JOHN MNYIKA: Salamu Za Mshikamano Kuunga Mkono Maandamano Ya Wadau Wa Habari
Kwa niaba ya Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) tukiwa ni sehemu ya
wadau wa sekta ya habari nchini, tunaunga mkono maandamano ya amani
mliyoitisha ya kupinga hatua ya serikali kulifungia gazeti la
MwahaHALISI.
Tunawapongeza wahariri kwa mshikamano wenu katika
kipindi hiki cha majaribu; endeleeni kusimama pamoja, ni umoja wenu ndio
utakaokuwa kinga ya pamoja dhidi mtu au chombo chombo chochote
kinachoingilia uhuru wenu. Mshikamano wenu ni ishara ya kushindwa kwa
mkakati wa ‘wagawe uwatawale’ na imani kwamba umoja ni nguvu. Wahariri
wote hawapaswi kukaa kimya kuhusu kufungiwa kwa MwanaHALISI kwa kuwa leo
ni kwa gazeti hilo, kesho itakuwa kwa gazeti lingine; hivyo ni vyema
kuungana pamoja kulinda uhuru, taaluma na sekta ya habari nchini.
Kwetu
sisi hatua hiyo ya serikali tunaitafsiri zaidi ya kufungia gazeti la
MwanaHALISI; ni hatua ya kufungia uhuru wa kusambaza habari na uhuru wa
kupokea habari. Hivyo hatua hiyo ni kinyume cha haki za binadamu,
kinyume cha utawala bora na ni kikwazo kwa demokrasia na maendeleo.
Hakika serikali na viongozi wake wamevuka mstari wa kukubali kukosolewa
na sasa wameamua kuanza kufungia uhuru wa fikra mbadala.
Hatua ya
Waziri mwenye dhamana na sekta ya habari kugeuka mlalamikaji, mwendesha
mashtaka na mfungaji ni mwelekeo mbovu wa kupuuza taasisi za kusimamia
uwajibikaji na haki. Uamuzi uliofanywa na serikali hauna tofauti na
unaofanywa na raia wanaojichukulia sheria mikononi(mob justice). Kwa
serikali inayoheshimu misingi ya asili ya haki, tulitarajia chombo
chochote cha habari, kikivunja sheria ama kukiuka maadili dhidi ya
serikali, viongozi wake ama watu binafsi mashtaka ama malalamiko
yangepelekwa kwa taasisi zinazohusika mathalani Baraza la Habari(MCT)
ama Mahakama.
Hatua ya serikali kufungia gazeti la MwanaHALISI
pamoja na kuwa imechukuliwa kwa mujibu wa sheria iliyopo, imekiuka
misingi ya asili ya utawala wa sheria. Kwani kulikuwa na sheria nyingine
nzuri ambazo serikali ingeweza kutumia kupitia mahakama lakini ikaamua
kuchagua kutumia sheria mbaya kwa kutumia mamlaka ya Waziri. Itakumbukwa
kwamba wadau wa sekta ya habari na hata serikali yenyewe imekuwa
ikikiri kwamba Sheria hiyo iliyotumiwa ni sheria mbovu inayohitaji
kufutwa ama kufanyiwa marekebisho makubwa ikiwemo kupunguza mamlaka
makubwa ya viongozi wa serikali dhidi ya vyombo vya habari.
Sheria
yoyote inayotambulika kuwa mbovu katika jamii yoyote, inapoteza uhalali
wa kihaki(legitimacy) miongoni mwa umma na hivyo kuendelea kuitumia ni
kuteteresha misingi ya utawala wa sheria na kutoa mfano mbaya kwa vijana
nchini na wananchi kwa ujumla. Hivyo, tunachukua fursa hii kuitaka
serikali kuharakisha mchakato wa kupitisha sheria ya vyombo habari na
sheria ya uhuru wa taarifa.
