FOLLOWERS

Wednesday, August 1, 2012

SOMA : SEHEMU YA PILI YA BARUA NDEFU YA ADO SHAIBU KWA PROFESA ISA SHIVJI

PROFESA ISSA SHIVJI

BARUA NDEFUKWA KOMREDIPROFESA ISSAGULAMHUSEIN SHIVJI (2).
 Kutoka kwa Ado Shaibu,
S.L.P kijiji cha Namasakata,
Wilaya ya Tunduru.


Kwako Komredi Profesa Issa Shivji,Shikamoo! Ni matumaini yangu kwamba waraka wangu wa kwanza ulikufikia. Kabla ya kuendelea na barua yetu ya leo, ngoja nikupe mchapo kidogo. Majuzi nilikuwa kijijini kwetu Namasakata. Usiku niliwakusanya vijana wenzangu nakuwasimulia habari zako.
 Nilipowasimulia ile habari ya wewe kuwakatalia mwaliko Maprofesa wenzakowa ng’ambo waliotaka ukatoe mada kwenye chuo chao huko ulaya, vijana wale wa Namasakata waliduwaa sana. Niliwaeleza msimamo wako wa kugomea mwaliko ule ‘’mnono’’ ili kuonesha mwitiko wako kwa uvamizi wa kimabavu wa Marekani nchini Iraq. Nakumbuka ulivyotueleza wazi wakati ule kwamba ile haikuwa vita dhidi ya silaha za maangamizi kama walivyodai mabingwa wa propaganda za kivita, bali ilikuwa vita ya kugombea mafuta. Miaka michache baadaye, Rais George Bush alikili hadharani kwamba uvamizi wa Iraq ulifanywa kimakosa. Hongera sana kwa msimamo ule. Zama hizi wasomi wenye msimamo ni wachache sana.
Wanakijiji wa Namasakata wanakukaribisha sana kijijini kwetu ujionee mwenyewe jinsi wanavyoyumbishwa na sera za uliberali mamboleo zililozalisha soko holela badala ya soko huria. Kwa mfano, msimu wakorosho wa mwaka huu wanakijiji wa Namasakata wamekaa kwa miezi zaidi ya minne bila kulipwa pesa zao za korosho. Naambiwa hali ni hiyohiyo kwa wakulima wa Tandahimba, Newala, Masasi, Pwani na mikoa yote ya kusini.
Sasa turudi kwenye barua yangu. Kama nilivyokueleza awali kwenye barua yangu ya kwanza, waraka wangu ni mjumuiko wa maswali kuhusu taifa letu. Maswali haya yananisumbua sana; yananichoma ndani kwa ndani kwa kukosa majibu. Nimekuwa nikijiuliza maswali haya kila muda: najiuliza mchana na usiku. Sasa naomba nianze maswali yanguna ni matumaini yangu kwamba utanipatia majibu mujarabu.
Swali langu la kwanza linahusu itikadi ya ujamaa na kujitegemea, hususani Azimio la Arusha.Profesa kwa miaka nenda rudi unahubiri Azimio la Arusha.Ingekuwa kwenye muktadha wa ulimwengu wa kiroho ningekuita nabii wa Azimio la Arusha!Ni adimu kwa wewe kuhutubu eneo fulani bila kulitaja Azimio la Arusha.
Swali langu ni kutaka kujua kwa nini unaendelea kulishabikia Azimio katika zama hizi. Umesahau kauli ya mwalimu Nyerere mbele ya wanahabari  kwamba inahitaji roho ngumu mithili ya ile ya mwendewazimu kulizungumzia Azimio katika zama za leo? Si bado unakumbuka maneno ya Mzee Ruksa wakati akiling’oa azimio la Arusha na kusimika Azimio la Zanzibar kwamba’’kila kitabu na zama zake’’?Majuzi nilistuka nilipomsikia Mzee Ruksa na Mzee Cleopa Msuya wakijivua lawama ya kuliua na kulizika azimio la Arusha na kudai waliolivunja ni ‘’viongozi maharamia’’ wasiomuogopa Mungu.
Hiyo inaweza kuwa mifano ya zamani kidogo.Nina imani unakumbuka mfanowa karibuni pale Amiri Jeshi Mkuu wa sasa alipohojiwa ughaibuni kuhusu Azimio la Arusha na kuweka wazi kwamba ‘’ujamaa hausawili mazingira yetu ya sasa’’?
     Majuzi wakati tunamuaga Profesa Goran Hyden pale ukumbi wa Nkurumah, kuna vijana walipinga fikra za usasa za uliberali mamboleo na kukumbushia misingi ya Azimio la Arusha; misingi ya utu na usawa. Nakumbuka Barozi Mwapachu aliwang’akia vijana wale kwamba wasiendelee na fikra za kijamaa zisizotekelezeka katika dunia ya leo na aliwaasa wahadhiri wa UDSM waachane na mtindo wa upandikizaji wa fikra za ki-maksi kwa wanafunzi: fikra muflisi zilizofeli!
