PROFESA ISSA SHIVJI |
BARUA NDEFUKWA KOMREDIPROFESA ISSAGULAMHUSEIN SHIVJI (2).
Kutoka kwa Ado Shaibu,
S.L.P kijiji cha Namasakata,
Wilaya ya Tunduru.
Kwako Komredi Profesa Issa Shivji,Shikamoo!
Ni matumaini yangu kwamba waraka wangu wa kwanza ulikufikia. Kabla ya kuendelea
na barua yetu ya leo, ngoja nikupe mchapo kidogo. Majuzi nilikuwa kijijini
kwetu Namasakata. Usiku niliwakusanya vijana wenzangu nakuwasimulia habari
zako.
Nilipowasimulia ile habari ya wewe kuwakatalia
mwaliko Maprofesa wenzakowa ng’ambo waliotaka ukatoe mada kwenye chuo chao huko
ulaya, vijana wale wa Namasakata waliduwaa sana. Niliwaeleza msimamo wako wa
kugomea mwaliko ule ‘’mnono’’ ili kuonesha mwitiko wako kwa uvamizi wa kimabavu
wa Marekani nchini Iraq. Nakumbuka ulivyotueleza wazi wakati ule kwamba ile
haikuwa vita dhidi ya silaha za maangamizi kama walivyodai mabingwa wa
propaganda za kivita, bali ilikuwa vita ya kugombea mafuta. Miaka michache
baadaye, Rais George Bush alikili hadharani kwamba uvamizi wa Iraq ulifanywa
kimakosa. Hongera sana kwa msimamo ule. Zama hizi wasomi wenye msimamo ni
wachache sana.
Wanakijiji wa Namasakata
wanakukaribisha sana kijijini kwetu ujionee mwenyewe jinsi wanavyoyumbishwa na
sera za uliberali mamboleo zililozalisha soko holela badala ya soko huria. Kwa
mfano, msimu wakorosho wa mwaka huu wanakijiji wa Namasakata wamekaa kwa miezi
zaidi ya minne bila kulipwa pesa zao za korosho. Naambiwa hali ni hiyohiyo kwa
wakulima wa Tandahimba, Newala, Masasi, Pwani na mikoa yote ya kusini.
Sasa turudi kwenye barua yangu. Kama
nilivyokueleza awali kwenye barua yangu ya kwanza, waraka wangu ni mjumuiko wa
maswali kuhusu taifa letu. Maswali haya yananisumbua sana; yananichoma ndani
kwa ndani kwa kukosa majibu. Nimekuwa nikijiuliza maswali haya kila muda:
najiuliza mchana na usiku. Sasa naomba nianze maswali yanguna ni matumaini
yangu kwamba utanipatia majibu mujarabu.
Swali langu la kwanza linahusu
itikadi ya ujamaa na kujitegemea, hususani Azimio la Arusha.Profesa kwa miaka
nenda rudi unahubiri Azimio la Arusha.Ingekuwa kwenye muktadha wa ulimwengu wa
kiroho ningekuita nabii wa Azimio la Arusha!Ni adimu kwa wewe kuhutubu eneo
fulani bila kulitaja Azimio la Arusha.
Swali langu ni kutaka kujua kwa nini
unaendelea kulishabikia Azimio katika zama hizi. Umesahau kauli ya mwalimu
Nyerere mbele ya wanahabari kwamba
inahitaji roho ngumu mithili ya ile ya mwendewazimu kulizungumzia Azimio katika
zama za leo? Si bado unakumbuka maneno ya Mzee Ruksa wakati akiling’oa azimio
la Arusha na kusimika Azimio la Zanzibar kwamba’’kila kitabu na zama zake’’?Majuzi
nilistuka nilipomsikia Mzee Ruksa na Mzee Cleopa Msuya wakijivua lawama ya
kuliua na kulizika azimio la Arusha na kudai waliolivunja ni ‘’viongozi
maharamia’’ wasiomuogopa Mungu.
