UMOJA WA VIJANA NA FIKRA
MGANDO
Ado Shaibu.
Kimuundo, vyama vya siasa huwa na jumuiya
za kuiwezesha kutimiza matakwa yake ya kisiasa. Mathalani, kwa upande wa CCM
kuna Jumuiya ya Wazazi, Umoja wa wanawake (UWT) na Umoja wa vijana (UVCCM).
Hata baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, muundo
wa vyama vingi vya siasa nchini umenakili kwa kiwango kikubwa muundo wa taasisi
na jumuiya za CCM. Kwa mfano, kwa upande wa CHADEMA, kuna Baraza la Wanawake
(BAWACHA) , Baraza la wazee wa chama na baraza la vijana (BAVICHA).
Lengo la makala hii ni kuelezea, japo kwa
ufupi, mchango wa umoja wa vijana katika chama cha siasa na kutoa changamoto
kwa jumuiya za vijana katika vyama vyetu vya siasa vya leo katika mfumo wa
vyamavingi. Haitoshangaza kuona nikitupia jicho CCM kwa kiwango kikubwa kuliko
vyama vingine kutokana na ukweli kwamba chenyewe ndicho kilichobeba dhamana ya
kuwaletea maendeleo watanzania mpaka uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Tukidurusu historia ya nchi yetu ,
tutakumbuka kwamba uanzishwaji wa jumuiya za vijana katika vyama vya siasa sio
jambo geni hata kabla ya uhuru. Kwa mfano, kwa upande wa Tanganyika, kulikuwa
na ''Tanu Youth League''(TYL) na kwa
upande wa zanzibar, kulikuwa na ASP Youth
League.
Katika makala zangu zilizopita huko nyuma
katika gazeti hili, nimewahi kueleza kwa ufupi mchango wa tawi la TANU Youth League pale chuo kikuu (UDSM)
na Umoja wa Wanafunzi Wanaharakati ( University
Student Revolutionary Front-USARF).
Tofauti na hali ilivyo sasa kwenye vyama vya
siasa ambapo kwa sehemu kubwa vijana hutumiwa kama wapambe tu wa wawania nafasi
za uongozi ndani ya vyama , enzi hizo TYL na USARF yalikuwa majukwaa ya
kujadili, kutathmini na kuchukua hatua kuhusu mustakabali wa Tanzania, kupaza
sauti kuhusu ukombozi wa Afrika na kutetea wanyonge wa pande zote za ulimwengu.
Hebu nitoe mifano michache: Wakati Tanzania
ilipotangaza Azimio la Arusha mwaka 1967 ili kuondosha unyonge wetu na kukata
mirija ya unyonyaji iliyowanufaisha mabwanyenye wachache, umoja wa vijana wa
TANU haukuishia kutoa matamko ya kuunga mkono azimio na kutembea kilomita
nyingi kuiunga mkono TANU kwa uamuzi wa kizalendo na wenye kuleta nuru ya
matumaini kwa wanyonge walio wengi.
Kwa upande wa tawi la TYL pale mlimani na
umoja wa USARF, wao walienda mbali zaidi na kushiriki kikamilifu katika
kuhakikisha ufanisi wa sera na programu za azimio la Arusha zilizolenga
kuwakomboa wanyonge hasa wakulima na wafanyakazi wa kada ya chini.
Wanachama
wa TYL na wale wa USARF kama kina Issa Shivji (sasa profesa wa kigoda cha
mwalimu Nyerere katika umajumuhi wa Afrika), Karim Hirji (sasa profesa wa biostatistics chuo kikuu cha Afya-
Muhimbili), Zakia Hamdan Meghi (sasa mbunge wa kuteuliwa na rais na waziri wa
zamani wa fedha) Yoweri Kaguta Museveni ( sasa rais wa Uganda), Henry Mapolu (sasa
marehemu) na wengineo wengi ambao ni vigumu kuwaorodhesha wote, walipigana
vilivyo kulijenga Azimio la Arusha kwa vitendo.
Wana TYL na makomredi wa USARF wa pale
mlimani walizunguka katika shule za sekondari mikoani na kufundisha itikadi ya
ujamaa na kujitegemea; walitembelea vijiji vya ujamaa; kulima mashamba na wanavijiji
kwenye mashamba ya vijiji na kujadili nao ujenzi wa sera ya ujamaa na
kujitegea. kwa wanawake kama Zakia Hamdani Meghi wa miaka ile, huu ulikuwa
wasaa wa kuuvua utukufu wa uanachuo na kushirikiana na wanawake wa vijijini
kuteka maji visimani, kupika chakula na kutafakari kwa pamoja kuhusu ukombozi
wa mwanamke wa Afrika.
