FOLLOWERS

Thursday, August 2, 2012

MAALUM KWA WAGOMBEA UVCCM : UMOJA WA VIJANA NA FIKRA MGANDO


UMOJA WA VIJANA NA FIKRA MGANDO
 Ado Shaibu.

     Kimuundo, vyama vya siasa huwa na jumuiya za kuiwezesha kutimiza matakwa yake ya kisiasa. Mathalani, kwa upande wa CCM kuna Jumuiya ya Wazazi, Umoja wa wanawake (UWT) na Umoja wa vijana (UVCCM). Hata baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, muundo wa vyama vingi vya siasa nchini umenakili kwa kiwango kikubwa muundo wa taasisi na jumuiya za CCM. Kwa mfano, kwa upande wa CHADEMA, kuna Baraza la Wanawake (BAWACHA) , Baraza la wazee wa chama na baraza la vijana (BAVICHA).
  Lengo la makala hii ni kuelezea, japo kwa ufupi, mchango wa umoja wa vijana katika chama cha siasa na kutoa changamoto kwa jumuiya za vijana katika vyama vyetu vya siasa vya leo katika mfumo wa vyamavingi. Haitoshangaza kuona nikitupia jicho CCM kwa kiwango kikubwa kuliko vyama vingine kutokana na ukweli kwamba chenyewe ndicho kilichobeba dhamana ya kuwaletea maendeleo watanzania mpaka uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
   Tukidurusu historia ya nchi yetu , tutakumbuka kwamba uanzishwaji wa jumuiya za vijana katika vyama vya siasa sio jambo geni hata kabla ya uhuru. Kwa mfano, kwa upande wa Tanganyika, kulikuwa na ''Tanu Youth League''(TYL) na kwa upande wa zanzibar, kulikuwa na ASP Youth League.
   Katika makala zangu zilizopita huko nyuma katika gazeti hili, nimewahi kueleza kwa ufupi mchango wa tawi la TANU Youth League pale chuo kikuu (UDSM) na Umoja wa Wanafunzi Wanaharakati ( University Student Revolutionary Front-USARF).
   Tofauti na hali ilivyo sasa kwenye vyama vya siasa ambapo kwa sehemu kubwa vijana hutumiwa kama wapambe tu wa wawania nafasi za uongozi ndani ya vyama , enzi hizo TYL na USARF yalikuwa majukwaa ya kujadili, kutathmini na kuchukua hatua kuhusu mustakabali wa Tanzania, kupaza sauti kuhusu ukombozi wa Afrika na kutetea wanyonge wa pande zote za ulimwengu.
   Hebu nitoe mifano michache: Wakati Tanzania ilipotangaza Azimio la Arusha mwaka 1967 ili kuondosha unyonge wetu na kukata mirija ya unyonyaji iliyowanufaisha mabwanyenye wachache, umoja wa vijana wa TANU haukuishia kutoa matamko ya kuunga mkono azimio na kutembea kilomita nyingi kuiunga mkono TANU kwa uamuzi wa kizalendo na wenye kuleta nuru ya matumaini kwa wanyonge walio wengi.
  Kwa upande wa tawi la TYL pale mlimani na umoja wa USARF, wao walienda mbali zaidi na kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha ufanisi wa sera na programu za azimio la Arusha zilizolenga kuwakomboa wanyonge hasa wakulima na wafanyakazi wa kada ya chini.
   Wanachama wa TYL na wale wa USARF kama kina Issa Shivji (sasa profesa wa kigoda cha mwalimu Nyerere katika umajumuhi wa Afrika), Karim Hirji (sasa profesa wa biostatistics chuo kikuu cha Afya- Muhimbili), Zakia Hamdan Meghi (sasa mbunge wa kuteuliwa na rais na waziri wa zamani wa fedha) Yoweri Kaguta Museveni ( sasa rais wa Uganda), Henry Mapolu (sasa marehemu) na wengineo wengi ambao ni vigumu kuwaorodhesha wote, walipigana vilivyo kulijenga Azimio la Arusha kwa vitendo.
    Wana TYL na makomredi wa USARF wa pale mlimani walizunguka katika shule za sekondari mikoani na kufundisha itikadi ya ujamaa na kujitegemea; walitembelea vijiji vya ujamaa; kulima mashamba na wanavijiji kwenye mashamba ya vijiji na kujadili nao ujenzi wa sera ya ujamaa na kujitegea. kwa wanawake kama Zakia Hamdani Meghi wa miaka ile, huu ulikuwa wasaa wa kuuvua utukufu wa uanachuo na kushirikiana na wanawake wa vijijini kuteka maji visimani, kupika chakula na kutafakari kwa pamoja kuhusu ukombozi wa mwanamke wa Afrika.