Hiyo inaweza kuwa mifano ya zamani
kidogo.Nina imani unakumbuka mfanowa karibuni pale Amiri Jeshi Mkuu wa sasa alipohojiwa
ughaibuni kuhusu Azimio la Arusha na kuweka wazi kwamba ‘’ujamaa hausawili
mazingira yetu ya sasa’’?
Majuzi wakati tunamuaga Profesa Goran Hyden pale ukumbi wa Nkurumah,
kuna vijana walipinga fikra za usasa za uliberali mamboleo na kukumbushia
misingi ya Azimio la Arusha; misingi ya utu na usawa. Nakumbuka Barozi Mwapachu
aliwang’akia vijana wale kwamba wasiendelee na fikra za kijamaa
zisizotekelezeka katika dunia ya leo na aliwaasa wahadhiri wa UDSM waachane na
mtindo wa upandikizaji wa fikra za ki-maksi kwa wanafunzi: fikra muflisi
zilizofeli!
Nini lengo lako kulishadidia Azimio la Arusha wakati ‘’wenye dola’’ na
wanazuoni wa kimamboleo wanalipondaponda na kuweka wazi kwamba kwenye dunia ya
leo ya utandawazi, kufungua milango wazi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa
ndani na nje ni suala lisilo na mbadala?
Nimesoma sehemu fulani(ukimnukuu Mwalimu
Nyerere) kwamba misingi ya Azimio la Arusha itarudi(hasa misingi yake ya usawa
na utu) na kwamba dalili za wazi za ‘’ufufuo’’ wa Azimio la Arusha zimeanza
kuonekana.
Unamaanisha una matumaini kwamba
Azimio litarudi tena Tanzania?kwamba viongozi wetu hawatomiliki tena hisa
kwenye kampuni za kibwanyenye?wasipokee mishahara miwili au zaidi?wasiwe
wajumbe wa bodi za mashirika na makampuni ya kibeberu?Unamaanisha tutarudisha
tena vijiji vya ujamaa na kutaifisha makampuni?Unamaanisha nini unaposema
azimio linarudi?
Najua kama azimio litarudi,halitowakataza
tena viongozi wetu wafanyabiashara kufanya biashara ya kupangisha nyumba.Na
sasa tunaambiwa wana majumba mpaka Arabuni na Ulaya.Nina uhakika azimio jipya
litaporudi halitoweka sharti hilo litalowakosesha raha viongozi wetu watukufu.Hata
Mzee kingunge alisema kwa hili la kuwanyima viongozi wetu kufanya biashara ya
kupangisha nyumba walipotoka!(rejea mazungumzo yako na mzee Ngombale Mwilu
kwenye jarida la Chemichem toleo la
pili)
Halafu kama azimio linarudi;ni nani
analirudisha?Mmetufundisha darasani kwamba ujamaa wa kiafrika,tofauti na ule wa
kisayansi wa karl Marx na Fredrick Engels,uliletwa na viongozi waliopigania
uhuru na sio vuguvugu la kimapinduzi la wafanyakazi na wakulima.Uliletwa na
kina Nyerere,Nkurumah na Tom mboya.Ni viongozi gani wataolirudisha azimio hivi
leo?Ni viongozi hawahawa wanaopokea posho mbili bungeni kwa kazi ileile?Ni
viongozi hawahawa wanaopayuka majukwaani na kulalama kuhusu matumizi mabaya ya serikali
wakati wao wenyewe wakiendesha magari ya kifahari ya serikali na kula mlungula?
Kwamba viongozi hawa wanaopokea posho namishahara mitatu na zaidi kwa
kazi ileile watakaa bungeni na kupitisha sheria hata yenye harufu tu ya Azimio
la Arusha;Sheria ya kuwabana wasijilimbikizie ukwasi wakati masikini wa kijijinikwetu
Namasakata na kwingineko Tanzania wakitaabika kwa ufukara?Thubutu!kwamba
viongozi hawa watapata ufunuo mpya na kuwachukulia ‘’wasakatonge’’Kuwa ni
binadamu wenye haki na wanastahili usawa?