Mpango wa elimu kwa watu wazima
ulipoanzishwa miaka ya sitini wanachuo wa umoja wa vijana wa TANU na wenzao wa
USARF hawakuishia kuwa watoa matamko ya kupongeza tu; kumbukumbu zinaonyesha
walishiriki kikamilifu kuwafundisha kina mama na wazee kufuta ujinga. Walitenga
muda wa ziada kuwaongoza wazee wa mijini na vijijini katika vita ya kufuta
ujinga wa kutojua kusoma na kuandika kupitia madarasa ya elimu ya watu wazima.
Pengine tofauti kubwa kabisa baina ya
jumuiya za vijana za miaka ya sitini na sabini kwa upande mmoja na jumuiya za
miaka ya leo kwa upande mwingine; tofauti ambayo huko nyuma nimewahi
kuimithilisha na tofauti ya kichuguu na mlima kilimanjaro, ni kuhusu kufanya
utafiti. Kwa kweli yapo malalamiko kwamba vijana wa sasa tunahusudu kukurupuka
kutoa matamko, tuhuma na malalamiko bila kufanya uchambuzi wa kina na utafiti.
Wana TYL na USARF wa miaka ya sitini na
sabini walihusudu sana kutanguliza utafiti kabla ya kuyatolea matamko masuala
mbalimbali. Ukipata bahati ya kusimuliwa jinsi USARF ilivyoanzisha madarasa
yake ya mijadala na itikadi kila wikiendi pale mlimani lazima utakiri jinsi
vijana wale walivyojibidiisha kuusaka ukweli, kuusambaza na kuusimamia. Pia,
kijarida cha ''Cheche'' kilichotolewa na USARF na kujizolea heshima hadi nje ya
mipaka ya nchi, kilisheheni mada za kiutafiti kuhusu masuala mbalimbali ya
jamii ya Tanzania na dunia kwa ujumla zilizowasilishwa na wanafunzi na
wahadhiri kama kina Profesa Walter Rodney.
Kilele cha mafanikio ya utafiti wao wa
ujanani kilifikiwa kwa utafiti wa profesa shivji (enzi za uanafunzi wake)
uliokwenda kwa jina la ''silent class struggle'' katika jarida la ‘’cheche’’. katika utafiti huo uliowakera
baadhi ya watawala wa miaka hiyo, pamoja na mambo mengine, Prof.Shivji alionya
kwamba badala ya kujenga ujamaa kama ulivyofafanuliwa na Azimio la Arusha,
taratibu tabaka la mabwanyenye wa kiutawala ambao Prof.Shivji aliliita ‘’Bureaucratic
bourgeoisie’’ lilianza kuchomoza Tanzania.
Licha
ya kupuuzwa kwake miaka ile, takribani muongo mmoja baadaye, CCM ilikiri ukweli
wa Prof.Shivji katika muongozo wa CCM wa mwaka 1981 kwamba kulikuwa na kuchipua
kwa tabaka jipya la mabwanyenye na wahujumu uchumi walioanza kuhujumu ufanisi
wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea.
Pia kumbukumbu zinaonyesha kwamba baadhi ya
sera za taifa zilitokana na ushawishi wa Umoja wa vijana wa TANU. Kwa mfano,
kumbukumbu za wizara ya ulinzi na Jeshi la kujenga taifa zinaonyesha kwamba
uamuzi wa kuanzisha jeshi la kujenga taifa (JKT), ulitokana na mapendekezo ya
mkutano mkuu wa TYL uliofanyika tarehe 25 Agosti 1962 mjini Tabora chini ya
Joseph Nyerere aliyekuwa katibu wa umoja huo.
kiujumla yako mambo mengi yaliyotekelezwa
na jumuiya za vijana miaka ya sitini mpaka themanini. Kadiri Rabana
atavyotujalia uhai na fursa zaidi, tutaendelea kuchambua michango hiyo ili
vijana wa leo tupate darasa la kujadili na kujifunza kutoka kwa vijana wa enzi
hizo.
Sasa tujiulize swali la msingi; Je umoja wa
vijana wa CCM (UVCCM) na jumuiya za
vijana za vyama vya upinzani zinatekeleza majukumu yake ya kihistoria
kwa ukamilifu? Ukiachilia maeneo machache, hasa katika utoaji wa matamko na
maandamano ya kuunga mkono hotuba za viongozi wa kitaifa, jumuiya za vijana
zimepoteza kwa kiwango cha kutisha jukumu lake la kihistoria la kuwasemea
vijana, kuyatafiti matatizo ya vijana na kuishauri serikali kuhusu mambo
mbalimbali yanayoviza mustakabali wa vijana na kufifisha ustawi wa taifa letu kwa
ujumla.
Kwa
mtizamo wangu, badala ya vijana wa UVCCM kuitisha vikao na kulumbana kuhusu
atokako rais ajaye wa Tanzania, nilitamani vijana hao wangeitisha vikao vya
kutathmin mustakabali wa ‘’machinga’’ wa ubungo, Tandika na kwingineko Tanzania
wanaofurushwa na wanamgambo wa jiji bila kuelekezwa pa kwenda.
