SERIKALI YA KENYA:
imesema inazifanyia kazi taarifa za raia wake kukamatwa na kufikishwa
kortini nchini kwa tuhuma za kumteka na kufanya jaribio la kumuua
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka.
Hatua
hiyo imekuja siku moja baada ya Jeshi la Polisi kutangaza kukamatwa na
kufikishwa mahakamani kwa raia wa Kenya, Joshua Mulundi anayetuhumiwa
kuhusika na tukio la kumteka, kumpiga na kumtupa Dk Ulimboka katika
Pori la Akiba la Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam hivi
karibuni.
Balozi
wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso, alisema kwa njia ya simu jijini Dar es
Salaam jana kuwa Serikali yake itachunguza uraia na tuhuma
zinazomkabili mtu huyo ili kubaini ukweli.
“Ndiyo
kwanza nimewasili kutoka nje ya nchi…, nitafuatilia kwa makini kupata
taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo sahihi na mamlaka husika za hapa
Tanzania na Kenya ili kupata taarifa ya kweli,” alisema Balozi Mutiso na
kuongeza: “Siwezi kueleza zaidi kwa sasa kwani itakuwa naeleza uvumi.”
MAT wadai kutoridhishwa
Wakati
Balozi wa Kenya akisema hayo, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT),
kimeelezea kutoridhishwa na hatua hiyo kikisisitiza msimamo wake wa
kutaka kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi kwa lengo la kuwabaini
wahusika na kuchukuliwa hatua stahiki.
MAT
pia imesema kwamba, inaendelea na mpango wake wa kuandamana,
ikibainisha kuwa kesho itawasilisha barua ya kuomba kibali cha kufanya
maandamano ya amani Polisi.
Imefafanua
kuwa malengo ya maandamano hayo yaliyopigwa 'stop' na polisi kwa kile
walichoeleza ni sababu mbalimbali za kiusalama na kwamba, madai mengi ya
madaktari yamefanyiwa kazi na Serikali.
"Nisingependa
kuingilia suala la kipolisi kwa ujumla wake, lakini moja ya madai yetu
ni kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza tukio la kutekwa, kupigwa na
kutupwa katika Msitu wa Pande kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk
Ulimboka," Katibu Mkuu wa (MAT) Dk Rodrick Kabangila aliliambia
Mwananchi Jumapili jana.
TUCTA nao wamo
Katika
hatua nyingine, Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (Tucta)
limelipongeza Jeshi la Polisi kwa kumkamata mtu anayedaiwa kumteka na
kumpiga kiongozi wa mgomo wa madaktari, Dk Steven Ulimboka.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema
kuwa, hatua ya kumkamata mtuhumiwa huyo inaleta matumaini ya kuwabaini
watu wengine waliohusika na vitendo hivyo, jambo ambalo linaweza
kurahisisha uchunguzi.
Alisema
kutokana na hali hiyo, jeshi hilo linatakiwa kuendelea na uchunguzi ili
waweze kuwabaini wahusika wengine na kubaini ukweli kuhusu tukio hilo
ambalo limesababisha kutokea kwa hisia tofauti katika jamii.
“Tunaliomba
Jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi ili waweze kuwabaini watuhumiwa
wengine na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema Mgaya.
Mkenya kukamatwa
Joshua
Mulundi, ambaye anatuhumiwa kumteka na kumtesa Dk Ulimboka alikamatwa
na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini
Dar es Salaam juzi alasiri na kusomewa mashtaka mawili na Wakili wa
Serikali, Ladslaus Komanya.
Wakili
Komanya alidai mahakamani hapo kuwa, Mulundi ambaye makazi yake ni
Murang'a nchini Kenya mnamo Juni 26, mwaka huu akiwa eneo la Leaders
Club alimteka Dk Ulimboka.
Hata hivyo, kumetokea utata wa jina, umri wake na makazi ya mtuhumiwa huyo.
Wakati
hati ya mashtaka mahakamani inasema ni Joshua Mulundi mwenye umri wa
miaka 21, mkazi wa Murang’a nchini Kenya, taarifa ya Jeshi la Polisi
imesema anaitwa Joshua Mahindi mwenye miaka 31 na mkazi wa Namanga
nchini Kenya.
Katika
shtaka la pili, Wakili Komanya alidai kuwa tarehe hiyohiyo mshtakiwa
alifanya jaribio la kumsababishia kifo Dk Ulimboka kwa kumpiga katika
eneo la Msitu wa Pande eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam, kinyume cha
sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo akidai kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo siyo sahihi.
Hakimu
Mkazi, Agnes Mchome alimwambia kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, isipokuwa
Mahakama Kuu pekee.
Afya ya Dk Ulimboka yazidi kuimarika
Akizungumzia
hali ya Afya ya Dk Ulimboka anayeendelea na matibabu nchini Afrika
Kusini, Katibu Mkuu huyo wa MAT alisema kuwa, Mwenyekiti huyo wa Jumuiya
ya Madaktari Tanzania anaendelea vizuri na sasa ameanza kufanya mazoezi
ya kutembea.
"Taarifa
tulizonazo sasa ni kwamba, hali ya Dk Ulimboka inaendelea vizuri.
Ameanza kufanya mazoezi ya kutembea mwenyewe, anakula na pia anaweza
kuzungumza vizuri. Amekuwa akifanya mawasiliano yeye mwenyewe na
madaktari wenzake wa hapa nchini ingawa bado kuna matibabu anayoendelea
nayo," alisema Dk Kabangila.
Mmoja
wa Madaktari wa karibu wa Dk Ulimboka aliyepo nchini, alisema
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania amewatumia ujumbe wa
kuwashukuru wanataaluma wenzake na Watanzania wote waliomchangia na
kumwezesha kupata matibabu nchini humo.
Hata
hivyo alisema kuwa, Dk Ulimboka ameomba suala la tukio lake la kutekwa
na kuumizwa lisiwe hoja ya kujadili, badala yake madaktari na wananchi
wote wajielekeze kudai haki zao, ambazo Serikali haijazipa kipaumbele.
Dk
Ulimboka alisafirishwa nje ya nchi Juni 30 kwa ajili ya matibabu
kufuatia jopo la madaktari lililokuwa likimtibu likiongozwa na Profesa
Joseph Kahamba kudai afya yake imebadilika ghafla na pia angestahili
kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya vipimo na matibabu zaidi ambayo
hayapatikani hapa nchini.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment