Kuna vitu navikumbuka katika maisha yangu, katika
muktadha wa historia nimeona, nimesikia na hata kutenda nimetenda mengi
ijapokuwa sijala chumvi nyingi. Kumbukumbu zangu zinaakumbuka mengi, namkumbuka
Christian Luvanda kila ninaposikia msiba na kweli naamini kuwa pengo la mtu
huliziba mwenyewe, popote unapotutazama Christian, pengo lako bado liko wazi
hajapatikana bado wa kuliziba. Mioyo yetu bado mizito, tunatamani kuamini kuwa
umetutoka lakini tunashindwa kaka yetu,
mioyo i radhi lakini akili zinatukumbusha umuhimu wako kila tunapoamka. Akili
mwamngu haujafutika na sijui ni lini utafutika. Kila siku ninapoamka ni kama
tarehe 31/01/2011 saa kumi na mbili na dakika thelathini na sita asubuhi.
Upumzike pema kaka yetu mpendwa.
Nakukumbuka kila niaposikiliza muziki wa hip hop,
amani ya Tanzania sasa ipo kitanzini wananchi wamepoteza matumaini ( citizens
have lost their hopes). Tunatamani kuendelea kucheka kama watanzania wamoja,
baadhi yetu hatujui nini hasa kipo nyuma ya pazia. Sitaki kukumbusha kuwa
ulifaulu na haukuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya
serikali wala kidato cha tano. Siku hizi wanachaguliwa bila kufaulu.
Nakumbuka, ni kweli mizinga tumechonga sisi asali
wamelamba wao. Mramba asali kamaliza asali mzingani, kasahau kuwa hata siku
moja hakuchonga mzinga ili hali alichovya chovya. Asali ni tamu na kila mtu anaitamani, hata mimi pia, achilia mbali
utamu wake lakini pia ni dawa. Mchana na usiku naitaafuta, najua hata vidonda
vya tumbo vinavyomtesa mama mzazi hupoozwa na asali. Waonjaji wameimaliza
tuliochonga mizinga tumebaki kutazamana. Ndiyo ni kweli, mizinga tumechonga
sisi asali wamelamba wao, kusoma tumesoma sisi kufaulu wamefaulu wao, shule
tumejenga sisi cha ajabu zimegeuka kuwa za kwao, kodi tumelipa sisi huduma bora
za kwao, tumevunjiwa nyumba zetu sisi, tumehamishiwa pembezoni sisi,
tumebebeshwa tofali na vifusi sisi, barabara wanasafilia wao wakati sisi
tukingoja katika msululu wa foleni. Ndiyo, vyao vya kwao na vyetu vidogo
wanavitaka pia bila aibu. Kusoma tumesoma sisi, mitihani tumefanya sisi,
matokeo wanayajadili wao.
Nakumbuka kuwa ni chama cha mapinduzi kila ninapoona
rangi ya kijani, ungetamani uchukie hata kuyatazama majani na miti kwa
mabadiliko haya ya tabia nchi, hakuna tena rangi ya kijani, miti inapukutisha
majani yake, ukame, ni rangi ya khaki kila sehemu kama ulivopenda iwe.
Nakumbuka harakati zako za mpakani na kombati yako ya khaki. Najua baba, mama
na mwana wote wako madarakani na mama amekuwa kaimu wa baba na namsaidia
majukumu ya kiofisi japokuwa katiba yetu iliyozeeka haimpi fursa hiyo lakini
ndiyo demokrasia yetu tuliyoichagua.
Nakumbuka sikutaka kuwa Isack Newton, nikaamua
kutoipenda fizikia na sikupata daraja la kwanza, namkumbuka Sanga Michael
alinisisitiza nisiache kusoma kemia, jeuri zangu na kutotizama mbali
sikumsikiliza, lakini nilikuja jua kwanini nilitakiwan kusoma na sasa
ninawahubiria wote umuhimu niliouona katika hili. Angalau nakumbuka
niliyojifunza katika biolojia, yananipa msaada na mwanga katika katika maisha
yangu ya kibinadamu.