       Nini lengo lako kulishadidia Azimio la Arusha wakati ‘’wenye dola’’ na wanazuoni wa kimamboleo wanalipondaponda na kuweka wazi kwamba kwenye dunia ya leo ya utandawazi, kufungua milango wazi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ni suala lisilo na mbadala?
Nimesoma sehemu fulani(ukimnukuu Mwalimu Nyerere) kwamba misingi ya Azimio la Arusha itarudi(hasa misingi yake ya usawa na utu) na kwamba dalili za wazi za ‘’ufufuo’’ wa Azimio la Arusha zimeanza kuonekana.
Unamaanisha una matumaini kwamba Azimio litarudi tena Tanzania?kwamba viongozi wetu hawatomiliki tena hisa kwenye kampuni za kibwanyenye?wasipokee mishahara miwili au zaidi?wasiwe wajumbe wa bodi za mashirika na makampuni ya kibeberu?Unamaanisha tutarudisha tena vijiji vya ujamaa na kutaifisha makampuni?Unamaanisha nini unaposema azimio linarudi?
    Najua kama  azimio litarudi,halitowakataza tena viongozi wetu wafanyabiashara kufanya biashara ya kupangisha nyumba.Na sasa tunaambiwa wana majumba mpaka Arabuni na Ulaya.Nina uhakika azimio jipya litaporudi halitoweka sharti hilo litalowakosesha raha viongozi wetu watukufu.Hata Mzee kingunge alisema kwa hili la kuwanyima viongozi wetu kufanya biashara ya kupangisha nyumba walipotoka!(rejea mazungumzo yako na mzee Ngombale Mwilu kwenye jarida la Chemichem toleo la pili)
        Halafu kama azimio linarudi;ni nani analirudisha?Mmetufundisha darasani kwamba ujamaa wa kiafrika,tofauti na ule wa kisayansi wa karl Marx na Fredrick Engels,uliletwa na viongozi waliopigania uhuru na sio vuguvugu la kimapinduzi la wafanyakazi na wakulima.Uliletwa na kina Nyerere,Nkurumah na Tom mboya.Ni viongozi gani wataolirudisha azimio hivi leo?Ni viongozi hawahawa wanaopokea posho mbili bungeni kwa kazi ileile?Ni viongozi hawahawa wanaopayuka majukwaani  na kulalama kuhusu matumizi mabaya ya serikali wakati wao wenyewe wakiendesha magari ya kifahari ya serikali na kula mlungula?
    Kwamba viongozi hawa wanaopokea posho namishahara mitatu na zaidi kwa kazi ileile watakaa bungeni na kupitisha sheria hata yenye harufu tu ya Azimio la Arusha;Sheria ya kuwabana wasijilimbikizie ukwasi wakati masikini wa kijijinikwetu Namasakata na kwingineko Tanzania wakitaabika kwa ufukara?Thubutu!kwamba viongozi hawa watapata ufunuo mpya na kuwachukulia ‘’wasakatonge’’Kuwa ni binadamu wenye haki na wanastahili usawa?
Au sijakuelewa Profesa?Pengine unamaanisha watu wenyewe wataridusha Azimio.Kwamba umma wenyewewa wanyonge utapigania usawa na kushiriki kujenga ujamaa?Lakini profesa si unajua nguvu ya dola? Ni naniwa kuanzisha vuguvugu la wanyonge katika mazingira ya sasa? Ni nani atakuwa Lenin na Trosky wetu; Mao Tse Tung wetu; Fidel Castro na Che Guavala Wetu? Ni nani wa kuwaongoza wanyonge kwenda kwenye usawa na haki?
Si umetufundisha mwenyewe kwamba vuguvugu la wafanyakazi lilianza kuchipua Tanzania tangu miaka ya sabini?(Rejea kazi yako ya Working class in Tanzaniana Silent Class Struggle, utafiti wako wa enzi zile ukiwa kijana ).Nani alizima vuguvugu lile la wanyonge?watashindwa nini kuzima vuguvugu lolote la wanyonge sasa? Au umesahau mkong’oto waliokumbana nao wamasai wa Loriondo?Madam Shamsa Mwangunga alisema waliofurushwa ni wakenya! Kwa Kweli nilipomsikia tumbo langu liliunguruma kwa hasira.