    Mpango wa elimu kwa watu wazima ulipoanzishwa miaka ya sitini wanachuo wa umoja wa vijana wa TANU na wenzao wa USARF hawakuishia kuwa watoa matamko ya kupongeza tu; kumbukumbu zinaonyesha walishiriki kikamilifu kuwafundisha kina mama na wazee kufuta ujinga. Walitenga muda wa ziada kuwaongoza wazee wa mijini na vijijini katika vita ya kufuta ujinga wa kutojua kusoma na kuandika kupitia madarasa ya elimu ya watu wazima.
   Pengine tofauti kubwa kabisa baina ya jumuiya za vijana za miaka ya sitini na sabini kwa upande mmoja na jumuiya za miaka ya leo kwa upande mwingine; tofauti ambayo huko nyuma nimewahi kuimithilisha na tofauti ya kichuguu na mlima kilimanjaro, ni kuhusu kufanya utafiti. Kwa kweli yapo malalamiko kwamba vijana wa sasa tunahusudu kukurupuka kutoa matamko, tuhuma na malalamiko bila kufanya uchambuzi wa kina na utafiti.
    Wana TYL na USARF wa miaka ya sitini na sabini walihusudu sana kutanguliza utafiti kabla ya kuyatolea matamko masuala mbalimbali. Ukipata bahati ya kusimuliwa jinsi USARF ilivyoanzisha madarasa yake ya mijadala na itikadi kila wikiendi pale mlimani lazima utakiri jinsi vijana wale walivyojibidiisha kuusaka ukweli, kuusambaza na kuusimamia. Pia, kijarida cha ''Cheche'' kilichotolewa na USARF na kujizolea heshima hadi nje ya mipaka ya nchi, kilisheheni mada za kiutafiti kuhusu masuala mbalimbali ya jamii ya Tanzania na dunia kwa ujumla zilizowasilishwa na wanafunzi na wahadhiri kama kina Profesa Walter Rodney.
    Kilele cha mafanikio ya utafiti wao wa ujanani kilifikiwa kwa utafiti wa profesa shivji (enzi za uanafunzi wake) uliokwenda kwa jina la ''silent class struggle'' katika jarida la ‘’cheche’’. katika utafiti huo uliowakera baadhi ya watawala wa miaka hiyo, pamoja na mambo mengine, Prof.Shivji alionya kwamba badala ya kujenga ujamaa kama ulivyofafanuliwa na Azimio la Arusha, taratibu tabaka la mabwanyenye wa kiutawala ambao Prof.Shivji aliliita ‘’Bureaucratic bourgeoisie’’ lilianza kuchomoza Tanzania.
   Licha ya kupuuzwa kwake miaka ile, takribani muongo mmoja baadaye, CCM ilikiri ukweli wa Prof.Shivji katika muongozo wa CCM wa mwaka 1981 kwamba kulikuwa na kuchipua kwa tabaka jipya la mabwanyenye na wahujumu uchumi walioanza kuhujumu ufanisi wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea.
   Pia kumbukumbu zinaonyesha kwamba baadhi ya sera za taifa zilitokana na ushawishi wa Umoja wa vijana wa TANU. Kwa mfano, kumbukumbu za wizara ya ulinzi na Jeshi la kujenga taifa zinaonyesha kwamba uamuzi wa kuanzisha jeshi la kujenga taifa (JKT), ulitokana na mapendekezo ya mkutano mkuu wa TYL uliofanyika tarehe 25 Agosti 1962 mjini Tabora chini ya Joseph Nyerere aliyekuwa katibu wa umoja huo.
     kiujumla yako mambo mengi yaliyotekelezwa na jumuiya za vijana miaka ya sitini mpaka themanini. Kadiri Rabana atavyotujalia uhai na fursa zaidi, tutaendelea kuchambua michango hiyo ili vijana wa leo tupate darasa la kujadili na kujifunza kutoka kwa vijana wa enzi hizo.
   Sasa tujiulize swali la msingi; Je umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) na jumuiya za  vijana za vyama vya upinzani zinatekeleza majukumu yake ya kihistoria kwa ukamilifu? Ukiachilia maeneo machache, hasa katika utoaji wa matamko na maandamano ya kuunga mkono hotuba za viongozi wa kitaifa, jumuiya za vijana zimepoteza kwa kiwango cha kutisha jukumu lake la kihistoria la kuwasemea vijana, kuyatafiti matatizo ya vijana na kuishauri serikali kuhusu mambo mbalimbali yanayoviza mustakabali wa vijana na kufifisha ustawi wa taifa letu kwa ujumla.