Namkumbuka profesa Shabani kila inapotajwa Udom,
kuishi na kusoma hapa kumenifanya niyaamini maneno ya wahenga kuwa “ Mungu siyo
athumani “, na wala Mungu hawezi kuwa shabani pia. Nakumbuka tarehe 12/06/2011
kila inapotajwa haki. Kumekuwa na haki za mafungu, haki za wafungwa, haki za
wanasiasa, haki za wanafunzi. Haki itakuja kuwa na maana moja mbele ya sheria
ijapokuwa ukubwa wa mafungu yake una tofauti kubwa. Nakumbuka kuwa kuna harufu
ya kifo kila inapotajwa haki.
Namkumbuka Martin Luther King Junior kila ninapomsikiliza
Barack Obama, kifo chake kilishabihiana na haki na leo watu wanaiona haki
aliyoihubiri. Hofu ya kifo ilimtoweka mbele ya kilio cha haki, alijua atakufa
na alijua kuwa atauawa kwa aliyoyahubiri lakini ilimpasa kuhubiri haki. Kuna
maisha yanavutia kama ya hawa wanaharakati, kukiona kifo kilipo na kukifuata
kwa nguvu zako zote ulizonazo.
Namkumbuka Amina Chifupa kila ninapowaona mateja
(wala unga), iliniuma nilipowaona wengi mpaka katika viunga vya manispaa ya
Iringa. Naona kuwa ujasiri wa mtu mara kwa mara hurandana na kifo. Vaa ujasiri,
sema kweli na hubiri kweli katika maisha yako na jiandae na kifo na kama
unaamini katika Mungu, fanya toba kila mara unapokuwa umeamua kuhubiri haki.
Nalikumbuka Azimio la Arusha na maneno ya hayati
baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kila nipoona jahazi la Tanzania
likienda mrama katika bahari hii ya dhiki. Wanasema kuwa na rasilimali siyo
utajiri kwa nchi, utajiri wan chi ni uwezo wa wananchi kuzibadili rasilimali
walizonanzo kuwa pesa. Najiuliza ni kweli wasemayo? , najiuliza ni wapi hasa ni
wananchi wa hii nchi wenye jukumu la kubadili rasiimali hizi kuwa pesa? Maana
ni kama kuna wananchi wa aina mbili, wenye jukumu la kubadilisha rasilimali
hizi kuwa pesa na wenye jukumu la kufaidi pesa zilizobadilishwa kutoka katika
rasilimali hizi za nchi.
Naamini rushwa na ufisadi ni mapacha wa kufanana,
sijalisahau bado azimio la Zanzibar. Wahenga walisema “ usipoziba ufa utajenga
ukuta”. Hakuna ugumu kuandaa tume kuchunguza, hakuna ubaya kurudi nyuma na
kujitathmnini, ugumu unakuja katika kufanya maamuzi, ubaya unakuja katika
kufanya maamuzi sahihi. Urahisi unatoka wapi kumsema mwenzio kuwa ni mchafu ili
hali wote mmezama katika shimo lililojaa kinyeshi?. Kinyesi ni kinyesi na
kitabaki kuwa ni uchafu hata kama wewe katika utashi wako utabadili ukweli na
kuona kuwa kinyeshi si kichafu na kuamua kukila. Msafi na mchafu kwa hakika
hawafanani, lakini hata wasafi kuna usafi wa ndani na usafi wan je, pia hata
wachafu kuna waliowachafu ndani mpaka nje na kuna waliowasafi nje ndani
wachafu. Ubaya wa unafiki ni kwamba humchafua mtu nje ambako ndiko huonekana na
watu na uzuri wa ukweli ni kwamba humsafisha mtu ndani na kumpa amani.