       Majuzi nimebahatika kupitia tamko la Mtandao wa Vikundi  vya Wakulima Wadogo Tanzania(MVIWATA) walilolitoa pale Morogoro kuadhimisha miaka hamsini ya uhuru wetu.
     Naomba nikukumbushe waliyoyasema wakulima wale: kwanza waliweka wazi sikitiko lao kuhusu kusalitiwa kwa misingi ya Azimio la Arusha na hivyo basi kukuza pengo baina ya walalahoi na walalaheri. Pia waliweka wazi kwamba wanapinga kwa nguvu zote ukandamizaji na unyonyaji wanaofanyiwa wakulima wa Tanzania na wakoloni mamboleo kwa kushirikiana na makuwadi wa ubeberu. Nilihamasika sananiliposoma kwamba wameamua kuchukua hatua ya kukuza umoja wa wakulima wanaonyonywa na kukandamizwa.
Unajua suluhu waliyoisema? Kwamba watawanyima kura wanasiasa uchwara wote na pia watapiga kelele dhidi ya dhuluma ya wakulima. Ninachojiuliza ni kama wakulima hawa wanalenga kulirudisha Azimio la Arusha au wanachotaka ni maslahibora ndani ya ubepari? Kama wanataka Azimio, watalirudishaje? Katika vyama vyetu, ni nani watayempa kura ambaye ana ndoto na nia thabiti ya kulirudisha Azimio la Arusha?
Kuna jambo la msingi nilitaka kusahau. Profesa, sisi tuliozaliwa zama za rais Mwinyi hatujashuhudia mengi kuhusu ujamaa. Tumeishia kuusoma ujamaa vitabuni tuna kusimuliwa. Na kama unavyojua, vitabu vinachanganya kwelikweli! Mupo mulioandika jinsi ujamaa ulivyokuwa mfumo wa usawa na utu: mmetusimulia jinsi ujamaa ulivyolenga kumkomboa mnyonge kutoka katika minyororo ya unyonyaji na madhila mengineyo.
Lakini Profesa, wapo wengine, tena wengi sana wameandika na kusimulia mabaya ya ujamaa. Wapo wanaosema ujamaa ulitaka kutaifisha kila kitu hadi magenge na vijiduka vya mitaani ambavyo kimsingi vilipaswa kuendeshwa na watu binafsi. Si unakumbuka ule utani wa wakenya kwamba ‘’kama unataka vitu vya bure nenda Tanzania ambako watu wanachangia kila kitu ikiwemo wake zao?’’
Wapo pia wanaokumbushia operesheni vijiji ya miaka ya sabini na dhahama yake. Wengine wanakwenda mbali zaidi na kukumbushia jinsi uhaba wa bidhaa muhimu ulivyotamalaki wakati ule wa ujamaa.Hata rais mkapa alikumbushia baadhi ya madhila haya mulipomuita pale Nkurumah majuzi. Si unakumbuka alivyounguruma na kumpongeza Mzee Salim Ahmed Salim kwa uamuzi wake wa ‘’kizalendo’’ wa kufungua mipaka ili kupunguza uhaba wa bidhaa aliodai uliletwa na sera yetu ya ujamaa na kujitegemea?
Binafsi naomba kutangaza maslahi kwamba nauhusudu baadhi ya sera za ujamaa.Kwanza neno lenyewe ‘’ujamaa’’ limekaa kiutu.Lakini hii haimaanishi kwamba ujamaa ni msahafu! Ni lazima tujifunze tulipojikwaa miaka ile ya sabiniili tusidondoke tena. Hili litawezekana kama tukifanya tafakuri ya kina na kuudurusu ujamaa.
 Kama kweli ndoto zako (na za Mwalimu Nyerere) kuhusu ufufuo wa Azimio la Arusha zitatimia, basi rai yangu ni kwamba katika huo ujamaa mpya, wanavijiji washirikishwe kikamilifu kabla ya operesheni yeyote ya vijiji: Programu za maendeleo ziendeshwe kwa kuzingatia sheria na sio kwa ubabe kama ilivyokuwa miaka ile. Pia serikali isijihusishe nashughuli za uchuuzi kama enzi zile: Ijihusishe na biashara kubwa kubwa tu. Je pia huoni mahitaji ya kudurusu miiko yetu ya uongozi ya enzi zile ili iendane na wakati kama wanavyosema wengi?
Sasa nikuulize swali langu la pili……
Kwa maoni e-mail adoado75@hotmail.com au ado75haki@gmail.com simu: 0653619906.
               