Au sijakuelewa Profesa?Pengine
unamaanisha watu wenyewe wataridusha Azimio.Kwamba umma wenyewewa wanyonge
utapigania usawa na kushiriki kujenga ujamaa?Lakini profesa si unajua nguvu ya
dola? Ni naniwa kuanzisha vuguvugu la wanyonge katika mazingira ya sasa? Ni
nani atakuwa Lenin na Trosky wetu; Mao Tse Tung wetu; Fidel Castro na Che
Guavala Wetu? Ni nani wa kuwaongoza wanyonge kwenda kwenye usawa na haki?
Si umetufundisha mwenyewe kwamba
vuguvugu la wafanyakazi lilianza kuchipua Tanzania tangu miaka ya sabini?(Rejea
kazi yako ya Working class in Tanzaniana
Silent Class Struggle, utafiti wako
wa enzi zile ukiwa kijana ).Nani alizima vuguvugu lile la wanyonge?watashindwa
nini kuzima vuguvugu lolote la wanyonge sasa? Au umesahau mkong’oto
waliokumbana nao wamasai wa Loriondo?Madam
Shamsa Mwangunga alisema waliofurushwa ni wakenya! Kwa Kweli nilipomsikia tumbo
langu liliunguruma kwa hasira.
Majuzi nimebahatika kupitia tamko la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania(MVIWATA)
walilolitoa pale Morogoro kuadhimisha miaka hamsini ya uhuru wetu.
Naomba nikukumbushe waliyoyasema wakulima wale: kwanza waliweka wazi
sikitiko lao kuhusu kusalitiwa kwa misingi ya Azimio la Arusha na hivyo basi
kukuza pengo baina ya walalahoi na walalaheri. Pia waliweka wazi kwamba
wanapinga kwa nguvu zote ukandamizaji na unyonyaji wanaofanyiwa wakulima wa
Tanzania na wakoloni mamboleo kwa kushirikiana na makuwadi wa ubeberu.
Nilihamasika sananiliposoma kwamba wameamua kuchukua hatua ya kukuza umoja wa
wakulima wanaonyonywa na kukandamizwa.
Unajua suluhu waliyoisema? Kwamba
watawanyima kura wanasiasa uchwara wote na pia watapiga kelele dhidi ya dhuluma
ya wakulima. Ninachojiuliza ni kama wakulima hawa wanalenga kulirudisha Azimio
la Arusha au wanachotaka ni maslahibora ndani ya ubepari? Kama wanataka Azimio,
watalirudishaje? Katika vyama vyetu, ni nani watayempa kura ambaye ana ndoto na
nia thabiti ya kulirudisha Azimio la Arusha?
Kuna jambo la msingi nilitaka kusahau.
Profesa, sisi tuliozaliwa zama za rais Mwinyi hatujashuhudia mengi kuhusu
ujamaa. Tumeishia kuusoma ujamaa vitabuni tuna kusimuliwa. Na kama unavyojua,
vitabu vinachanganya kwelikweli! Mupo mulioandika jinsi ujamaa ulivyokuwa mfumo
wa usawa na utu: mmetusimulia jinsi ujamaa ulivyolenga kumkomboa mnyonge kutoka
katika minyororo ya unyonyaji na madhila mengineyo.
Lakini Profesa, wapo wengine, tena
wengi sana wameandika na kusimulia mabaya ya ujamaa. Wapo wanaosema ujamaa
ulitaka kutaifisha kila kitu hadi magenge na vijiduka vya mitaani ambavyo
kimsingi vilipaswa kuendeshwa na watu binafsi. Si unakumbuka ule utani wa
wakenya kwamba ‘’kama unataka vitu vya bure nenda Tanzania ambako watu
wanachangia kila kitu ikiwemo wake zao?’’
