FOLLOWERS

Friday, August 3, 2012

CHADEMA NA POLISI WAVUTANA

Chadema, Polisi wavutana
Thursday, 02 August 2012 20:52
MKUTANO WAO WAPIGWA MARUFUKU,WENYEWE WASEMA LAZIMA UFANYIKE
Joseph Zablon
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeingia tena katika mzozo na Jeshi la Polisi nchini, baada ya mkutano wake uliopangwa kufanyika mjini Morogoro kuzuiwa kwa maelezo kwamba, hakuna askari wa kutosha wa kuuwekea ulinzi.

Pamoja na zuio hilo, Chadema wanasema lazima mkutano huo ufanyike kwa maelezo kwamba sababu zilizotolewa na polisi siyo za msingi na zina ajenda ya kuhujumu kampeni yao waliyoiita ‘vua gamba, vaa gwanda’.

Mvutano huo unatishia amani mji wa Morogoro na viunga vyake, ikiwa Chadema wataendelea na msimamo wao huo, hali polisi wakitumia nguvu kuzuia mkutano huo na mingine midogo katika kata 28 iliyoombwa isifanyike.

Chadema kiliwahi kuingia katika mvutano na polisi katika baadhi ya matukio makubwa ambayo ni pamoja na katika miji ya Mwanza huku mapambano ya jijini Arusha yakisababisha mauaji.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Mkuu wa Operesheni wa Chadema, Benson Kigaila alisema kuwa wamepokea taarifa ya polisi ya kuwataka wasifanye mkutano huo, lakini wao kama chama hawatarudi nyuma.

"Mkutano wetu upo palepale na utahudhuriwa na viongozi wote wa kitaifa, wakiwamo wabunge wetu wote na utafunguliwa na Mwenyekiti wa wetu wa Taifa, Freeman Mbowe," alisema Kigaila.

Kigaila alisema mikutano hiyo ni ya kukiimarisha chama  na inaratibiwa na chama na sio polisi hivyo, kwa jeshi hilo walikuwa wanatoa taarifa na kuomba ulinzi na sio kulitaka liwapangie utekelezaji wake.

"Mkutano ni makubaliano ya ndani ya chama na ajenda yetu ni kuwahamasisha Watanzania kujiunga na chama na ni sehemu ya operesheni Sangara," alisema Kigaila na kuongeza kuwa, maandalizi kwa ajili ya mkutano huo yamekamilika.

Zuio la mkutano
Kigaila alisema zuio la mkutano huo limetokana na barua yenye kumbukumbu Namba MRG/SO.7/2/A/219, ya Agosti Mosi mwaka huu kutoka kwa Kamanda wa Polisi Morogoro kwenda kwa Katibu Chadema wilaya.

Kigaila alisema baada ya kujitokeza hali hiyo aliwasiliana na kamanda wa polisi na walimuomba wafanyie mkutano wao eneo la Mvomero ombi ambalo pia lilikataliwa kwa madai kuwa haiwezekani kutokana na  mgomo wa walimu.

"Mara waseme kuna Nane nane, CCM nao wana mkutano Morogoro hivyo haiwezekani, tunapomwambia tukafanyie Mvomero anadai kuna mgomo wa walimu sasa hoja yake ipi hapa tunashindwa kumuelewa," alisema Kigaila.

Alidai ni wazi jeshi hilo linatumika kwa manufaa ya kisiasa kwani yeye anavyofahamu ni kwamba ikiwa kuna vyama viwili vinavyotaka kufanya mikutano yake, basi hupangiwa maeneo tofauti.

"Kama wengine wakipanga eneo fulani basi sheria inataka chama kingine kifanye mkutano wake mita 500 kutoka walipo wenzao,” alisema.

Kigaila alisema mkutano wao huo utafuatiwa na mingine katika kata 28 za mji huo kabla ya kuelekea katika miji ya Iringa, Dodoma, Manyara na Singida na awamu inayofuata itahusisha mikoa ya Tabora, Shinyanga, Simiyu na Mwanza.

Operesheni hiyo itaendelea katika miji ya Mara, Kagera na Geita kabla ya kurudi kumalizia mikoa iliyokuwa imesalia Kusini na ni operesheni ya kawaida ya kuhamasisha watu kujiunga na chama hicho

Taarifa ya polisi
Kulingana na taarifa hiyo (ambayo Mwananchi limeona nakala yake), sehemu yake inasomeka: “Rejea barua yako ya Julai 30, 2012 ya kutoa taarifa na kuomba ulinzi kwa ajili ya maandamano na mikutano ya hadhara mliyokusudia kufanya K/Ndege Agosti 4, 2012 na Agosti 5 kwa Kata 28”.

"Katika tarehe  zilizoainishwa hapo juu Chama cha Mapinduzi (CCM), wamekusudia kufanya mikutano ya hadhara ya wanachama, wapenzi na makada wao katika maeneo hayo hayo," inasema taarifa hiyo.

Inaongeza kuwa Agosti mosi hadi 10 mwaka huu, maadhimisho ya sherehe za Nane Nane yanaendelea katika Mkoa huo na kama vile haitoshi, katika tarehe zilizoanishwa, mgomo wa walimu wa shule za msingi na sekondari unaendelea nchi nzima.

Sehemu ya taarifa hiyo iliongeza kwamba, kutokana na sababu hizo shughuli zote zinahitaji ulinzi na usalama ambao utasimamiwa na polisi, hivyo kutokana na mgawanyo uliopo wa askari itakuwa vigumu kusimamia shughuli zote kwa wakati mmoja.

"Kwa mantiki hiyo, kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro amesitisha mikutano ya hadhara na maandamano hayo kwa mujibu wa kifungu namba 43 (1-6) cha sheria za Polisi na polisi wasaidizi sura 322 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002," inabainisha barua hiyo.


No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...