Najua mafuta ya ng’ombe mzee hayakatwi kwa kisu butu
nab ado naamini hatua ya kwanza kuelekea mafaniko ni uthubutu. Bado haijafutika
akilini mwangu ziara ya tarumbeta na injili ya mapacha watatu. Kivipi mwanadamu
kutangaza utu ili hali hausadiki?. Matendo ya muhubiri na maneno yapasa kweli
kurandana ili kuleta maana ya unachokizungumza kwa hadhira.
Najua sadaka hutolewa kuunusuru utu wa mtu, sadaka
itolewayo kuinusuru dhuluma siyo sadaka ni kufuru. Iweje usimame mbele ya
wanadamu kutangaza umetolewa sadaka?. Maandiko ninayoyaamini yananifundisha
kuwa sadaka ilikwishatolewa moja ya mwanakondoo wa kweli aliyeshinda mauti.
Umeunusuru utu wa mtanzania ama umeinusuru dhuluma dhidi ya utu wa mtanzania .
matendo machafu bado naamini yanahitaji toba iliyo ya kweli, nakumbuka kufanya
toba na kumuangukia Mungu wangu kila ninpofanya kosa nab ado naamini hajanitoa nilikotoka
ili nije niishie hapa nilipofika sasa, safari yangu bado ni ndefu katika haya
mapito ya dunia.
Hawakumbuki wanaendesha juu ya barabara ya Shaabani
Robert, nakumbuka kuwa wanaendesha katika nchi ya kusadikika. Mwanadamu anakuwa
na matarajio gani pale anapokata tawi la mti ambalo yeye mwenyewe amelikalia?.
Bila shaka ni anguko kuu litakaloacha vizazi vyake bila chochote cha kujivunia
isipokuwa taabu, dhiki na mahangaiko.
Namkumbuka profesa Seith Chachage na Makuhadi wa
Soko Huria wakati ninapoona mashirika ya umma yakihudhuria sherehe za minada ya
hadhara ya majengo ya ofisi zao kutokana na kufilisika. Bado sijasahau namsoma
profesa Issa Shimvji ndani ya Insha za Wanyonge ili hali jasho laangu bado
halinikauki na nawaona wanyonge wenzangu wengi bado wakilisaka tonge. Bado nina
uelewa ulio tata kila ninapozisoma insha za Mabala wa Mabala, Hidaya taabu
mjini, mpenziwe Frank naye bado anahaha na kijiji. Bado sisahau kila asubuhi
najiuliza swali ni vipi hili taifa change lenye nusu karne nitalijenga.
Natamani kuwa mwandishi kama Paschally Mayega,
nimfundishe kila mtu yale niyawazayo akilini ili name niwe mwalimu mkuu wa
watu. Nimfundishe japo mtu mmoja kuwa uzalendo haupatikani jkt bali mnaotaka
kutupeleka ndiyo mmeukalia uzalendo tusiuone katika macho yetu. Kivipi amani
kwa ncha ya upanga na wananchi kila siku mtaani wanaumia. Naikumbuka miezi mine
ya njaa kila ninapokisoma cheti cha BAIR na ninshaambiwa bila undugu sipati
kazi wizara.
Namkumbuka Daudi Mwangosi kila ninapowaona askari
polisi, nakumbuka yaliyotokea Nyololo njia panda iendayo shule ninayoipenda
Igowole sekondari. Nasisimka, mwili joto kali kama ninapigwa pasi. Maaskofu
roho mkononi, uko wapi umoja na mshikamano wa watanzania tuliojivunia?, uko
wapi umojaa baba wa taifa aliotuachia. Nakumbuka ulituunganisha kwa lugha ya
Kiswahili, ukakipenda , ukakitangaza na ukakiheshimisha kote barani afrika,
lakini nakumbuka ulipigania umuhimu na nafasi ya lugha ya kiingereza kubaki
palepale kilipo.
No comments:
Post a Comment