Alama kuu ya 'kanisa' la kilimwengu la
kishetani
Maandiko yanasema kwamba: Nao
wanaoufuatia uhai wangu hutega mitego; nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya;
na kufikiri hila mchana kutwa. (Zab. 38:12).
Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba; wametandika wavu kando ya njia;
wameniwekea matanzi. (Zab. 140:5).
Pia imeandikwa: Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake
bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye
miongoni mwao, hushuka na kuingia humo. (Isaya 5:14).
Shetani halali. Usiku na mchana, karne hadi karne yuko katika hekaheka za
kuwakusanya wanadamu ili kwenda nao kwenye jehanamu ya moto.
Zipo njia maelfu za kutekeleza malengo yake hayo. Lakini msingi wa hayo yote,
ni kumtumia mwanadamu mwenyewe. Wako wanadamu wengi leo ambao ni waabudu
shetani na wanajua kabisa; na wameamua toka mioyoni mwao kwamba wao watakuwa ni
raia wa kuzimu.
Wako wengine, walio kundi kubwa zaidi, ambao wameingizwa kwenye uraia wa kuzimu
bila wao kujua. Lakini ukiwauliza kama wao ni raia wa kuzimu watakataa
katakata. Hata hivyo, ukweli ni kwamba ni washirika wa huko kwa asilimia mia
moja.
Sitaongelea kila njia anayotumia shetani kuwanasa wanadamu, lakini nitapenda
tuangalie njia ambayo si wengi wanaweza hata kuidhania.
Biblia inamtaja ibilisi kama kerubi afunikaye (Ezekieli 28:14). Kwa hiyo yeye
ni fundi wa kufunika mambo na kuyafanya yaonekane ya kawaida au ya kuvutia
kumbe ni mitego ya mauti.
Ulimwengu wa giza unatumia sana alama (symbolism). Ziko alama mbalimbali za
kishetani ambazo zimeingizwa sehemu nyingi mno kiasi kwamba si rahisi
kuzigundua maana sasa zinaonekana kama ni mambo ya kawaida tu. Zinaweza kuwa
kwenye bidhaa tunazotumia kila siku kama vile mavazi, mikufu, bangili, pete,
hereni, muziki, sinema, video games, nk.
Shetani hafanyi mambo yake kwa haraka. Amepanga mambo yake kwa miaka mingi na
kuyaingiza polepole kiasi kwamba muda si mrefu, dunia itashuhudia mlipuko wa
kazi zake za uharibifu. Hata sasa uovu umeshashika kasi kubwa; na bado unazidi
kufunguka zaidi na zaidi; maana kuzimu kumeongeza tamaa.
Tambua kwamba waabudu shetani wana ajenda kubwa moja, nayo ni kufika mahali
ambapo watauteka ulimwengu wote. Sasa ili kutekeleza malengo hayo, wanahitaji
pia fedha. Njia mojawapo ya kupata fedha ni kuuza bidhaa mbalimbali, zikiwamo
za mapambo. Lakini bidhaa hizo zinakuwa na lengo jingine zaidi ya lile la
kuleta fedha. Nalo ni kuyatuma mashetani ulimwenguni kote ili kukamata akili na
fahamu za watu na kuziweka mbali na Mungu wa kweli. Kwa hiyo, mara
zinapotengenezwa, kabla ya kusambazwa, wanasema kuwa ‘wanazibariki.’ Na ni wazi
kuwa shetani anapobariki kitu ina maana kuwa anakilaani.
Kwa hiyo, unapokuwa nazo, huo ni mlango tosha wa shetani na laana zake kuingia
maishani mwako na kuanza kukuongoza katika njia yake, hata kama wewe hujui.
Zifuatazo ni baadhi tu ya alama ambazo inawezekana umeshaziona au hata kuzivaa;
lakini ni alama za kishetani ambazo kimsingi zinakuwa zimepandiwa au kunuiziwa
mapepo.
|
No comments:
Post a Comment