MWANACHAMA
maarufu wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Azim Dewji amezishauri
klabu kubwa za Simba na Yanga nchini kuanza kuutumia mtaji wa wanachama
wake kujijenga kiuchumi, na kuepuka kuwa tegemezi.
Dewji, ambaye ni mmoja wa wafanyabiashatra maarufu nchini, alisema
kwamba kila klabu ina zaidi ya wafuasi milioni 15 nchi nzima, lakini
ajabu klabu zinaendelea kuwa ombaomba.
“Huu ni mtaji mkubwa sana, lakini utashangaa klabu haina hata asilimia
moja (150,000) ya wanachama wa kweli. Kila siku utasikia wanachama 3,000
hadi 6,000. Kiongozi wa klabu anachaguliwa na wanachama wasiofika
2,000?
“Jamani, kwa klabu inayoshabikiwa na mamilioni ya watu inashindwaje
kujijenga kiuchumi kwa kuwatumia mashabiki wake waliozagaa kila kona ya
nchi? Jiulize, kama angalau hao watu 150,000 tu wakilipa ada ya mwaka ya
12,000 ambayo hata hivyo bado ni ndogo, si wanaweza kuvuna sh bilioni 1.8 kwa mwaka, hizi si fedha nyingi?
“Kuna haja ya kufanya mapinduzi ya kweli, badala ya kufikiria kuifunga
Simba au Yanga na kutwaa ubingwa wa Bara. Timu yenye uchumi imara, ndiyo
inayokuwa na jeuri ya kuwa na kikosi imara na hivyo kufanya vizuri
zaidi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Huko ndiko tunakopaswa
kwenda,” alisisitiza.
Aidha, Dewji ameipongeza Yanga kwa kufanikiwa kutetea ubingwa wa
michuano ya Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame
mwishoni mwa wiki, baada ya kuizamisha Azam kwa mabao 2-0 katika mchezo
mkali wa fainali kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Dewji, aliyewahi kuifadhili Simba na kuifikisha fainali za Kombe la CAF
mwaka 1993, alisema pamoja na yeye kuwa `Simba Damu’, ana kila sababu
za kuimwagia sifa Yanga kwa kuwa imezika haraka matatizo yake na
kugeukia kusaka maendeleo.
“Huwezi kuamini kama Yanga iliyopigwa 5-0 na kuibua tafrani nzito
Jangwani, ndiyo hii ya leo. Wameikubali hali na kubadilika ndani ya muda
mfupi sana. Wana amani na matunda yake yameonekana ingawa walikuwa na
kipindi kifupi cha kusuka timu na kurejesha mshikamano ndani ya klabu.
“Naipongeza Yanga na hasa Mwenyekiti wake, Yussuf Manji kwa sababu
naamini imani ya wanachama juu yake ndiyo iliyorekebisha hali haraka,
naye kama kiongozi kuhakikisha usajili makini unafanyika, kocha
anapatikana na uzalendo ndani ya Yanga unarejea,” alisema Dewji.
Aliongeza kuwa, pamoja na matunda ya haraka ya uongozi wa Manji,
wana-Yanga wanapaswa kumpa ushirikiano ili kuiondoa Yanga katika
utegemezi wa miaka nenda rudi, huku akisisitiza Manji hatabaki Yanga
milele.
“Wana kiongozi shupavu, sasa washirikiane naye kuujenga uchumi wa
klabu. Haya mambo ya kutegemea mtu kila kukicha si mazuri. Na hili si
kwa Yanga tu, hata Simba na klabu nyingine zinapaswa kujikita katika
kujijenga kiuchumi ili ziwe na jeuri ya fedha bila ya kutegemea mifuko
ya mwanachama mmoja mmoja,” alisema. |
No comments:
Post a Comment