6 comments:

Anonymous said...

kazi nzuri mkuu..je we bado unaamini ujamaa una nafasi katika maisha yetu hivi sasa hasa kwenye dunia yetu ya utandawazi?

Unknown said...

ulifanya makosa kulitupa azimio la arusha jumla..baadhi ya tenets za ujamaa kama vile miiko ya uongozi,serikali kuhodhi baadhi ya sekta nyeti,usawa na utu zina mashiko mpaka leo..kwa mawazo yangu, nadhani tunapaswa kudurusu mfumo huu na kuchukua baadhi ya mambo yaliyo na umuhimu kwetu..though i also admit that baadhi ya mambo ya azimio yalifaa zaidi kama vile kukataza viongozi wasipangishe hata nyumba na kununua hata hisa moja yalifaa zaidi wakati ule wa miaka ya themanini kuliko yalivyofaa sasa..

Unknown said...

hapo juu i mean (tu)lifanya makosa kuutupa ujamaa kwa ujumla and not (u)lifanya makosa..

gabriel batikwisa said...

kazi nzur but mi siamini kama yupo wa kuturejesha kwenye usawa..watu wabinafsi sana kaka..azimio hawawezi kulipenda sababu liliwakosesha utajiri..hapo unaposema wabunge wetu wanapayuka majukwaani huku wakila mlungula na kuendesha magari ya kifahari unamzungumzia mh zitto?

Unknown said...

binafsi mpaka sasa sijaona chama chochote kinachohubiri azimio la arusha..kipo chama cha kulirejesha na kulihifadhi kwa maanisha azimio la arusha kweli? sidhani kama kipo...ikiwa mwalimu nyerere muasisi wa azimio la arusha alishuhudia azimio la arusha likichinjwa na kuzikwa kwa azimio la kisiri siri la zanzibar 1992 na akashindwa kulinusuru pamoja na uzalendo na influence aliyokuwa nayo..nani anaweza kusimama leo kulihubiri azimio la arusha??..."kuzungumzia azimio la arusha inahitaji mtu uwe na akili ya mwendawazimu..julius nyerere"

Unknown said...

mkuu gabriel batikwisa, suala la zitto bado ni pre-mature..after all, makala hii niliiandika kitambo kidogo japo kwenye jukwaa hili imewekwa karibuni..but ukweli kwamba viongozi wetu ni wabinafsi hauna shaka..umesahau mbunge wa bahi ana kesi ya kujibu mahakamani kwa sababu ya kula mlungula?

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...