Makamu wa raisi wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dk Mohamed Ghalib Bilal |
Katika
mazungumzo hayo, Makamu wa Rais alielezea kufurahishwa kwake na
uhusiano mzuri ulipo kati ya Tanzania na Marekani na pia akafafanua kuwa
Marekani imekuwa ni rafiki wa kweli kwa Tanzania kutokana na michango
yake ya maendeleo iliyopo nchini.
Dk.
Bilal aliueleza ujumbe huo uliomtembelea Ikulu leo kuwa, serikali ya
Tanzania inaona faraja kushirikiana na Marekani na kueleza kuwa mchango
wa Marekani kwa Tanzania ni mkubwa na Tanzania inakaribisha uhusiano
zaidi hasa katika sekta za Kilimo na Nishati.
“Waziri
wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton alikuja hapa, akatupa
matumaini ya kuondokana na tatizo la umeme. Tayari wapo wawekezaji wengi
kutoka Marekani ambao wana nia ya kuwekeza katika nishati,” alisema
Makamu wa Rais.
Kwa
upande wake Seneta Coons alimueleza Makamu wa Rais kuwa, jimboni kwake
Delaware wapo wakulima wengi ambao wangependa kuja nchini kuwekeza
katika kilimo. Pia alifafanua namna Tanzania inavyoweza kuzalisha umeme
wa ‘Geothermal’ kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka Marekani.
Seneta
Coons amewahi kuishi Afrika Mashariki katika miaka 25 iliyopita
sambamba na mambo mengine ni seneta mwenye uwezo wa kuzungumza
Kiswahili. Seneta huyu anatokea katika eneo la uwakilishi ambalo pia
anatokea Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden na amepata nafasi ya
Useneta baada ya Biden kuachia kiti hicho.
Hata
hivyo, Makamu wa Rais alisema pamoja na juhudi zote za kuhifadhi
mazingira na viumbe hai bado Tanzania inakabiliwa na matatizo ya
ujangiri, uvuvi haramu, magugu maji kufunika kabisa baadhi ya maziwa na
mito.
Alipotakiwa
kutoa maoni yake kuhusu vurugu za hivi karibuni za Zanzibar Dkt. Bilal
alisema haoni sababu yoyote ile kwa watu wanaohubiri kuwa hawataki
Muungano kisha wakakimbilia kuchoma makanisa na kuvunja baa. Alisema
kuwa, kikundi hiki kimekuwepo siku nyingi na kinatumia kivuli cha dini
katika kufanya siasa. Vile vile Makamu wa Rais alieleza kuwa, Zanzibar
ni kisiwa kidogo na kupitia Muungano wananchi wa Zanzibar wananufaika na
kamwe serikali ya awamu ya nne haiwezi kuvumilia kuona watu wachache
wenye agenda iliyojificha wakiharibu jambo bora kabisa lililofanyiwa
kazi kwa zaidi ya miaka 48.
“Kila
ukipita mikoani unakutana na Wazanzibar wanaishi. Kupitia Muungano
tumefungua fursa nyingi. Sioni sababu ya watu kuibuka sasa kuupinga
Muungano na tena kwa kufanya fujo. Tutaendelea kudhibiti hali hii na
kuhakikisha kuwa amani inabakia katika nchi yetu,” alisema.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment