FOLLOWERS

Sunday, June 3, 2012

MAHMOUD MGIMWA NA CHARLES IKEREGE KATIKA UTATA

Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini na mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge inayoshughulikia viwanda na biashara mheshimiwa Mahmoud Mgimwa
Aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa TBS Charles Ikerege wa kwanza kushoto
www.freemedia.co.tz/daima/habari

Kwa mujibu wa habari ya jumapil ikatika gazeti la Tanzania daima iliyoandikwa na Asha Bani MKURUGENZI wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege aliyesimamishwa kazi, anaelekea kulivuruga Bunge na kusababisha mgongano wa kimamlaka.
Kuibuka kwa mvurugano huo kunatokana na hatua ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa kusafiri kwenda nje ya nchi na menejimenti ya TBS pasipo kupata baraka au kibali cha Spika wa Bunge.
Mbali ya hilo, Mgimwa ambaye hivi karibuni alituhumiwa kuandaa ripoti ya kumsafisha mkurugenzi huyo wa TBS baada ya ziara hiyo, ameibuka na kukana kupata kufanya hivyo.
Sambamba na hayo, hali ya mkorogano ndani ya Bunge imeongezwa na hatua ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuibuka na kueleza kutojua chochote kuhusu ziara hiyo wala ripoti iliyokuwa na mwelekeo wa kumsafisha Ekelege ambaye hivi karibuni aliibua mjadala mkali bungeni.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Spika Makinda alisema alikuwa hana taarifa zozote kuhusu suala hilo wala safari ya Mgimwa kwenda Japan na China akiwa ameongozana na menejimenti ya TBS.
“Mgimwa alisafiri kama Mgimwa. Mimi Spika sina taarifa na wala ofisi yangu haijampa kibali, na sitambui wala sijui ameendajeendaje huko, labda akwambie yeye, maana sisi tuna utaratibu wetu,” alisema Makinda.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Mgimwa alikiri kusafiri na timu hiyo ya watu 14 kutoka TBS katika kipindi cha kati ya Mei 6 na 14 mwaka huu, lakini akasema yeye alienda huko kwa ajili ya kujifunza na si kufanya uchunguzi kama ilivyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Kuhusu kutopata ridhaa ya Spika au kibali chake, Mgimwa ambaye ni mbunge wa Mufindi Kaskazini, alisema ziara hiyo aliyoiita ya kujifunza, ilikuwa haina uhusiano wowote na shughuli za Kamati ya Bunge Viwanda na Biashara.
Mbali ya hilo, Mgimwa alikana kuandaa ripoti yoyote kwa niaba ya kamati yake ambayo pamoja na mambo mengine, ilikuwa ikimsafisha Ekelege, na akasema iwapo kulikuwa na taarifa yoyote basi ilitolewa na TBS wenyewe ambao ndio waliomwalika katika ziara hiyo.
“Mwandishi labda nikueleweshe hiyo isije kuleta matatizo. Mimi nilienda kama mimi kujifunza na wala kuhusu ripoti mimi sijui kwa kuwa sikuiandika. Waulizeni TBS ambao ndio waliandika na kamati yangu haihusiki kwa lolote na wala yenyewe haikufanya ziara.
“Ni kweli nilienda Japan na menejimenti hiyo na nilialikwa kama mtu binafsi na kwamba hakuna ripoti yoyote niliyoandika, pengine kama imeandikwa na TBS wenyewe, hivyo waulizwe hiyo ripoti wao. Sikwenda kumsafisha mtu mimi,” alisema Mgimwa.
Hata hivyo, ripoti iliyotolewa na TBS yenye mwelekeo wa kumsafisha Ekelege na taasisi yake, ambayo Tanzania Daima Jumapili iliiona nakala yake, inaeleza kuridhishwa na namna mawakala wa shirika hilo wanavyofanya kazi nzuri katika nchi za China na Japan.
Akifafanua zaidi, Mgimwa kutokana na uzoefu alioupata, anaamini kuna haja kwa wajumbe wa kamati yake kwenda katika nchi zenye ofisi za TBS kwa ajili ya kujifunza, na kwamba alikuwa akitarajia kutuma maombi kwa Spika ili awape ruhusa waende wakaangalie sheria mbalimbali kama zinafaa au la.
Habari kutoka ndani ya duru za kamati za Bunge zinaeleza kwamba, hatua hiyo ya Mgimwa inaonekana kuchukua mwelekeo tofauti na unaokinzana na ule uliochukuliwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), ambayo katika ripoti yake kwenye mkutano uliopita wa Bunge, iliibua shutuma nzito dhidi ya TBS na mkurugenzi wake, Ekelege.
Taarifa hiyo ya POAC ambayo ilimbana pia aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami kwa tuhuma za kumlinda Ekelege, iliibua kile kilichoonekana kuwa ni uoza ndani ya TBS, ambayo ilibainika kuwa na ofisi hewa katika baadhi ya mataifa ambako ilikuwa ikidai kukagua ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini.
Ripoti hiyo ya POAC ambayo ilimlaumu Chami kwa kushindwa kumsimamisha kazi au kumwajibisha Ekelege, ilitokana na ziara walizofanya baadhi ya wajumbe wake waliotembelea Hong Kong na Singapore na kubaini kasoro hizo.
Siku chache tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Dk. Abdallah Kigoda kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, waziri huyo alitangaza kumsimamisha kazi Ekelege na kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...