Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini na mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge inayoshughulikia viwanda na biashara mheshimiwa Mahmoud Mgimwa |
Aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa TBS Charles Ikerege wa kwanza kushoto |
Kwa mujibu wa habari ya jumapil ikatika
gazeti la Tanzania daima iliyoandikwa na Asha Bani MKURUGENZI wa Shirika la
Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege aliyesimamishwa kazi, anaelekea
kulivuruga Bunge na kusababisha mgongano wa kimamlaka.
Kuibuka kwa mvurugano huo kunatokana na
hatua ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa
kusafiri kwenda nje ya nchi na menejimenti ya TBS pasipo kupata baraka au
kibali cha Spika wa Bunge.
Mbali ya hilo, Mgimwa ambaye hivi karibuni
alituhumiwa kuandaa ripoti ya kumsafisha mkurugenzi huyo wa TBS baada ya ziara
hiyo, ameibuka na kukana kupata kufanya hivyo.
Sambamba na hayo, hali ya mkorogano ndani ya
Bunge imeongezwa na hatua ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuibuka na kueleza
kutojua chochote kuhusu ziara hiyo wala ripoti iliyokuwa na mwelekeo wa
kumsafisha Ekelege ambaye hivi karibuni aliibua mjadala mkali bungeni.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili,
Spika Makinda alisema alikuwa hana taarifa zozote kuhusu suala hilo wala safari
ya Mgimwa kwenda Japan na China akiwa ameongozana na menejimenti ya TBS.
“Mgimwa alisafiri kama
Mgimwa. Mimi Spika sina taarifa na wala ofisi yangu haijampa kibali, na
sitambui wala sijui ameendajeendaje huko, labda akwambie yeye, maana sisi tuna
utaratibu wetu,” alisema Makinda.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili,
Mgimwa alikiri kusafiri na timu hiyo ya watu 14 kutoka TBS katika kipindi cha
kati ya Mei 6 na 14 mwaka huu, lakini akasema yeye alienda huko kwa ajili ya
kujifunza na si kufanya uchunguzi kama
ilivyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Kuhusu kutopata ridhaa ya Spika au kibali
chake, Mgimwa ambaye ni mbunge wa Mufindi Kaskazini, alisema ziara hiyo
aliyoiita ya kujifunza, ilikuwa haina uhusiano wowote na shughuli za Kamati ya
Bunge Viwanda na Biashara.
Mbali ya hilo, Mgimwa alikana kuandaa ripoti
yoyote kwa niaba ya kamati yake ambayo pamoja na mambo mengine, ilikuwa
ikimsafisha Ekelege, na akasema iwapo kulikuwa na taarifa yoyote basi ilitolewa
na TBS wenyewe ambao ndio waliomwalika katika ziara hiyo.
“Mwandishi labda nikueleweshe hiyo isije
kuleta matatizo. Mimi nilienda kama mimi
kujifunza na wala kuhusu ripoti mimi sijui kwa kuwa sikuiandika. Waulizeni TBS
ambao ndio waliandika na kamati yangu haihusiki kwa lolote na wala yenyewe
haikufanya ziara.
“Ni kweli nilienda Japan na menejimenti hiyo
na nilialikwa kama mtu binafsi na kwamba hakuna ripoti yoyote niliyoandika,
pengine kama imeandikwa na TBS wenyewe, hivyo waulizwe hiyo ripoti wao.
Sikwenda kumsafisha mtu mimi,” alisema Mgimwa.
Hata hivyo, ripoti iliyotolewa na TBS yenye
mwelekeo wa kumsafisha Ekelege na taasisi yake, ambayo Tanzania Daima Jumapili
iliiona nakala yake, inaeleza kuridhishwa na namna mawakala wa shirika hilo wanavyofanya kazi nzuri katika nchi za China na Japan.
Akifafanua zaidi, Mgimwa kutokana na uzoefu
alioupata, anaamini kuna haja kwa wajumbe wa kamati yake kwenda katika nchi
zenye ofisi za TBS kwa ajili ya kujifunza, na kwamba alikuwa akitarajia kutuma
maombi kwa Spika ili awape ruhusa waende wakaangalie sheria mbalimbali kama zinafaa au la.
Habari kutoka ndani ya duru za kamati za
Bunge zinaeleza kwamba, hatua hiyo ya Mgimwa inaonekana kuchukua mwelekeo
tofauti na unaokinzana na ule uliochukuliwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC), ambayo katika ripoti yake kwenye mkutano uliopita wa
Bunge, iliibua shutuma nzito dhidi ya TBS na mkurugenzi wake, Ekelege.
Taarifa hiyo ya POAC ambayo ilimbana pia
aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami kwa tuhuma za kumlinda
Ekelege, iliibua kile kilichoonekana kuwa ni uoza ndani ya TBS, ambayo
ilibainika kuwa na ofisi hewa katika baadhi ya mataifa ambako ilikuwa ikidai
kukagua ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini.
Ripoti hiyo ya POAC ambayo ilimlaumu Chami
kwa kushindwa kumsimamisha kazi au kumwajibisha Ekelege, ilitokana na ziara
walizofanya baadhi ya wajumbe wake waliotembelea Hong Kong na Singapore na
kubaini kasoro hizo.
Siku chache tu baada ya Rais Jakaya Kikwete
kumteua Dk. Abdallah Kigoda kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, waziri huyo
alitangaza kumsimamisha kazi Ekelege na kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma
zilizokuwa zikielekezwa kwake.
No comments:
Post a Comment