    Kwa mtizamo wangu, badala ya vijana wa UVCCM kuitisha vikao na kulumbana kuhusu atokako rais ajaye wa Tanzania, nilitamani vijana hao wangeitisha vikao vya kutathmin mustakabali wa ‘’machinga’’ wa ubungo, Tandika na kwingineko Tanzania wanaofurushwa na wanamgambo wa jiji bila kuelekezwa pa kwenda.
   Binafsi nilidhani badala ya UVCCM kuunda kamati ya kutatua matatizo ya kufikirika, ingeunda kamati ya kudurusu ule mkakakati wa serikali wa ‘’nguvu kazi’’ (Human Resources Deployment Act,1983) na kutafakari changamoto zake ili kuepusha matatizo waliyokumbana nayo wafanyabiashara ndogondogo wa miaka ile  ya themanini yasiendelee kuwakumba wafanyabiashara wa sasa katika mipango ya jiji. Nilidhani kwa ujana wao, wangejibidiisha kutafakari na kutathmini namna ya kutengeneza mfumo bora zaidi utaowafanya wafanyabiashara ndogondogo ambao wengi wao ni vijana, kujiingizia kipato zaidi na kutoa mchango wao kwa taifa bila kubughudhiwa.
  
   Mimi nilidhani badala ya wana UVCCM kujibidiisha kuunda makundi hasimu ya kambi za urais wa 2015, wangejibidiisha kufanya tafakuri ya kina ya tatizo la ajira ambalo viongozi wa chama na serikali wamelibatiza kuwa ‘’bomu linalosubiri kulipuka’’ na kwa njia ya utafiti, kutafuta hatua mujarabu za kuchukua katika kuzalisha ajira zaidi na kuwakomboa mamilioni ya vijana wanaoshinda vijiweni kwa kukosa ajira.
   Kwa kweli hamu yangu ilikuwa ni kuona UVCCM ikiachana na mtindo wa sasa wa kuishia kwenye matamko na maandamano ya kuunga mkono hotuba na kwenda mbali zaidi kujiuliza kwa nini licha ya serikali kutenga pesa nyingi kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kuliko nchi nyingi za Afrika mashariki na kati, migogoro vyuoni haiishi? Nilidhani wangetafiti na kupendekeza kuhusu namna bora zaidi ya kudhibiti mamilioni yanayoishia mikononi mwa baadhi ya wahasibu wasio watiifu vyuoni na baadhi ya wahujumu uchumi pale bodi ya mikopo wanaojichotea mamilioni ya walipakodi yaliyotengwa kusomesha watoto wa walalahoi.
   
    Nilidhani badala ya kuendelea kulumbana na kukashifiana kwenye mitandao ya kijamii, UVCCM wangeenda vijijini kama walivyofanya USARF na TYL na kujionea wenyewe jinsi  vijana wenzetu wakulima kule Tandahimba, Newala, Pwani, Masasi, Tunduru na kwingineko Tanzania wanavyokatishwa tamaa kwa kutolipwa malipo ya korosho kwa miezi kadhaa na kucheleweshewa pembejeo za kilimo kwa sababu ya ufisadi wa wafanyabiashara wachache kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya.
    Badala ya kuishia kupongeza ujenzi wa maelfu ya madarasa ya shule za kata, ningefurahi kama wana UVCCM wangeenda mbali zaidi na kutawanyika Tanzania nzima ili kujionea madhila wanayokumbanayo wanafunzi wa shule za kata zisizo na walimu, vitabu na maabara! Kisha baada ya hapo watafakari hatma ya mfumo wetu wa elimu na jinsi ubidhaishaji wa elimu tangu ngazi ya elimu ya elimu ya awali unavyozalisha pengo la kutisha baina ya walalaheri na walalahoi katika uliberali mamboleo.
   Hata kwa upande wa wapinzani, nilidhani kina John Heche na makomredi wengine wa BAVICHA wangeacha  kupoteza muda wao kujibu matamko ya kina John Magale Shibuda na wengineo ndani ya CHADEMA wanaotangaza nia ya kuwania urais 2015 kupitia CHADEMA na badala yake kujibidiisha kujenga mapinduzi ya kifikra kwa vijana wenzao.
   Kama alivyowahi kutuasa Dk.Kitila Mkumbo, nadhani huu ni wakati muafaka kwa BAVICHA, UVCCM na vijana kwenye vyama vingine vya siasa ‘’kubalehe kisiasa’’ kwa kuacha siasa za kitoto na kujibidiisha kwenye mambo ya msingi yatakayoleta tija kwa vijana wenzao na kuchochea mustakabali wa taifa. Ni wakati muafaka wa kuonyesha ujana wa fikra: fikra za kimapinduzi.
             Fanya tafakuri ya kina kisha chukua hatua!
Simu: 0653619906     Barua pepe: adoado75@hotmail.com
Makala hii ilichapwa kwa mala ya kwanza kwenye gazeti la RAI toleo na.982.

1 comment:

oscar mfinanga said...

well said kijana..UVCCM inapaswa kuyatilia maanani maoni haya ili kurejesha makali ya enzi za TYL

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...