BUNGE LISIZUIWE KUINGILIA KATI MGOGORO KATI YA WALIMU NA WANAFUNZI DHIDI YA SERIKALI KWA KISINGIZIO CHA KESI KUWA MAHAKAMANI
Tarehe 1 Agosti 2012 niliieleza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia swali
langu la msingi bungeni kwamba serikali hutoa ruzuku (capitation
grants) kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari za Umma zikiwemo
za Jimbo la Ubungo, japo utekelezaji wa sera husika huwa unasuasua sana
kwa kiwango kilichowekwa kutokulingana na mahitaji halisi ya wanafunzi;
viwango vinavyotengwa katika Bajeti ni chini ya vinavyotajwa kwenye Sera
na Fedha hazitolewi zote isipokuwa hutolewa kidogo kidogo na hazifiki
kikamilifu mashuleni; nikahoji ni lini serikali itarekibisha hali hiyo
ili kuboresha elimu nchini.
Ofisi ya Waziri Mkuu katika majibu
yake imekiri kwamba kweli viwango vya ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa
shule za msingi na sekondari havijafikiwa mpaka sasa na hata fedha
zinazotengwa kwa mujibu wa bajeti hazitolewi kwa kiwango kilichopitishwa
na bunge kwa kile alichoeleza kuwa ni makusanyo ya Serikali.
Niliuliza maswali mawili ya nyongeza; nilihoji ni lini serikali
itatekeleza sera husika kwa kuwa upungufu wa ruzuku kwa shule za umma ni
kati ya vyanzo vya kuporomoka kwa elimu kutokana na kuathiri uendeshaji
wa shule ikiwemo upatikanaji wa vifaa shuleni, na kwa kuwa kwenye
vyombo vya habari jana na leo kati walimu na wanafunzi wameeleza kwamba
hali hiyo ni kati ya sababu za mgomo unaoendelea hivyo nikata serikali
itoe kauli bungeni ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro unaoendelea.
Hata hivyo Spika wa Bunge alimkataza Naibu Waziri asijibu swali kuhusu
mgogoro kati ya walimu na wanafunzi dhidi ya serikali na kutaka kujibiwa
kwa swali ya lini ruzuku itaanza kutolewa kwa kuzingatia viwango vya
sera hata hivyo serikali ilitaja kiwango cha fedha ya ruzuku kwa mwaka
wa fedha 2012/2013 bila kueleza iwapo viwango kwa mujibu wa sera
vitafikiwa kwenye ngazi zote ikiwemo katika shule za msingi.
Kwa mara nyingine tena Bunge limezuia kupewa taarifa kuhusu masuala hayo
kwa kisingizio cha kesi kuwa mahakamani hatua ambayo inadhihirisha kwa
mara nyingine tena umuhimu wa kusikilizwa kwa rufaa niliyokata tarehe 31
Julai 2012 ili suala la mgomo wa walimu, madai ya wanafunzi na hatma ya
sekta ya elimu lijadiliwe kwa dharura bungeni.
Nimefanya hivyo
kwa niaba ya walimu, wanafunzi na wadau wengine wa elimu katika Jimbo
la Ubungo na Tanzania kwa ujumla ili bunge lipewe fursa ya kutimiza
wajibu wake wa kikatiba kuisimamia serikali itekeleze madai ya walimu na
kuepusha athari za migogoro inayoendelea katika shule za umma nchini.
Tarehe 30 Julai 2012 kwa nyakati mbalimbali kumetolewa miongozo na
maamuzi na Mheshimiwa Naibu Spika Job Ndugai ya kukataa hoja kwa mujibu
wa Kanuni ya 47 ya kuahirishwa kwa Shughuli za Bunge kujadili jambo la
dharura la mgomo wa walimu na yatokanayo na mgomo huo kwa kutumia kanuni
ya 64 (1) (c) ya kanuni za bunge toleo 2007 ambayo inamkataza mbunge
kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama.
Nimewasilisha rufaa kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) kueleza kutoridhika
na uamuzi wa Naibu Spika wa kutumia kanuni ya 64 (1) (c) kudhibiti Bunge
kutumia uhuru na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ya nchi; sheria ya
haki, kinga na madaraka ya bunge na kanuni nyingine za Kanuni za Kudumu
za Bunge kwa sababu tatu.
Mosi, Suala la yatokanayo na mgomo
wa walimu hususani hali tete ya sekta ya elimu kwenye shule za umma
haliko mahakamani, kilichopo mahakamani ni mgogoro kati ya Chama cha
Walimu Tanzania (CWT) na serikali kuhusu madai ya walimu:
Pili,
hata masuala yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti
kwa mujibu wa kanuni 64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni
kwa muongozo na utaratibu utakaowezesha majadiliano kufanyika bila
kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge.
Tatu; izingatiwe pia kuwa masuala
yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa mujibu wa
kanuni 64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo
na utaratibu utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa
mahakama kwa kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Kwa kuzingatia sababu nilizozieleza, nimeomba kamati ya kanuni
ibatilishe maamuzi yaliyofanyika na kutoa pia muongozo wa kikanuni;
hivyo nimeomba Katibu wa Bunge amtaarifu Spika kwa mujibu wa kanuni ya 5
(4) na kuitisha kikao cha dharura cha kamati ya kanuni kwa mujibu wa
kanuni ya 5 (5) ya kanuni za Kudumu za Bunge na kulijulisha bunge kuhusu
uamuzi utakaotolewa.
Wako katika kuwawakilisha wananchi, John Mnyika (Mb) Mbunge wa Jimbo la Ubungo, CHADEMA 01 Agosti, 2012
|
No comments:
Post a Comment