Mkuu wa mkoa wa pwani Bi Mwantum Mahiza |
Kufuatia kuzuka mapigano makali kati ya wafugaji na wakulima katika mji
wa Ikwiriri wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Mkuu wa mkoa huo Mwantum
Mahiza amezuia na kusitisha zoezi la uingizaji wa mifugo inayoingizwa mkoani
humo na wafugaji waliohamishwa kutoka bonde la mto Ihefu na mikoa mingine
nchini.
Akitoa tamko hilo mbele ya kikao cha kamati ya ushauri ya
mkoa huo Mahiza amesema mkoa umeamua kuzuia kabisa uingizaji wa mifugo yoyote
ndani ya mkoa huo kwa ajili ya malisho kutokana na migogoro na mapigano
ya mara kwa mara yanayotokea kati ya wakulima na wafugaji.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa amesema
usitishaji na uzuiaji wa mifugo inayoingizwa katika mkoa huo haihusu mifugo
inayosafirishwa kwenda mikoa au nchi jirani kwajili biashara bali inahusu
mifugo inayoingizwa kwajili ya malisho.
Mahiza amesema tayari amemuandikia
barua waziri wa mifugo Dokta David Matayo kumueleza kusudio hilo.
Tamko la kuzuia uingizaji wa mifugo kwa
mkoa wa Pwani linakuja ikiwa ni wiki mbili tu zimepita tangu kuzuka kwa
mapigano makali kati ya wakulima na wafugaji katika mji wa ikwiriri wilayani
Rufiji na kusababisha kifo cha mtu mmoja, uchomaji wa nyumba na uharibifu
mkubwa wa mali.
No comments:
Post a Comment