FOLLOWERS

Sunday, July 29, 2012

DR ULIMBOKA KULITEKA BUNGE

SAKATA la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, na mgogoro wa madaktari ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuliteka Bunge leo.
Suala hilo licha ya kuzuia kujadiliwa bungeni kwa madai kuwa kesi yake iko mahakamani, idadi kubwa ya wabunge imeonyesha kiu ya kulijadili.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Husein Mwinyi, leo anatarajia kuwasilisha hotuba ya bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Dk. Mwinyi na Naibu wake Dk. Rashid Seif waliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuongoza wizara hiyo miezi miwili iliyopita wakichukua nafasi za Dk. Haji Mponda na Dk. Lucy Nkya, walioondolewa kwa madai ya kushindwa kuwajibika ipasavyo.
Mponda na Nkya, walidaiwa kushindwa kushughulikia matatizo yanayoikabili sekta ya afya hivyo kuwafanya madaktari wafanye mgomo mwanzoni mwa mwaka huu.
Katika madai yao madaktari walikuwa wakitaka watendaji wakuu wa wizara hiyo waondolewe kwenye nafasi zao ndipo wazungumze na serikali.
Sharti hilo lilitekelezwa na serikali ambapo iliwaondoa madarakani Katibu Mkuu, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa, huku uchunguzi dhidi ya tuhuma zao ukiendelea mpaka sasa.
Waziri Mwinyi atakuwa na kibarua kizito kwa wabunge kwani mbali na kutakiwa kueleza hatua zilizochukuliwa kwa watuhumiwa hao, pia Bunge litapaswa kuelezwa hatua zilizofikiwa na serikali katika kutatua mgogoro wa madaktari hasa utekelezaji wa madai yao 10 yaliyosababisha wagome mara tatu na kuleta madhara kwa wagonjwa.
Sakata la Dk. Ulimboka lilitokea usiku wa Juni 28, siku mbili baada ya madaktari kuanza mgomo jambo lililowafanya baadhi ya watu kuvihusisha vyombo vya dola.
Hata hivyo viongozi mbalimbali akiwemo Rais Jakaya Kikwete walikana serikali kuhusika nalo.
Wabunge wang’ang’ania
Licha ya viongozi wa Bunge kudai suala hilo liko mahakamani na mtu mmoja ameshakamatwa, wabunge wengi wameonekana kupinga jambo hilo kwa madai kuna hila ya kuwazuia kulijadili.
Miongoni mwa wabunge wanaoonekana kuwa na kiu ya kutaka kulizungumzia suala la Dk. Ulimboka ni mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, ambaye wiki iliyopita alisema sinema ya Dk. Ulimboka haijaeleweka katika jamii.
Kauli ya mbunge huyo ilikuwa kijembe kwa Jeshi la Polisi ambalo lilitangaza kumkamata mtuhumiwa wa tukio hilo na kumfikisha mahakamani.
Suala hilo huenda likazua malumbano makali bungeni hasa kutokana na hatua ya serikali kuwafutia leseni madaktari walioshiriki kwenye mgomo hivi karibuni.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili mjini hapa jana, walisema kuwa wanataka serikali itoe ufafanuzi ni kwa nini imewafutia leseni madaktari wanafunzi kwa vitendo “interns” wakati ikielewa fika kuwa sekta hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa watumishi.
Ripoti ya mgomo yatakiwa
Mbunge Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amewataka wadau mbalimbali wa sekta ya afya nchini kuungana kutaka ripoti ya Kamati ya Bunge Huduma za Jamii iliyoshughukia suala la mgomo wa madaktari iwasilishwe bungeni na itumike kama hadidu rejea wakati wa kujadili suala zima la mgomo wa madaktari.
Mnyika alisema maelezo yaliyotolewa bungeni na Naibu Spika, Job Ndugai, kuwa taarifa hiyo iliwasilishwa bungeni hayakuwa ya kweli kwa kuwa wabunge hawajapewa nakala ya taarifa hiyo na kwamba bado inaendelea kufanywa siri.
Alisema tabia ya viongozi wa Bunge kuzuia mijadala mbali mbali kwa kigezo kuwa kesi ziko mahakamani ni kutowatendea wananchi haki.
“Kesho na keshokutwa Bunge litajadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, kwa zaidi ya miezi mitatu Bunge limekuwa likizuiwa kutumia haki, uhuru na madaraka yake kwa mujibu wa ibara za 63 na 100 za Katiba ya nchi kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kuhusu hali ya sekta ya afya nchini na migogoro kati ya serikali na madaktari.”
“Bunge linapaswa kutumia madaraka yake vema kujadili mustakabali wa maisha ya Watanzania ili iweze kujua chanzo cha mgogoro ulioendelea kati ya serikali na madaktari ili iweze kutoa ushauri wa namna ya kuzuia wakati mwingine isijirudie.” na Edson Kamukara.......TANZANIA DAIMA

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...