Aidha tumeshangazwa na uamuzi wa
serikali kufanya maamuzi yake kwa ubaguzi kwa kulichukulia hatua gazeti
la MwanaHALISI na kukwepa kuyachukulia hatua magazeti mengine ambayo
yameandika habari inayoshabihiana na maudhui ya habari iliyoandikwa na
gazeti hilo. Kwa muda mrefu sasa, habari za uwepo wa viongozi ama
makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) yenye kupanga ‘kumng’oa’ Rais
Jakaya Kikwete miongoni mwa wanaotarajiwa kugombea urais kupitia chama
hicho mwaka 2010 zimeandikwa na magazeti mbalimbali.
Hatua hii
ya kibaguzi inaibua maswali kuhusu dhamira ya serikali kulifungia gazeti
hilo wakati huu ambapo mchango wa gazeti hilo na mengine yaliyo mstari
wa mbele kupinga ufisadi na kutetea rasilimali za taifa unahitajika kwa
kiasi kikubwa. Hata baada ya kulifungia gazeti la MwanaHALISI, habari za
aina hiyo zimeendelea kuandikwa ikiwemo na vyombo vya habari vya nje;
mathalani tarehe 24 Oktoba, 2008 kutoka Ufaransa gazeti la Africa
Intelligence inayomtaja Rostam Aziz kukusanya fedha kwa ajili ya
kufadhili kundi lake katika uchaguzi huo. Katika muktadha huo, serikali
inapaswa kulifungia gazeti la MwanaHALISI mara moja, kama imeonyesha
wazi kushindwa kuyachukulia hatua magazeti mengine.
Kadhalika kwa
mtiririko wa matukio katika taifa letu, kuna mwelekeo wa Serikali na
CCM kuminya maoni yenye kumkosoa au kumgusa Rais Kikwete. Mjadala wa
Rais Kikwete ‘kung’olewa’ katika uchaguzi mwaka 2010 unaelekea
kuichukiza kwa kiasi kikubwa Serikali na CCM. Gazeti la MwanaHALISI
liliandika habari ya namna hiyo, likafungiwa na Serikali. Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe akiwa katika ‘Operesheni Sangara’, alitoa hoja
hiyo na matokeo yake CCM ikaibuka na kujibu kwa vitisho na vioja.
Vijana
wa Tanzania wangependa kupata mfano uongozi bora wenye kukubali
kukosolewa na kukubali mabadiliko badala ya uongozi legelege wenye
kuendeleza udikitekta wa kimawazo na hivyo kuminya fikra huru. Si dhambi
kwa CHADEMA ama mtu yoyote kutaka kuiondoa CCM ama kiongozi wake yoyote
madarakani mwaka 2010 kupitia njia za kidemokrasia.
Mwisho,
tunatoa mwito kwa watanzania wote kusoma alama za nyakati na kuunga
mkono harakati hizi za wahariri na wadau wa sekta ya habari kutetea
uhuru wa kweli katika taifa letu. Jamii itambue kwamba kitisho cha uhuru
na haki kwa mtu Fulani au mahali Fulani ni tishio kwa watu wote na
mahali pote. Yanayofanywa kwa vyombo vya habari, yanaweza pia kufanywa
kwa watetezi wengine kwani hivi karibuni taifa limeshuhudia Asasi ya
HAKIELIMU ikitishiwa kutokana na jitihada zake za kuhamasisha mabadiliko
ya fikra katika sekta ya elimu na kupiga vita ufisadi unaoathiri sekta
hiyo. Tuko katika kipindi cha majaribu; kuibuka kwa mijadala yenye
kuchochea mgawanyiko/ubaguzi, kuongezeka kwa matabaka na malalamiko juu
ya hali za maisha. Katika wakati huu ambapo misingi ya nchi yetu iliyopo
katika Ngao ya Taifa ya Uhuru na Umoja inapotikiswa ni wakati wa
kuunganisha “Nguvu ya Umma” kupinga aina zote za ufisadi na kutetea
rasilimali za taifa kwa kuhamasisha maadili, fikra mbadala na mabadiliko
ya kweli. Kuunga mkono maandamano ya wadau wa sekta ya habari ni sehemu
ya azma hiyo. Mshikamano, daima; pamoja, tutashinda!
Wasalaam,
John Mnyika Mkurugenzi wa Vijana Taifa.
|
No comments:
Post a Comment