LIGI KUU TANZANIA BARA 2012/2013
Michuano
ya Ligi Kuu kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu wa 2012/2013
itaanza Septemba 15 mwaka huu kwa timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja
tofauti.
Mechi
za ufunguzi zitakuwa kati ya Simba vs African Lyon (Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam), Polisi Morogoro vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro),
Tanzania Prisons vs Yanga (Sokoine, Mbeya), Mgambo JKT vs Coastal Union
(Mkwakwani, Tanga), JKT Ruvu vs Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es
Salaam), Kagera Sugar vs Azam (Kaitaba, Bukoba) na Toto Africans vs
Oljoro JKT (Kirumba, Mwanza).
Mzunguko
wa kwanza (first round) utamalizika Novemba 11 mwaka huu ambapo kwenye
mzunguko huo mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba itachezwa Oktoba 3
mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ligi
hiyo itamalizika Mei 18 mwakani kwa mechi kati ya Toto Africans vs
Ruvu Shooting (Kirumba), Mgambo JKT vs African Lyon (Mkwakwani), JKT
Ruvu vs Mtibwa Sugar (Azam Complex), Tanzania Prisons vs Kagera Sugar
(Sokoine), Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Azam (Sheikh
Amri Abeid Kaluta) na Polisi Morogoro vs Coastal Union (Jamhuri).
Endapo
Simba na Azam hazitafanikiwa kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi
ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa
marekebisho.
MECHI YA UFUNGUZI WA MSIMU WA LIGI 2012/2013
Mechi
ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria ufunguzi rasmi wa Ligi
Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 kati ya bingwa mtetezi Simba na
makamu bingwa Azam itachezwa Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
MTIHANI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI SEPT 27
Mtihani
kwa ajili ya watu wanaotaka kuwa mawakala wa wachezaji wanaotambuliwa
na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Septemba
27 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
Kwa
wanaotaka uwakala huo wanatakiwa kujisajili ambapo watapewa kanuni
mbalimbali za FIFA na TFF ili waweze kujiandaa kikamilifu kwa mtihani
huo utakaokuwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni maswali kutoka FIFA
wakati nyingine ni kutoka TFF. Ada ya mtihani ni dola 50 za Marekani.
Pia
Damas Ndumbaro na Ally Mleh wa Manyara Sports Management ambao tayari
ni mawakala wanaotambuliwa na FIFA wanatakiwa kufanya mtihani huo kama
wanataka kuendelea na uwakala kwa vile muda wa leseni zao za awali
umemalizika.
Mawakala wengine ambao ni John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully leseni zao bado ziko hai.
WACHEZAJI 17 WAPINGWA KWENYE USAJILI
Klabu
mbalimbali zimewasilisha pingamizi Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kupinga usajili wa wachezaji 17 walioombewa usajili
katika timu za Ligi Kuu.
Toto
Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton
aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal
Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.
Pia
Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday
Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu
za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa
beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho
haijalipwa.
Super
Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake
wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert
Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union)
kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho
hazikufuatwa.
Mchezaji
Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT
kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo
Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili
wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya
kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.
Azam
inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo
bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani. Nayo Simba inapinga
Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye
uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.
Vilevile
Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika
usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na
klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na
nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na
klabu hiyo.
Nayo
Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte,
Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za
kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la
Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile
ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi
lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa
kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati
wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo,
Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng,
Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti
wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu)
kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa
2012/2013.
SERENGETI BOYS KUJIPIMA KWA ASHANTI
Timu
ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys)
iliyokuwa kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Kenya itavunja rasmi
kambi yake kesho (Jumamosi) kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Ashanti
United.
Mechi
hiyo dhidi ya Ashanti United iliyoko daraja la kwanza itachezwa kuanzia
saa 10 jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa
kiingilio cha sh. 2,000.
Serengeti
Boys ilikuwa Septemba 9 mwaka huu icheze na Kenya kwenye mechi ya
raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17,
lakini Kenya ikajitoa ambapo sasa itacheza na Misri katika raundi ya
pili. Mechi ya kwanza itachezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es
Salaam.
Mwishoni
mwa Septemba, Serengeti Boys itarejea tena kambini kujiandaa kuikabili
Misri ambapo kabla inatarajia kupata mechi ya kirafiki ya kimataifa
dhidi ya timu itakayotangazwa baadaye.
MCHEZAJI WA MTIBWA SUGAR NAYE APATA ITC
Shirikisho
la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) limetuma Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Ayoub Hassan Isiko aliyejiunga na
Mtibwa Sugar akitokea timu ya Bull FC ya nchini humo.
ITC
hiyo ilitumwa jana (Agosti 30 mwaka huu), hivyo kufanya wachezaji ambao
ITC hazijapatikana hadi sasa kubaki wawili tu. Dirisha la usajili wa
wachezaji litafungwa rasmi Septemba 4 mwaka huu.
Wachezaji
ambao ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng
kutoka AFC Leopards ya Kenya waliojiunga na Simba. ITC hizo zinatarajiwa
kupatikana wakati wowote kwani tayari Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limeshaziomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya
(FKF) baada ya nyaraka zote zilizokuwa zikitakiwa kupatikana.( KWA HISANI YA FATHER KIDEVU BLOG)
|
No comments:
Post a Comment