Binafsi nilidhani badala ya UVCCM kuunda
kamati ya kutatua matatizo ya kufikirika, ingeunda kamati ya kudurusu ule
mkakakati wa serikali wa ‘’nguvu kazi’’ (Human Resources Deployment
Act,1983) na kutafakari changamoto zake ili kuepusha matatizo waliyokumbana
nayo wafanyabiashara ndogondogo wa miaka ile ya themanini yasiendelee kuwakumba
wafanyabiashara wa sasa katika mipango ya jiji. Nilidhani kwa ujana wao,
wangejibidiisha kutafakari na kutathmini namna ya kutengeneza mfumo bora zaidi
utaowafanya wafanyabiashara ndogondogo ambao wengi wao ni vijana, kujiingizia
kipato zaidi na kutoa mchango wao kwa taifa bila kubughudhiwa.
Mimi nilidhani badala ya wana UVCCM kujibidiisha
kuunda makundi hasimu ya kambi za urais wa 2015, wangejibidiisha kufanya
tafakuri ya kina ya tatizo la ajira ambalo viongozi wa chama na serikali
wamelibatiza kuwa ‘’bomu linalosubiri kulipuka’’ na kwa njia ya utafiti,
kutafuta hatua mujarabu za kuchukua katika kuzalisha ajira zaidi na kuwakomboa
mamilioni ya vijana wanaoshinda vijiweni kwa kukosa ajira.
Kwa kweli hamu yangu ilikuwa ni kuona UVCCM
ikiachana na mtindo wa sasa wa kuishia kwenye matamko na maandamano ya kuunga
mkono hotuba na kwenda mbali zaidi kujiuliza kwa nini licha ya serikali kutenga
pesa nyingi kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kuliko nchi nyingi za Afrika
mashariki na kati, migogoro vyuoni haiishi? Nilidhani wangetafiti na
kupendekeza kuhusu namna bora zaidi ya kudhibiti mamilioni yanayoishia mikononi
mwa baadhi ya wahasibu wasio watiifu vyuoni na baadhi ya wahujumu uchumi pale
bodi ya mikopo wanaojichotea mamilioni ya walipakodi yaliyotengwa kusomesha
watoto wa walalahoi.
Nilidhani badala ya kuendelea kulumbana na kukashifiana
kwenye mitandao ya kijamii, UVCCM wangeenda vijijini kama walivyofanya USARF na
TYL na kujionea wenyewe jinsi vijana wenzetu
wakulima kule Tandahimba, Newala, Pwani, Masasi, Tunduru na kwingineko Tanzania
wanavyokatishwa tamaa kwa kutolipwa malipo ya korosho kwa miezi kadhaa na
kucheleweshewa pembejeo za kilimo kwa sababu ya ufisadi wa wafanyabiashara
wachache kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya.
Badala
ya kuishia kupongeza ujenzi wa maelfu ya madarasa ya shule za kata, ningefurahi
kama wana UVCCM wangeenda mbali zaidi na kutawanyika Tanzania nzima ili
kujionea madhila wanayokumbanayo wanafunzi wa shule za kata zisizo na walimu,
vitabu na maabara! Kisha baada ya hapo watafakari hatma ya mfumo wetu wa elimu
na jinsi ubidhaishaji wa elimu tangu ngazi ya elimu ya elimu ya awali
unavyozalisha pengo la kutisha baina ya walalaheri na walalahoi katika
uliberali mamboleo.
Hata
kwa upande wa wapinzani, nilidhani kina John Heche na makomredi wengine wa
BAVICHA wangeacha kupoteza muda wao
kujibu matamko ya kina John Magale Shibuda na wengineo ndani ya CHADEMA
wanaotangaza nia ya kuwania urais 2015 kupitia CHADEMA na badala yake
kujibidiisha kujenga mapinduzi ya kifikra kwa vijana wenzao.
Kama alivyowahi kutuasa Dk.Kitila Mkumbo, nadhani
huu ni wakati muafaka kwa BAVICHA, UVCCM na vijana kwenye vyama vingine vya
siasa ‘’kubalehe kisiasa’’ kwa kuacha siasa za kitoto na kujibidiisha kwenye
mambo ya msingi yatakayoleta tija kwa vijana wenzao na kuchochea mustakabali wa
taifa. Ni wakati muafaka wa kuonyesha ujana wa fikra: fikra za kimapinduzi.
Fanya tafakuri ya kina kisha
chukua hatua!
Simu: 0653619906 Barua pepe: adoado75@hotmail.com
Makala hii ilichapwa kwa mala
ya kwanza kwenye gazeti la RAI toleo na.982.
1 comment:
well said kijana..UVCCM inapaswa kuyatilia maanani maoni haya ili kurejesha makali ya enzi za TYL
Post a Comment