FOLLOWERS

Wednesday, June 6, 2012

UTAFITI WA TAMWA JUU YA KUFELI NA MIMBA SHULE ZA KATA

Ananilea Nkya, Mkurugenzi Mtendaji TAMWA

Wakuu wapya wa wilaya wanapaswa kuandaa mipango mkakati ya kuondoa matatizo yanayochangia wanafunzi wa shule za kata kufeli na wasichana wengi kukatishwa masomo kutokana na kupata mimba au kulazimishwa kuolewa.
Viongozi hawa wanatakiwa kuchukua hatua hii kufuatia utafiti uliofanyika mapema mwaka huu kubaini kuwa wanafunzi wa kike ndio wanaathirika zaidi kutokana na matatizo yanayozikabili shule za sekondari za kata nchini.
Walimu, wanafunzi na wazazi waliohojiwa katika utafiti huo uliofanyika katika mikoa 20 nchini ikiwepo 16 ya Tanzania Bara na minne ya Zanzibar walisema serikali inapaswa kutimiza wajibu wake kuhakikisha matatizo yanayozikabili shule za kata yanatatuliwa.
Utafiti huo unaonyesha shule nyingi za sekondari za kata zina upungufu mkubwa wa walimu, wanafunzi hawapati chakula, hakuna vitabu na wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenye mazingira hatarishi.
Tatizo kubwa lililojitokeza katika utafiti huo ni upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi. Shule zote za kata zinakabiliwa na upungufu wa walimu. Mifano:
a) Shule ya Sekondari Uleling’ombe, Wilaya ya Kilosa, mkoa wa Morogoro, ina mwalimu mmoja tu, anayefundisha vidato vyote. Shule ya Sekondari Gongwe ina walimu watatu tu, na miongoni mwao, mmoja tu ndiye anafundisha masomo yote ya sayansi.

b) Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Rukwa: Mpanda inahitaji walimu 640. Hivi sasa ina walimu 162; na upungufu wa walimu 478. Haina walimu wa masomo ya sayansi.

c) Wilaya ya Kisarawe, mkoa wa Pwani ina walimu 243, na upungufu wa walimu 221. Walimu waliopungua ni wa masomo ya sayansi - Fizikia, Kemia, Baolojia na Hisabati. Wilaya imeleta walimu wapya 56. Kati ya hao, walimu sita (6) ndio wanaweza kufundisha masomo ya sayansi.

d) Katika Skuli ya Gamba, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja hakuna mwalimu hata mmoja wa masomo ya Fizikia, Hisabati na Kemia. Kuna mwalimu mmoja tu wa sayansi, anayefundisha somo la Baolojia kwa madarasa 10, kidato cha kwanza hadi cha nne.

e) Shule ya Sekondari ya Bahi, Wilaya ya Bahi, Mkoa wa Dodoma ina mwalimu mmoja wa sayansi anayefundisha fizikia kwa wanafunzi 376 wa kidato cha kwanza hadi cha nne.

f) Wilaya ya Bariadi ina upungufu wa walimu 226 ili kufikia mahitaji halisi ya walimu 640. Katika shule 10 za Wilaya ya Bariadi zilizotafitiwa, kuna jumla ya walimu 77, na upungufu wa jumla ya walimu 136.

g) Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora ina uhaba mkubwa wa walimu, na ina shule zenye mwalimu mmoja mmoja wanaofundisha masomo yote (mfano Shule ya Sekondari Nguvumoja) na nyingine zina walimu wawili wanaofundisha masomo yote shule nzima (mfano Shule ya Sekondari Bukoko).

Utafiti huo ulibaini kuwa baadhi ya matatizo makubwa yanayofanya walimu kuzikimbia shule za kata ni pamoja na mishahara yao kucheleweshwa, na mazingira magumu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa nyumba za kuishi, ukosefu wa maji, barabara za kufika kwenye shule hizo na umeme ambao ni muhimu kwa kijisomea na matumizi mengine yakiwemo mawasiliano ya simu za mkononi.

Imebainika kuwa baadhi ya wanafunzi ambao wengi ni watoto wenye umri chini ya miaka 18, kutokana na shule kuwa mbali, hulazimika kupanga vyumba na kuishi wenyewe bila uangalizi wa shule au wazazi; na hivyo kuwa katika hatari ya kufeli masomo, kupata mimba na kupata maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU).

Utafiti huo ulioandaliwa na TAMWA kwa kushirikiana na vyombo vya habari ulibaini kuwa katika baadhi ya shule kuna wanafunzi wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 15 kwa siku - kwenda na kurudi shuleni - huku wakiwa wanakatisha kwenye vichaka, misitu, mabonde na milima, na hivyo kuwa katika hatari ya kubakwa.

Utafiti huu ulifanywa kwa lengo la kuliwezesha taifa kubaini mambo yanayochangia wanafunzi wengi wa shule za kata kufeli na wengine wengi kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali ili serikali, wananchi na wadau wote wa elimu wachukue hatua kurekebisha hali hiyo.

Utafiti ulifanyika katika wilaya moja kila mkoa na zilitembelewa shule kati ya saba hadi 10 kila wilaya na kuzungumza na wanafunzi wa kike na wa kiume, walimu, wazazi, na viongozi mbalimbali.

Wanafunzi waliohojiwa walisema kwa kiwango kikubwa tatizo la wanafunzi kufeli na kukatisha masomo kutokana na mimba kwa kiasi kikubwa kunachangiwa na shule kukosa walimu, chakula, vitabu na mabweni yasiyo ya kulipia kwa wanafunzi wanaotoka mbali.

Sheria ya Kudhibiti makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 imeweka bayana kwamba mtu yeyote atakayefanya mapenzi na msichana mwenye umri chini ya miaka 18 atakuwa anatenda kosa la jinai la ubakaji.

Lakini utafiti ulibaini kuwa tatizo la wanafunzi wa sekondari za kata kubakwa ni kubwa. Kwa mfano katika Shule ya Sekondari Nasuri, wilayani Namtumbo, mkoani Rukwa yenye wanafunzi 691, ilibainika kuwa mwaka jana 2011 pekee, wanafunzi 26 walipata mimba na kukatisha masomo. Mkoa wa Shinyanga mwaka huo wanafunzi 51 walipata mimba wakati Tabora wanafunzi 41 nao walikumbwa na janga hilo. Aidha ilibainika kuwepo changamoto za kuweka kumbukumbu za matumio ya mimba.

Vile vile tatizo la kufeli lilionekana kubwa katika shule zaidi ya 150 za Tanzania Bara ambazo zilifanyiwa utafiti na idadi ya wanafunzi waliofeli katika mtihani wa taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012 ni wasichana.

Tanzania Bara wilaya zilizohusishwa kwenye utafiti na mikoa yake kwenye mabano ni Kilindi (Tanga) Bahi (Dodoma) Igunga (Tabora), Bariadi (Shinyanga) Kisarawe (Pwani), Namtumbo (Ruvuma), Rombo (Kilimanjaro) Lindi Vijijini (Lindi), Mtwara Newala (Mtwara), Muleba (Kagera), Kilosa (Morogoro), Manyoni (Singida), Kiteto (Manyara), Longido (Arusha), Sengerema (Mwanza) na Sumbawanga Vijijini (Rukwa).

Zanzibar wilaya za utafiti zilikuwa Chake Chake (Kaskazini Pemba), Micheweni (Kusini Pemba), Kati (Kusini Unguja), Kaskazini A (Kaskazini Unguja).

Ananilea Nkya
Mkurugenzi Mtendaji TAMWA

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...