FOLLOWERS

Monday, July 2, 2012

AJIRA MPYA 56678 KUONGEZEKA NA MISHAHARA KUPANDISHWA

SERIKALI imetangaza nyongeza ndogo ya mishahara ya kima cha chini kwa watumishi wa umma, ambacho hakikuwekwa wazi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani.
Akisoma hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Waziri Kombani alisema katika mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali inatarajia kutumia sh trilioni 3.7 kugharimia malipo ya mishahara, upandishwaji wa vyeo na kulipia malimbikizo na mapunjo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala na Taasisi za umma.
Alisema Serikali itarekebisha mishahara ya watumishi wake kwa kuzingatia uwezo wa bajeti na makubaliano yaliyofikiwa na Baraza la Majadilino la pamoja katika Utumishi wa Umma lililoundwa kwa mujibu wa sheria ya majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma.
Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, aliposoma bajeti ya serikali kwa mwaka 2012/13 Juni 14 mwaka huu, hakuzungumzia moja kwa moja kuhusu kupanda kwa mishahara ya watumishi wa umma, lakini alisema kodi ya mapato kwa wafanyakazi itaanza kukatwa kwa mtu anayeanza na mshahara wa sh 171,000 kutoka sh 135,000.
Kwa mujibu wa Waziri Kombani, kiasi cha sh trilioni 3.7 ukilinganisha na sh trilioni 3.2 za mwaka wa fedha wa 2011/12 kimeongezeka kwa sh bilioni 510, sawa na asilimia 15.6.
“Kwa hiyo wale wenye madai mbalimbali, watalipwa madai yao,” alisema Kombani.
Kwa mujibu wa Kombani, katika hatua ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, serikali itaendelea kutekeleza sera ya malipo ya mshahara na motisha katika utumishi wa umma kwa kuzingatia mkakati wake wa utekelezaji ambapo inatarajiwa kuwa kazi kubwa katika mwaka wa huu wa fedha ni kuandaa mwongozo wa kutoa motisha kwa watumishi wanaofanya kazi katika mazingira magumu.
“Aidha serikali itafanya utafiti kuhusu mishahara na maslahi ya wafanyakazi baina ya sekta binafsi na serikali kwa lengo la kuwianisha na kuoanisha mishahara ya watumishi wa umma,” alisema.
Akizungumzia ajira mpya katika mwaka huu wa fedha, Waziri Kombani alisema Serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 56,678 na kipaumbele kitakuwa katika sekta ya elimu, afya, kilimo na mifugo. Hata hivyo nafasi hizi hazijumuishi nafasi mpya za baadhi ya vyombo vya dola.
Aidha Serikali inatarajia kuwapandisha vyeo watumishi 44,419 wa kada mbalimbali.
Kuhusu kuwahudumia viongozi wastaafu, Waziri Kombani alisema Serikali itaendelea kuwagharimia viongozi hao kwa mujibu wa sheria ya mafao ya viongozi.
“Aidha ujenzi wa msingi wa kituo cha kuwaenzi waasisi wa taifa, Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume utaanza katika mwaka huu wa fedha,” alisema.
Waziri Kombani aliomba kuidhinishiwa sh bilioni 9.14 kwa ajili ya ofisi ya Rais kama matumizi ya kawaida, sh bilioni 267.4, kwa ajili ya sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, sh bilioni 217 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh bilioni 50 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Waziri Kombani aliomba kuidhinishiwa sh sh bilioni 42.4, kati ya hizo sh bilioni 22. 4 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo wakati sh bilioni 20 ni matumizi ya kawaida.
Sekretarieti ya maadili ya umma, iliombewa sh bilioni 7.3 ambapo sh bilioni 5.9 ni za matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo imetengewa sh bilioni 1.4.
Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma imeombewa sh bilioni 2.4 ambazo zote ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida wakati tume ya utumishi wa umma iliomba kuidhinishiwa sh bilioni 7.9.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...