wengine katika kamati hiyo iliyoundwa kwenye kikao cha kazi cha Baraza
la Mawaziri, Jumamosi iliyopita chini ya Pinda, ni Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa
Chakula, Kilimo na Ushirika, Adam Malima na Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima.
Habari zaidi zilidai kuwa mawaziri hao watafanya kazi hiyo sasa na hata
baada ya Bunge la Bajeti ili ushauri wao uweze kuzingatiwa katika
maandalizi ya bajeti ijayo ya 2013/2014.
“Tunawatarajia kwamba watatusaidia hata katika bajeti za kisekta zinazokuja,” alisema mjumbe mwingine wa kikao hicho.
Wasiwasi ulikuwa ni iwapo ushauri wa kamati hiyo utaweza kuzingatiwa
katika majumuisho ya Waziri wa Fedha na Uchumi wakati atakapohitimisha
Bajeti yake, lakini jana Spika wa Bunge, Anne Makinda alifungua milango
inayowezesha Serikali kuongeza vyanzo vipya vya mapato hata baada ya
Bajeti Kuu kupitishwa.
Uamuzi wa Bunge
Jana Spika Makinda alisema Bunge limeahirisha kujadili na kupitisha
Muswada wa Sheria za Fedha wa mwaka huu, na sasa muswada huo utapitishwa
mwishoni kabisa mwa Mkutano wa nane Bunge.
Hatua hiyo ni dalili kwamba Serikali sasa iko tayari kufanya
marekebisho makubwa ya Bajeti yake na hata zile za kisekta, hasa katika
maeneo ya kuongeza vyanzo vipya vya mapato kadri Kamati za Bunge,
wabunge na Kambi ya Upinzani watakavyopendekeza.
Kusogezwa huko pia kumewezesha kuongezwa siku moja ya majadiliano ya
hotuba ya Bajeti kutoka siku nne hadi tano, pia unatoa fursa ya Serikali
kuongeza vyanzo vyake vya mapato kwa kuzingatia maoni, mawazo na
ushauri wa wabunge.
Muswada wa Sheria ya Fedha ulikuwa umepangwa kuwasilishwa kesho kama
hitimisho la mjadala wa Bajeti ya Serikali, lakini sasa umepelekwa mbele
kutokana na kile Makinda alichosema kuwa ni kutoa fursa kwa wabunge
kuishauri Serikali kuhusu vyanzo vipya vya mapato.
Makinda alisema uamuzi huo ulifanywa katika kikao cha Kamati ya Uongozi
cha Juni 18, mwaka huu baada ya kuzingatia maoni ya wabunge, Serikali
na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ambao walitaka kuahirishwa kwake,
ili kuruhusu Serikali kuongeza vyanzo vya mapato kadri
itakavyoshauriwa na wabunge.
Aliongeza kuwa Bunge limeridhika kwamba licha ya kutopitishwa kwa
muswada huo mapema kama inavyotakiwa, bado Serikali itaweza kukusanya
kodi kwa kutumia sheria nyingine za nchi zilizopo.
Mabadiliko hayo ni mwanzo wa mchakato wa mabadiliko ya Kanuni za Bunge
ili kuwezesha vikao vya Bunge la Bajeti kufanyika mapema na
kuhitimishwa Juni 30, ili kuruhusu Serikali kuanza mwaka wa fedha baada
ya Bajeti nzima na Sheria ya Fedha kuwa vimepitishwa.
“Mabunge mengi ya Jumuiya ya Madola yana utaratibu wa kupitisha Muswada
wa Sheria ya Fedha na Muswada wa Mutumizi mwishoni kabisa mwa mjadala
wa Bajeti. Lakini tumefuatilia na kubaini kuwa mchakato wa kupitia
Bajeti ya Serikali huanza mapema na kumalizika kabla ya mwaka mpya wa
fedha kuanza,”alisema Makinda na kuongeza:
“Bunge letu lingepaswa liwe linakutana na kuanza mchakato wa kupitia
Bajeti ya Serikali mapema, ili inapofika Juni 30, mkutano wa Bajeti uwe
umemalizika na Muswada wa Sheria ya Fedha kuanza kutumika ifikapo Julai
Mosi ambapo mwaka mpya wa fedha unaanza”.
Alisema kutokana na hali hiyo Kanuni za Bunge zitaendelea kufanyiwa
marekebisho ili mikutano ya Bunge la Bajeti iweze kuanza mapema kama
ilivyo katika nchi nyingine za Jumuiya ya Madola.
Kwa upande Lukuvi, alisema uamuzi wa Serikali kukubali hoja ya
kusogezwa mbele muswada huo, ni kutoa fursa ya kuzingatiwa kwa maoni ya
wabunge na kuendelea kuibuliwa kwa vyanzo vipya vya mapato.
“Kama Serikali isingekubali, basi ujue hilo la kuahirisha muswada
lisingewezekana kabisa, maana ukishapitisha Muswada wa Sheria ya Fedha
hata maoni yatakayoendelea kutolewa kwenye bajeti nyingine yangekuwa
hayana maana,” alisema Lukuvi.
Mbunge alipua mawaziri
MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), amewataka wabunge kumsaidia Rais
Jakaya Kikwete kuikataa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13, kwa kuwa
mawaziri wake wameshindwa kumsaidia kuleta Bajeti ambayo inajibu
matatizo ya Watanzania.
Alitoa kauli hiyo wakati akichangia kwenye mjadala wa Bajeti na baadaye
kutoa ufafanuzi wa kauli yake nje ya Bunge, kuwa mawaziri wa Kikwete
wameshindwa kumsaidia, kwani wametenga fedha nyingi katika matumizi
mengineyo na kutelekeza mpango wa Serikali wa Miaka Mitano.
No comments:
Post a Comment