Wapo pia wanaokumbushia operesheni
vijiji ya miaka ya sabini na dhahama yake. Wengine wanakwenda mbali zaidi na
kukumbushia jinsi uhaba wa bidhaa muhimu ulivyotamalaki wakati ule wa
ujamaa.Hata rais mkapa alikumbushia baadhi ya madhila haya mulipomuita pale
Nkurumah majuzi. Si unakumbuka alivyounguruma na kumpongeza Mzee Salim Ahmed
Salim kwa uamuzi wake wa ‘’kizalendo’’ wa kufungua mipaka ili kupunguza uhaba
wa bidhaa aliodai uliletwa na sera yetu ya ujamaa na kujitegemea?
Binafsi naomba kutangaza maslahi
kwamba nauhusudu baadhi ya sera za ujamaa.Kwanza neno lenyewe ‘’ujamaa’’
limekaa kiutu.Lakini hii haimaanishi kwamba ujamaa ni msahafu! Ni lazima tujifunze
tulipojikwaa miaka ile ya sabiniili tusidondoke tena. Hili litawezekana kama
tukifanya tafakuri ya kina na kuudurusu ujamaa.
Kama kweli ndoto zako (na za Mwalimu Nyerere)
kuhusu ufufuo wa Azimio la Arusha zitatimia, basi rai yangu ni kwamba katika
huo ujamaa mpya, wanavijiji washirikishwe kikamilifu kabla ya operesheni yeyote
ya vijiji: Programu za maendeleo ziendeshwe kwa kuzingatia sheria na sio kwa
ubabe kama ilivyokuwa miaka ile. Pia serikali isijihusishe nashughuli za
uchuuzi kama enzi zile: Ijihusishe na biashara kubwa kubwa tu. Je pia huoni
mahitaji ya kudurusu miiko yetu ya uongozi ya enzi zile ili iendane na wakati
kama wanavyosema wengi?
Sasa nikuulize swali langu la pili……
6 comments:
kazi nzuri mkuu..je we bado unaamini ujamaa una nafasi katika maisha yetu hivi sasa hasa kwenye dunia yetu ya utandawazi?
ulifanya makosa kulitupa azimio la arusha jumla..baadhi ya tenets za ujamaa kama vile miiko ya uongozi,serikali kuhodhi baadhi ya sekta nyeti,usawa na utu zina mashiko mpaka leo..kwa mawazo yangu, nadhani tunapaswa kudurusu mfumo huu na kuchukua baadhi ya mambo yaliyo na umuhimu kwetu..though i also admit that baadhi ya mambo ya azimio yalifaa zaidi kama vile kukataza viongozi wasipangishe hata nyumba na kununua hata hisa moja yalifaa zaidi wakati ule wa miaka ya themanini kuliko yalivyofaa sasa..
hapo juu i mean (tu)lifanya makosa kuutupa ujamaa kwa ujumla and not (u)lifanya makosa..
kazi nzur but mi siamini kama yupo wa kuturejesha kwenye usawa..watu wabinafsi sana kaka..azimio hawawezi kulipenda sababu liliwakosesha utajiri..hapo unaposema wabunge wetu wanapayuka majukwaani huku wakila mlungula na kuendesha magari ya kifahari unamzungumzia mh zitto?
binafsi mpaka sasa sijaona chama chochote kinachohubiri azimio la arusha..kipo chama cha kulirejesha na kulihifadhi kwa maanisha azimio la arusha kweli? sidhani kama kipo...ikiwa mwalimu nyerere muasisi wa azimio la arusha alishuhudia azimio la arusha likichinjwa na kuzikwa kwa azimio la kisiri siri la zanzibar 1992 na akashindwa kulinusuru pamoja na uzalendo na influence aliyokuwa nayo..nani anaweza kusimama leo kulihubiri azimio la arusha??..."kuzungumzia azimio la arusha inahitaji mtu uwe na akili ya mwendawazimu..julius nyerere"
mkuu gabriel batikwisa, suala la zitto bado ni pre-mature..after all, makala hii niliiandika kitambo kidogo japo kwenye jukwaa hili imewekwa karibuni..but ukweli kwamba viongozi wetu ni wabinafsi hauna shaka..umesahau mbunge wa bahi ana kesi ya kujibu mahakamani kwa sababu ya kula mlungula?
Post a Comment